The chat will start when you send the first message.
1Kuhusu ile michango kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo hivyo.[#Rum 15:25-26; Mdo 11:29; Gal 2:10; 2 Kor 8:9]
2Siku ya kwanza ya juma kila mmoja wenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;[#Mdo 20:7]
3nami nitakapofika nitawatuma kwa barua wale mtakaowachagua, wachukue hisani yenu mpaka Yerusalemu.
4Na kama ikifaa niende na mimi, watasafiri pamoja nami.
5Lakini nitakuja kwenu, nikiisha kupita kati ya Makedonia; maana napita kati ya Makedonia.[#Mdo 19:21]
6Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha kokote nitakakokwenda.[#Rum 15:24; Tit 3:12]
7Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu natarajia kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia.[#Mdo 20:2; 18:21]
8Lakini nitakaa Efeso hadi siku ya Pentekoste;[#Law 23:15-21; Kum 16:9-11; Mdo 19:1,10; #Mdo 19:8-10]
9kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.[#2 Kor 2:12; Kol 4:3; Ufu 3:8]
10Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe;[#1 Kor 4:17; Flp 2:20]
11basi mtu yeyote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu.[#1 Tim 4:12]
12Lakini kuhusu Apolo, ndugu yetu, nilimsihi sana aje kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi.[#1 Kor 1:12; 3:6]
13Kesheni, simameni imara katika imani, iweni na ujasiri, mkawe hodari.[#Zab 31:24; Efe 6:10]
14Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.
15Tena ndugu, nawasihi; (mnawajua watu wa nyumbani mwa Stefana kwamba ni malimbuko ya Akaya, nao wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watakatifu);[#1 Kor 1:16; Rum 16:5]
16watiini watu kama hawa, na kila mtu afanyaye kazi pamoja nao, na kujitaabisha.[#Flp 2:29]
17Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu.
18Maana wameniburudisha roho yangu, na roho zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao.[#1 The 5:12]
19Makanisa ya Asia wawasalimu. Akila na Priska wawasalimu sana katika Bwana, pamoja na kanisa lililoko ndani ya nyumba yao.[#Mdo 18:2,18,26; Rum 16:3,5]
20Ndugu wote wawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.[#Rum 16:16; 2 Kor 13:12; 1 Pet 5:14]
21Hii ni salamu yangu Paulo kwa mkono wangu mwenyewe.[#Kol 4:18; 2 The 3:17]
22Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maranatha.[#Gal 1:8,9; #16:22 maana yake ni, Bwana wetu anakuja.]
23Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.
24Pendo langu na liwe pamoja nanyi nyote katika Kristo Yesu.