1 Wakorintho 12

1 Wakorintho 12

Karama za Roho

1Basi, ndugu zangu, kuhusu karama za roho, sitaki mkose kufahamu.

2Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa.[#Hab 2:18,19]

3Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu.[#Mk 9:39; Mt 7:21; 1 Yoh 4:2,3]

4Basi kuna karama tofauti; bali Roho ni yeye yule.[#Rum 12:6-8; Efe 4:4]

5Tena kuna huduma tofauti, na Bwana ni yeye yule.[#Efe 4:11]

6Kisha kuna uwezo tofauti wa kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

7Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.[#1 Kor 14:26]

8Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;

9mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;

10na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine fasiri za lugha;[#1 Kor 14:5; Mdo 2:4]

11lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.[#Rum 12:3; Efe 4:7; 1 Kor 7:7]

Mwili mmoja wenye viungo vingi

12Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.[#Rum 12:4-5; 1 Kor 10:17]

13Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wagiriki; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.[#Gal 3:28]

14Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.

15Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Unakuwa si wa mwili kwa sababu hiyo?

16Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si wa mwili; je! Linakuwa si la mwili kwa sababu hiyo?

17Kama mwili wote ukiwa jicho, kuko wapi kusikia? Kama wote ni sikio kuko wapi kunusa?

18Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.

19Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?

20Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.

21Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.

22Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vinahitajiwa zaidi.

23Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile tunavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.

24Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa;

25ili kusiwe na mgawanyiko katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.

26Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

27Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na kila mmoja wenu akiwa kiungo cha mwili huo.[#Rum 12:5; Efe 5:30]

28Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, aina za usaidizi, maongozi na aina za lugha.[#Efe 4:11,12]

29Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?

30Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?

31Jitahidini sana kupata karama zilizo kuu. Na nitawaonesheni njia iliyo bora zaidi.[#1 Kor 14:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya