The chat will start when you send the first message.
1Jawabu la upole hugeuza hasira;
Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.
2Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri;
Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.
3Macho ya BWANA yako kila mahali;[#2 Nya 16:9; Ayu 34:21; Mit 5:21; Yer 16:17; Zek 4:10; Ebr 4:13]
Yakimchunguza mbaya na mwema.
4Ulimi safi ni mti wa uzima;
Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.
5Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye;
Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.
6Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;
Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.
7Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa;
Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.
8Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;[#Isa 61:8; Yer 6:20; Amo 5:22; Lk 18:11]
Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.
9Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;[#Mit 21:21; Isa 51:1,7; 1 Tim 6:11]
Bali humpenda mtu afuatiaye wema.
10Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;
Naye achukiaye kukemewa atakufa.
11Kuzimu na Uharibifu viko wazi mbele za BWANA;[#Yn 2:24; Mdo 1:24]
Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?
12Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa;
Wala yeye hawaendei wenye hekima.
13Moyo wa furaha huchangamsha uso;
Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.
14Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa;
Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.
15Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya;
Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.
16Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA;[#Mit 16:8; Mhu 4:6; 1 Tim 6:6]
Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.
17Chakula cha mboga palipo na upendo;
Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.
18Mtu wa hasira huchochea ugomvi;
Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.
19Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba;
Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.
20Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;
Bali mpumbavu humdharau mamaye.
21Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili;[#Efe 5:15]
Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.
22Pasipo ushauri mipango vuhunjika;
Bali kwa wingi wa washauri huthibitika.
23Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake;
Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!
24Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;[#Flp 3:20]
Ili atoke katika kuzimu chini.
25BWANA ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi;
Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.
26Ushauri mbaya ni chukizo kwa BWANA;
Bali maneno yapendezayo ni safi.
27Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;[#Yos 6:18; 1 Sam 8:3; Mit 1:19; Isa 5:8; Zek 5:3]
Bali achukiaye zawadi ataishi.
28Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu;[#1 Pet 3:15]
Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.
29BWANA yuko mbali na wasio haki;[#Efe 2:12; Zab 34:15,16; Yn 9:31; Rum 8:26]
Bali huisikia sala ya mwenye haki.
30Mng'ao wa macho huufurahisha moyo;
Habari njema huinenepesha mifupa.
31Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai
Litakaa kati yao wenye hekima.
32Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe;
Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.
33Kumcha BWANA ni maonyo ya hekima;
Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.