1 Mambo ya Nyakati 13

1 Mambo ya Nyakati 13

Sanduku la Agano laletwa kutoka Kiriath-yearimu

1Kisha Daudi akafanya shauri na makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, naam, na kila kiongozi.[#2 Sam 5:1; 6:1; 1 Fal 8:1; 1 Nya 12:14; Zab 132:1; Mit 15:22]

2Daudi akawaambia jamii yote ya Israeli, Likiwa jema kwenu, tena likiwa limetoka kwa BWANA, Mungu wetu, na tutume watu huku na huku mahali pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi yote ya Israeli, ambao pamoja nao makuhani na Walawi wamo ndani ya miji yao yenye viunga, ili wakusanyike kwetu;[#1 Nya 10:7; Isa 37:4]

3nasi tujirudishie tena sanduku la Mungu wetu; maana hatukulitilia maanani katika siku za Sauli.[#1 Sam 7:1; 14:18; 23:2,4]

4Nao jamii nzima wakasema ya kwamba watafanya hivyo; kwa kuwa neno hilo lilikuwa jema machoni pa watu wote.

5Basi Daudi akawakusanya Israeli wote, toka Shihori, kijito cha Misri, hadi pa kuingilia Hamathi, ili walilete sanduku la Mungu kutoka Kiriath-yearimu.[#2 Sam 6:1; Yos 13:3; 1 Sam 6:21; 7:1]

6Basi Daudi akapanda, yeye na Israeli wote, mpaka Baala, ndio Kiriath-yearimu, ulio wa Yuda, ili kulileta toka huko sanduku la Mungu, BWANA akaaye juu ya makerubi, lililoitwa kwa Jina lake.[#Yos 15:9,60; Kut 25:22; 1 Sam 4:4]

7Wakalipandisha sanduku la Mungu juu ya gari jipya kutoka nyumba ya Abinadabu; na Uza na Ahio wakaliendesha lile gari.[#Hes 4:15]

8Wakacheza Daudi na Israeli wote, mbele za Mungu, kwa nguvu zao zote; na kwa nyimbo na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta.[#2 Sam 6:5]

9Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walijikwaa.[#2 Sam 6:6]

10Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hadi akafa pale pale mbele za Mungu.[#Hes 4:15; 1 Nya 15:13,15; Law 10:2]

11Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.[#13:11 Tazama 2 Sam 6:8]

12Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu?

13Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.

14Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.[#2 Sam 6:11; Mwa 30:27; 39:5; 1 Nya 26:5; Zab 37:22; Mit 3:9; 10:22; Mal 3:10]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya