1 Wafalme 22

1 Wafalme 22

Israeli kuungana na Yuda juu ya Shamu

1Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli.[#22:1 yaani Ahabu]

2Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli.[#2 Nya 18:2,34]

3Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu?[#Kum 4:43]

4Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi wangu ni kama farasi wako.[#2 Fal 3:7]

5Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la BWANA.

6Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.[#1 Fal 18:19; Yer 28:1-17; Eze 13:1-23]

7Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii mwingine wa BWANA, ili tumwulize yeye?[#2 Fal 3:11]

8Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.[#1 Fal 19:10; 20:43]

9Ndipo mfalme wa Israeli akamwita ofisa, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla.

10Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao.

11Na Sedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike.

12Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.[#Yer 23:25-32]

Utabiri wa Mikaya

13Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema.

14Mikaya akasema, Kama BWANA aishivyo, neno lile BWANA aniambialo, ndilo nitakalolinena.[#Hes 22:38; Zab 118:6; Mit 28:1; Yer 1:7-19; Eze 2:3-8; Mdo 4:13-31; 9:29; Rum 8:31; 2 Kor 3:12; Gal 1:9,10; Efe 6:19,20; Flp 1:20; 1 The 2:2-6; 1 Tim 3:13; Tit 1:9,10; Ebr 13:5,6]

15Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.

16Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA?

17Akasema, Niliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.[#Mt 9:36]

18Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

19Mikaya akasema, Sikia basi neno la BWANA; Nilimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kulia na wa kushoto.[#Isa 6:1; Dan 7:9,10; Ayu 1:6; 2:1; Zab 103:20; Zek 1:10; Mt 18:10; Ebr 1:7,14]

20BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

21Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya.

22BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.[#Amu 9:23; Ayu 12:16; Eze 14:9; 2 The 2:11]

23Basi angalia, BWANA ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye BWANA amenena mabaya juu yako.[#Eze 14:9]

24Ndipo akakaribia Sedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya BWANA alitokaje kwangu ili aseme na wewe?[#Yer 28:16; 2 Nya 18:23]

25Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.[#1 Fal 20:30]

26Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme;

27mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.

28Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.[#Hes 16:29; Kum 18:20]

Kushindwa kwa Ahabu na kifo chake

29Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi.

30Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani.[#2 Nya 35:22]

31Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.

32Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga kelele.[#2 Nya 18:31; Mit 13:20]

33Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

34Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.[#2 Sam 15:11]

35Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha lake ndani ya gari.

36Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.

37Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.

38Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena.[#Kum 32:35; 1 Fal 21:19; 2 Fal 10:10; Zab 33:11; 119:89; Isa 14:27; 40:8; Nah 1:2; Mt 24:35; 1 Pet 1:25]

39Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?[#Amo 3:15]

40Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.

Yehoshafati atawala Yuda

41Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.[#2 Nya 20:31]

42Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.

43Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa BWANA. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu.[#2 Nya 17:3; 1 Fal 14:23; Kum 12:5-14; 2 Fal 12:3]

44Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.[#2 Nya 19:2; 2 Kor 6:14]

45Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?

46Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi.[#Mwa 13:13; 1 Fal 14:24; 15:12; Yud 1:7]

47Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme.[#Mwa 25:23; 2 Sam 8:14; 2 Fal 3:9; 8:20]

48Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; lakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi.[#1 Fal 10:22; 9:26; 2 Nya 20:35,37]

49Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali.

50Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.[#2 Nya 21:1]

Ahazia atawala Israeli

51Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli.

52Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli.[#1 Fal 15:26]

53Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake.[#Amu 2:11; 1 Fal 16:31]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya