1 Yohana 1

1 Yohana 1

Neno la uzima

1Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kuhusu Neno la uzima;[#Yn 1:1,14]

2(na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena tunashuhudia, na kuwahubiria ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);[#Yn 1:4,14]

3hilo tuliloliona na kulisikia, tunawahubiria na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.

4Na haya tunayaandika, ili furaha yetu itimizwe.[#Yn 15:11; 16:24]

Mungu ni nuru

5Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake.[#Yak 1:17]

6Tukisema ya kwamba tunashirikiana naye, huku tukienenda katika giza, tunasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;[#1 Yoh 2:4; Yn 3:21]

7bali tukienenda katika nuru, kama yeye alivyo katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.[#Ebr 9:14; Ufu 1:5; 7:14]

8Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani yetu.

9Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kututakasa na udhalimu wote.[#Mit 28:13]

10Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, tunamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo ndani yetu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya