The chat will start when you send the first message.
1Mniige mimi kama mimi ninavyomwiga Kristo.[#1 Kor 4:16; Flp 3:17]
2Basi nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vile vile kama nilivyowatolea.
3Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.[#1 Kor 3:23; Efe 5:23; Mwa 3:16]
4Kila mwanamume, asalipo, au anapotoa unabii, naye amefunikwa kichwa, anaaibisha kichwa chake.[#1 Kor 12:10; 14:1]
5Bali kila mwanamke asalipo, au anapotoa unabii, bila kufunika kichwa, anaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa.
6Maana mwanamke asipojifunika kichwa, na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunike kichwa.
7Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.[#Mwa 1:26-27; 5:1]
8Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume.[#Mwa 2:18-23; 1 Tim 2:13]
9Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume.
10Kwa hiyo imempasa mwanamke awe na dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika.[#Mwa 6:2]
11Lakini, katika Bwana si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke.
12Maana kama mwanamke alitoka katika mwanamume, vile vile mwanamume naye huzaliwa na mwanamke; na vitu vyote asili yake hutoka kwa Mungu. Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu.
13Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunika kichwa?
14Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake?
15Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi.
16Lakini mtu yeyote akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu.
17Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara.
18Kwa maana kwanza mnapokutanika kanisani nasikia kuna migawanyiko kwenu; nami kwa kiasi fulani naamini;[#1 Kor 1:10-12; 3:3]
19kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu.[#1 Yoh 2:19; Kum 13:3]
20Basi mnapokutanika pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana;
21kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa.
22Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo.[#Yak 2:5,6]
23Kwa maana mimi nilipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,[#Mt 26:26-28; Mk 14:22-24; Lk 22:19,20]
24naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
25Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.[#Kut 24:6-8; Yer 31:31-34; Zek 9:11]
26Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.[#Mt 26:29]
27Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.[#Ebr 6:6; 10:29]
28Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.[#Mt 26:22; 2 Kor 13:5]
29Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.
30Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio wagonjwa na dhaifu, na watu kadhaa wamelala.[#1 Kor 15:20; Efe 5:14; 1 The 5:6]
31Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa.
32Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.[#Ebr 12:5,6]
33Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutanika mpate kula, ngojaneni;
34mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nikija nitayatengeneza.