1 Wakorintho 8

1 Wakorintho 8

Vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu

1Na kuhusu vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.[#Mdo 15:29]

2Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lolote bado, kama impasavyo kujua.[#Gal 6:3]

3Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye.[#Gal 4:9]

4Basi kuhusu kuvila vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu.[#1 Kor 10:19; Kum 6:4]

5Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi;[#Zab 82:6; Yn 10:34]

6lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.[#Mal 2:10; Kol 1:16; 1 Kor 12:5,6]

7Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika.[#1 Kor 10:27]

8Lakini chakula hakitupeleki karibu na Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.[#Rum 14:17]

9Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaza wale walio dhaifu.[#Gal 5:13]

10Kwa maana, mtu akikuona wewe uliye na ujuzi, umeketi chakulani ndani ya hekalu la sanamu, je! Dhamiri yake mtu huyo, kwa kuwa yuko dhaifu, haitathibitika hata yeye naye ale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu?

11Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.[#Rum 14:15]

12Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo.

13Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.[#Rum 14:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya