1 Wafalme 12

1 Wafalme 12

Makabila kumi ya kaskazini yajitenga

1Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme.[#2 Nya 10:1]

2Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri,[#1 Fal 11:26,40]

3wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,

4Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.[#1 Sam 8:11-18; 1 Fal 4:7,22; 9:15; Ayu 20:19-23; Mit 3:31; Mhu 5:8; Isa 58:6; Eze 45:8; Amo 4:1,2; Mik 2:1,3; Mal 3:5; 1 The 4:6]

5Akawaambia, Nendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao.

6Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa?[#Ayu 12:12; 32:7; Mit 27:10; Mhu 10:4; Yer 42:2-5; 43:2]

7Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.[#2 Nya 10:7; Mit 15:1]

8Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake.

9Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako?

10Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.[#1 Fal 3:7; 14:21; 2 Nya 10:10,11; 22:4; Zab 7:16; 140:11; Mit 18:6,7; Isa 47:6]

11Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge.

12Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.

13Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa;

14akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge.

15Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa BWANA, ili alitimize neno lake, BWANA alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni.[#Amu 14:4; 1 Fal 22:23; 2 Nya 10:15; 22:7; Zab 5:10; Amo 3:6; 1 Fal 11:11]

16Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hakuwasikia, hao watu walimjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya! Nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Ee Daudi. Hivyo Israeli wakaenda zao hemani kwao.[#2 Sam 20:1]

17Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu aliwatawala wao.[#1 Fal 11:13; 2 Nya 10:17; 11:13-17]

18Ndipo mfalme Rehoboamu akampeleka Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, nao Israeli wote wakampiga kwa mawe hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda katika gari, ili akimbilie Yerusalemu.[#2 Sam 20:24; 1 Fal 4:6; 5:14; 2 Nya 10:13]

19Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.[#1 Sam 10:19; 2 Fal 17:21; 2 Nya 10:19]

Yeroboamu atawala Israeli

20Ikawa, Israeli wote waliposikia ya kwamba Yeroboamu amerudi, wakapeleka watu wakamwita aje mkutanoni, wakamfanya mfalme juu ya Israeli wote; wala hapakuwa na mtu aliyeshikamana na nyumba ya Daudi, ila kabila la Yuda peke yake.[#1 Fal 11:13]

21Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda, pamoja na kabila la Benyamini, watu wateule elfu mia moja themanini, waliokuwa watu wa vita, ili wapigane na nyumba ya Israeli, waurudishe ufalme tena kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.[#2 Nya 11:1]

22Lakini likaja neno la Mungu kwa Shemaya mtu wa Mungu, kusema,[#2 Nya 11:2]

23Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na jamaa yote ya Yuda na Benyamini, na watu waliosalia, ukisema,

24BWANA asema hivi, Msiende, wala msipigane na ndugu zenu wana wa Israeli; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakalisikiliza neno la BWANA, wakarudi, wakaenda zao, sawasawa na neno la BWANA.[#Mit 16:9]

25Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli.[#Mwa 12:6; Amu 9:45; Mwa 32:30,31; Amu 8:17]

26Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi.[#Zab 14:1; Rum 8:7]

27Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda.[#Kum 12:5; 16:2,6]

28Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akatengeneza ng'ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri.[#2 Fal 10:29; 17:16; Hos 8:4-7; Kut 32:4]

29Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani.[#Mwa 28:19; Hos 4:15; Amu 18:29]

30Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani.[#1 Fal 13:34; 2 Fal 17:21]

31Tena akafanya nyumba za mahali pa juu, akafanya na watu wowote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani.[#1 Fal 13:32,33; Hes 3:10; 2 Fal 17:32; 2 Nya 11:14; Eze 44:7]

32Yeroboamu akaamuru kuweko sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo hivyo katika Betheli akiwatolea dhabihu wale ng'ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya.[#Law 23:33; Hes 29:12; 1 Fal 8:2,5; Amo 7:13]

33Akatoa dhabihu juu ya ile madhabahu aliyoifanya katika Betheli, siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouwaza moyoni mwake mwenyewe; akawaamuru wana wa Israeli waishike sikukuu hiyo, akapanda kuiendea madhabahu, ili kufukiza uvumba.[#Hes 15:39; 1 Fal 13:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya