1 Mambo ya Nyakati 14

1 Mambo ya Nyakati 14

Daudi ajiimarisha katika Yerusalemu

1Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.[#2 Sam 5:11; 1 Fal 5:1-12]

2Daudi akajua ya kwamba BWANA amemweka imara ili atawale Israeli, na kwamba milki yake imetukuka zaidi kwa ajili ya watu wake Israeli.

3Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi kuzaa wana na binti.[#Kum 17:14-17]

4Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;[#2 Sam 5:14; 1 Nya 3:5]

5na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;

6na Noga, na Nefegi, na Yafia;

7na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.

Kushindwa kwa Wafilisti

8Wafilisti waliposikia ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme wa Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.[#2 Sam 5:17; 1 Nya 11:3; Zab 2:1-5]

9Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya katika bonde la Warefai.[#1 Nya 11:15]

10Daudi akamwuliza Mungu, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye BWANA akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.

11Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, BWANA amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.

12Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.

13Lakini hao Wafilisti wakajitawanya tena mara ya pili bondeni.[#2 Sam 5:22]

14Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; zunguka mbali nao, na kuwajia ukielekea miforsadi.[#Yos 8:6,7; 2 Sam 5:23]

15Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.

16Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.[#2 Sam 5:25]

17Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye BWANA akawaletea mataifa yote hofu yake.[#Yos 6:27; 2 Nya 26:8; Kum 2:25; 11:25]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya