1 Wafalme 10

1 Wafalme 10

Ziara ya malkia wa Sheba

1Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.[#2 Nya 9:1; Zab 72:10,15; Isa 60:6; Yer 6:20; Mt 12:42; Lk 11:31; Amu 14:12; Mit 1:6]

2Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni.

3Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno aliloshindwa mfalme asimwambie.[#Mit 1:5; Isa 50:4]

4Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga,

5na chakula cha mezani pake, na maofisa wake walivyokaa, na kuhudumu kwao wahudumu wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na sadaka zake za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia.[#1 Nya 26:16]

6Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.

7Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.

8Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.[#Mit 8:34]

9Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa BWANA amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.[#1 Fal 5:7; Kum 7:8; 2 Nya 2:11; Dan 2:21; 2 Sam 8:15; Zab 72:2; Mit 8:15]

10Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia moja na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.

11Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani.[#1 Fal 9:27; Ayu 22:24; 2 Nya 9:10]

12Mfalme akafanya kwa miti hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya BWANA, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo.[#2 Nya 9:11]

13Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

14Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita,

15zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya watawala wa nchi.[#2 Nya 9:24; Zab 72:10; Isa 21:13; Gal 4:25]

16Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu.

17Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya msitu wa Lebanoni.[#1 Fal 14:26; 7:2]

18Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.[#2 Nya 9:17; Ebr 1:3,8; Ufu 20:11]

19Kiti kile kilikuwa na ngazi sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huku na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.

20Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya ngazi sita huku na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wowote.

21Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.

22Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.[#Mwa 10:4; 1 Fal 22:48; 2 Nya 20:36; Zab 48:7; Isa 2:16]

23Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.

24Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.

25Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.[#2 Sam 8:2,10; Ayu 42:11; Zab 68:29; Mt 2:11]

26Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu moja mia nne, na wapandao farasi elfu kumi na mbili, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.[#Kum 17:16; 1 Fal 4:26; 2 Nya 1:14; 9:25]

27Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.[#2 Nya 1:15]

28Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake.[#Eze 27:7]

29Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia moja na hamsini; hivyo basi watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.[#Yos 1:4; 2 Fal 7:6]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya