Wimbo ulio Bora 8

Wimbo ulio Bora 8

1Laiti ungekuwa kama ndugu yangu,

Aliyeyanyonya matiti ya mamangu!

Kama ningekukuta huko nje,

Ningekubusu, asinidharau mtu.

2Ningekuongoza nyumbani mwa mamangu,[#Mit 9:2]

Naye angenifundisha;

Ningekunywesha divai iliyokolea,

Divai mpya ya mkomamanga wangu.

3Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu,[#Wim 2:6; Isa 62:4,5; 2 Kor 12:9]

Nao wa kulia ungenikumbatia.

4Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,

Msiyachochee mapenzi, au kuyaamsha,

Hadi yatakapokuwa tayari.

Kurudi nyumbani

5Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani,[#Yn 17:14]

Akimtegemea mpendwa wake?

Nilikuamsha chini ya huo mpera;

Huko mama yako alikuonea uchungu,

Aliona uchungu aliyekuzaa.

6Nitie kama mhuri moyoni mwako,[#Isa 49:16; Yer 22:24; Hag 2:23; Flp 3:8]

Kama mhuri juu ya mkono wako;

Kwa maana upendo una nguvu kama mauti,

Na wivu ni mkali kama ahera.

Mwako wake ni mwako wa moto,

Na miali yake ni miali ya Yahu.

7Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,[#Mit 6:35]

Wala mito haiwezi kuuzamisha;

Kama mtu angetoa badala ya upendo

Mali yote ya nyumbani mwake,

Angedharauliwa kabisa.

8Kwetu sisi tuna dada mdogo,[#Zab 22:27]

Wala hana matiti;

Tumfanyieje dada yetu,

Siku atakapoposwa?

9Kama akiwa tu ukuta,[#Ufu 3:20]

Tumjengee buruji za fedha;

Na kama akiwa ni mlango,

Tumhifadhi kwa mbao za mierezi.

10Mimi nilikuwa ukuta,[#Kol 2:7; Eze 16:7]

Na matiti yangu kama minara;

Ndipo nikawa machoni pake

Kama mtu aliyeipata amani.

11Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-hamomi[#Mt 21:33]

Akawakodisha walinzi hilo shamba lake la mizabibu;

Kila mtu atoe vipande elfu moja vya fedha kwa matunda yake.

12Shamba langu la mizabibu, lililo langu mimi, liko mbele yangu.

Basi, Sulemani, wewe uwe na elfu zako,

Na hao wayalindao matunda yake wapewe mia mbili.

13Wewe ukaaye bustanini,[#Wim 2:14]

Hao rafiki huisikiliza sauti yako;

Unisikizishe mimi.

14Ukimbie, mpendwa wangu,[#Wim 2:17]

Nawe uwe kama paa, au ayala,

Juu ya milima ya manukato.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya