1 Wafalme 4

1 Wafalme 4

Maofisa tawala wa Sulemani

1Basi mfalme Sulemani akawa mfalme juu ya Israeli wote.

2Na hawa ndio wakuu aliokuwa nao; Azaria mwana wa Sadoki, kuhani,

3Elihorefu na Ahiya, wana wa Shausha, waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe;[#2 Sam 8:16; #4:3 Au, mkumbushi.]

4na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa jemadari wa jeshi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;[#1 Fal 2:35; 2:27]

5na Azaria mwana wa Nathani alikuwa afisa mkuu tawala; na Zabudi mwana wa Nathani alikuwa kuhani, rafiki yake mfalme.[#2 Sam 8:18; 20:26; 15:37; 16:16; 1 Nya 27:33]

6Na Ahishari alikuwa mkuu wa kasri; na Adoramu mwana wa Abda alikuwa msimamizi wa shokoa.[#1 Fal 5:14]

7Sulemani alikuwa na maafisa tawala kumi na wawili juu ya Israeli wote, walioleta chakula cha mfalme na nyumba yake; kila mtu alikuwa na mwezi mmoja katika mwaka kuleta chakula.

8Na haya ndiyo majina yao. Mwana wa Huri, mlimani mwa Efraimu.

9Mwana wa Dekari, kutoka Makasi, na Shaalbimu na Beth-shemeshi na Elon-beth-hanani.

10Mwana wa Hesedi, katika Arubothi; na Soko ilikuwa kwake na nchi yote ya Heferi.

11Mwana wa Abinadabu katika Nafath-dori yote; ndiye aliyekuwa naye Tafathi binti Sulemani kuwa mke wake.

12Baana mwana wa Ahiludi, katika Taanaki na Megido, na Beth-sheani yote, iliyo kando ya Sarethani, chini ya Yezreeli, tangu Beth-sheani mpaka Abel-mehola, hata kupita Yokmeamu.

13Mwana wa Geberi katika Ramoth-gileadi; na kwake ilikuwa miji ya Yairi mwana wa Manase iliyomo Gileadi; na kwake ilikuwa wilaya ya Argobu, iliyomo Bashani, miji mikubwa sitini yenye kuta na makomeo ya shaba.[#Hes 32:41; Kum 3:4]

14Ahinadabu mwana wa Ido, katika Mahanaimu.

15Ahimaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani.

16Baana mwana wa Hushai, katika Asheri na Bealothi.

17Yehoshafati mwana wa Parua, katika Isakari.

18Shimei mwana wa Ela, katika Benyamini.

19Geberi mwana wa Uri, katika nchi ya Gileadi, nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani; naye alikuwa mkuu pekee katika nchi hiyo.[#Kum 3:8]

Utukufu wa utawala wa Sulemani

20Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi.[#Mwa 22:17; 1 Fal 3:8; Mit 14:28; 1 Sam 30:16; 1 Nya 12:39; Ayu 1:18; Zab 72:3; Mik 4:4; Zek 9:15; Mdo 2:46]

21Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake.[#Mwa 15:18; Kut 23:31; Kum 11:24; Yos 1:4; 2 Nya 9:26; Zab 72:8]

22Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori thelathini za unga mzuri, na kori sitini za ngano,[#4:22 Kori ni kipimo cha Kiebrania cha kadiri lita 220.]

23na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia moja, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona.

24Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote.[#Mwa 10:19]

25Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani.[#Kum 33:28,29; Zab 33:12; 144:12-15; Yer 23:6; Mik 4:4; Zek 3:10]

26Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi elfu arubaini kwa magari yake, na wapandao farasi elfu kumi na mbili.[#Kum 17:16; 1 Fal 10:25,26; 2 Nya 9:25; Zab 20:7]

27Na maofisa wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu.

28Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake.[#Est 8:14; Mik 1:13]

Sifa za hekima ya Sulemani

29Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.

30Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya watu wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.[#Mwa 25:6; Ayu 28:28; Mit 2:1; Mdo 7:22; #4:30 Katika Kiebrania ni wana wote.]

31Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.[#1 Nya 15:19; 6:33]

32Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.[#Mit 1:1; Mhu 12:9; Wim 1:1]

33Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

34Watu wakaja kutoka mataifa yote, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake, ili waisikie hekima ya Sulemani.[#1 Fal 10:1; 2 Nya 9:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya