1 Wafalme 15

1 Wafalme 15

Abijamu atawala Yuda: Kuabudu sanamu na vita

1Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda.

2Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.[#2 Nya 11:21; 13:2]

3Akaziendea dhambi zote za babaye, alizozifanya kabla yake; wala moyo wake haukuwa mkamilifu na BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye.[#1 Fal 11:4; Zab 119:80]

4Lakini kwa ajili ya Daudi, BWANA, Mungu wake, akampa taa humo Yerusalemu, amwinue mwanawe baada yake, na kuufanya imara Yerusalemu;[#Mwa 12:2; 19:29; 2 Nya 21:7; Isa 37:35]

5kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa BWANA, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa kuhusu Uria, Mhiti.[#1 Fal 14:8; Lk 1:6]

6Basi kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote za maisha yake.[#15:6 Au, Abiya.]

7Na mambo yote ya Abiya yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.[#2 Nya 13:2,3,22]

8Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi. Akatawala Asa mwanawe mahali pake.[#2 Nya 14:1]

Asa atawala Yuda

9Mwaka wa ishirini wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala juu ya Yuda.

10Akatawala miaka arubaini na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.

11Basi, Asa akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu, kama alivyofanya babaye Daudi.[#2 Nya 14:2; 15:17]

12Akawafukuza mahanithi katika nchi, akaziondoa sanamu zote walizozifanya baba zake.[#1 Fal 14:21; 22:46]

13Hata na Maaka, mamaye, akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.[#Kum 13:6; 33:9; 2 Nya 15:16; Mt 10:37; 19:29; Lk 12:51,53; 14:26; Kut 32:20]

14Lakini mahali pa juu hapakuondoshwa; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu kwa BWANA siku zake zote.[#1 Fal 22:43; 2 Nya 15:17]

15Akavileta vile vitu alivyovitakasa baba yake, na vile alivyovitakasa yeye mwenyewe, katika nyumba ya BWANA, fedha; na dhahabu, na vyombo.

Ushirikiano na Shamu juu ya Israeli

16Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.

17Kisha, Baasha mfalme wa Israeli akashambulia Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu yeyote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.[#2 Nya 16:1; Yos 18:25; 1 Sam 15:34; 1 Fal 12:27]

18Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,[#1 Fal 20:1-5,33,34; 2 Fal 8:7-15; 2 Nya 16:2; Mwa 14:15; 1 Fal 11:23]

19Tumepatana mimi nawe, na baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea zawadi, fedha na dhahabu; basi nenda, uyavunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aache mashambulizi juu yangu.

20Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma wakuu wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli, akapiga Iyoni, na Dani, na Abel-beth-maaka na Kinerothi yote, na nchi yote ya Naftali.[#2 Fal 15:29; Amu 18:29; 2 Sam 20:14]

21Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo akaacha kuujenga Rama, akaenda akakaa Tirza.

22Ndipo mfalme Asa akatangaza kwa Yuda pia; asiachiliwe mtu; nao wakayachukua mawe ya Rama na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye mfalme Asa akajenga kwa vitu hivyo Geba wa Benyamini na Mispa.[#2 Nya 16:6; 1 Sam 8:16,17; Yos 21:17; 1 Sam 7:6]

23Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu.[#2 Nya 16:12; Zab 90:10; Mhu 12:1]

24Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.[#1 Fal 22:41-43; 2 Nya 17:1; Mt 1:8]

Nadabu atawala Israeli

25Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.

26Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.[#1 Fal 12:30]

27Basi Baasha wa Ahiya, wa ukoo wa Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.[#1 Fal 14:14; Yos 19:44; 21:23; 1 Fal 16:15]

28Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.[#Kum 32:35]

29Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi yeyote, hata alipomharibu sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;[#1 Fal 14:10,14; Ayu 18:13-21; Zab 21:10; 37:28,38; Isa 14:20]

30kwa sababu ya makosa yake Yeroboamu aliyoyakosa, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; kwa sababu ya chukizo lake alilomchukiza BWANA, Mungu wa Israeli, hata kumghadhibisha.

31Basi mambo yote ya Nadabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?

32Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.

Baasha atawala Israeli

33Katika mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya alianza kutawala juu ya Israeli wote huko Tirza, akatawala miaka ishirini na minne.

34Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA akaiendea njia ya Yeroboamu, na kosa lake ambalo kwa hilo aliwakosesha Israeli.[#1 Fal 12:28,29; 13:33; 14:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya