Wimbo ulio Bora 6

Wimbo ulio Bora 6

Uzuri wa bibi arusi usio na kifani

1Mpendwa wako amekwenda wapi,[#Wim 1:8]

Wewe uliye mzuri katika wanawake?

Mpendwa wako amegeukia upande upi,

Ili tumtafute pamoja nawe?

2Mpendwa wangu ameshukia bustani yake,[#Isa 40:11; Sef 3:17; Ufu 7:17; Isa 56:8; Yn 10:16]

Kwenye matuta ya rihani;

Ili kulisha penye bustani,

Ili kuchuma nyinyoro.

3Mimi ni wake mpendwa wangu, naye ni wangu,[#Wim 2:16; Ufu 21:2]

Hulisha kundi lake penye nyinyoro.

4Mpenzi wangu, u mzuri kama Tirza,[#2 Kor 10:4]

Mwenye kupendeza kama Yerusalemu,

Wa kutisha kama jeshi lenye bendera.

5Uyageuzie macho yako mbali nami,[#Wim 4:1]

Kwa maana yamenitisha sana.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi,

Wakijilaza mbavuni pa Gileadi.

6Meno yako kama kundi la kondoo,

Wakipanda kutoka kuoshwa;

Ambao kila mmoja amezaa mapacha,

Wala hakuna aliyefiwa kati yao.

7Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga,

Nyuma ya barakoa yako.

8Wako malkia sitini, na masuria themanini,

Na wanawali wasiohesabika;

9Hua wangu, mkamilifu wangu, ni mmoja tu,

Mtoto wa pekee wa mamaye.

Ndiye kipenzi chake aliyemzaa,

Binti wakamwona wakamwita heri;

Malkia na masuria nao wakamwona,

Wakamsifu, wakisema,

10Ni nani huyu atazamaye kama alfajiri,

Mzuri kama mwezi, safi kama jua,

Wa kutisha kama wenye bendera?

11Nilishukia katika bustani ya milozi,[#Wim 7:12]

Ili kuyatazama machipuko ya bondeni;

Nione kama mzabibu umechanua,

Kama mikomamanga imetoa maua.

12Kabla sijajua, roho yangu ilinileta

Katikati ya magari ya wakuu wangu.

13Rudi, rudi, Mshulami,

Rudi, rudi, ili sisi tukutazame.

Kwani mnataka kumtazama Mshulami,

Kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya