The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo niliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake.[#Ufu 10:1; Eze 43:2]
2Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ulio mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;[#Isa 13:21; 21:9; 34:11; Yer 9:11; 50:39; 51:8; Ufu 14:8; Dan 4:30]
3kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.[#Isa 23:17; Yer 25:15,27; 51:7; Nah 3:4]
4Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.[#Isa 48:20; 52:11; Yer 50:8; 51:6,9,45]
5Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.[#Mwa 18:20-21; Yer 51:9]
6Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni mara mbili.[#Zab 137:8; Yer 50:15,29; 2 The 1:6]
7Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.[#Isa 47:7-9; Yer 50:29]
8Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.[#Isa 47:9; Yer 50:34; Ufu 17:16]
9Na hao wafalme wa nchi, waliozini naye na kufanya anasa pamoja naye, watalia na kumwombolezea; wauonapo moshi wa kuungua kwake;[#Eze 26:16-17; #Eze 27:30-35; Isa 23:17; Ufu 17:2]
10wakisimama mbali kwa hofu ya maumivu yake, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu, Babeli, mji ule ulio na nguvu! Kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja.[#Dan 4:30; Eze 26:17; Isa 21:9; Yer 51:8; Ufu 14:8]
11Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena;[#Eze 27:31,36]
12bidhaa ya dhahabu, fedha, vito vyenye thamani, lulu, kitani nzuri, nguo ya rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, kila chombo cha pembe, kila chombo cha mti wa thamani nyingi, cha shaba, cha chuma na cha marimari;[#Eze 27:12-13,22]
13na mdalasini, iliki, uvumba, marhamu, ubani, mvinyo, mafuta ya mzeituni, unga mzuri na ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari, na miili na roho za wanadamu.[#Eze 27:13]
14Na matunda yaliyotamaniwa na roho yako yamekuondokea; na vitu vyote vilivyo laini na vitu vya fahari vimekupotea; wala watu hawataviona tena kamwe.
15Na wafanya biashara ya vitu hivyo, waliopata mali kwake, watasimama mbali, kwa hofu ya maumivu yake; wakilia na kuomboleza,[#Eze 27:31,36]
16wakisema, Ole, ole, mji ule mkuu! Uliovikwa kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na nguo nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na vito vya thamani, na lulu;[#Ufu 17:4]
17kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa. Na kila nahodha na kila aendaye mahali popote kwa matanga, na mabaharia, nao wote watendao kazi baharini, wakasimama mbali;[#Isa 23:14; Eze 27:26-30]
18wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio kama mji huu mkubwa![#Eze 27:32; Isa 34:10]
19Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa.[#Eze 26:19; 27:30-34]
20Furahini juu yake, enyi mbingu, na enyi watakatifu, mitume na manabii; kwa maana Mungu ametoa hukumu kwa ajili yenu juu yake.[#Kum 32:43; Yer 51:48; Isa 44:23]
21Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa.[#Yer 51:63-64; Eze 26:21; Dan 4:30]
22Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikika ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yoyote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa;[#Eze 26:13; Isa 24:8; #Yer 7:34; 25:10]
23wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana arusi na bibi arusi haitasikika ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako.[#Yer 7:34; 16:9; 25:10; Isa 23:8; 47:9]
24Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.[#Yer 51:9,49; Mt 23:35; Ufu 6:10; 17:6; 19:2]