1 Wafalme 7

1 Wafalme 7

Kasri ya Sulemani na majengo mengine

1Naye Sulemani alikuwa katika kuijenga nyumba yake mwenyewe miaka kumi na mitatu, akaimaliza nyumba yake yote.[#1 Fal 9:10; 10:17; 2 Nya 8:11]

2Kisha alijenga nyumba ya msitu wa Lebanoni; mikono mia moja urefu wake, na mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake, juu ya safu nne za nguzo za mwerezi, na mihimili ya mwerezi juu ya nguzo.

3Ikafunikwa juu kwa mwerezi juu ya mihimili arubaini na mitano, iliyokuwa juu ya nguzo; kumi na mitano kwa safu.

4Na madirisha yalikuwako safu tatu, mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

5Na milango yote na miimo ilikuwa ya mraba, ilivyoangaziwa; na mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

6Akaifanya baraza ya nguzo; mikono hamsini urefu wake, na mikono thelathini upana wake; na ukumbi mbele yake; na nguzo na mihimili minene mbele yake.

7Akaifanya baraza ya kiti cha enzi, ili ahukumu ndani yake, ndiyo baraza ya hukumu; nayo ikafunikwa mwerezi tangu sakafu mpaka dari.[#1 Fal 10:18; Zab 45:6; 110:1; Mit 20:8; 29:4; Isa 9:7]

8Nayo nyumba yake atakayokalia, katika behewa nyingine iliyokuwa ndani kupita baraza, ilikuwa ya kazi kama hiyo. Tena akamjengea nyumba binti Farao, (ambaye Sulemani alikuwa amemwoa), mfano wa ile baraza.[#Kum 17:16,17; 1 Fal 3:1]

9Hizi zote zilikuwa za mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, yaliyokatwa kwa misumeno, ndani na nje, tangu msingi hata mawe ya juu, na nje vile vile hata behewa kuu.

10Nao msingi ulikuwa wa mawe ya thamani, mawe makubwa, mawe mikono kumi, na mawe ya mikono minane.

11Na juu kulikuwa na mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, kulingana na cheo, na mierezi.

12Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya BWANA, na ukumbi wa nyumba.[#Yn 10:23; Mdo 3:11]

Mapambo Mazuri Kufuatana na Kazi ya Sonara Hiramu

13Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Hiramu kutoka Tiro.[#2 Nya 4:11; #7:13 Au, Huramu.]

14Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila la Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, stadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote.[#2 Nya 2:14; 4:16; Kut 31:3; 28:3; 36:1; Ayu 35:11; Isa 28:26; Dan 1:17; Lk 2:40]

15Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii.[#2 Fal 25:17; 2 Nya 3:15; 4:12; Yer 52:21]

16Akatengeneza mataji mawili ya shaba iliyoyeyushwa ya kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji la pili.

17Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji la pili.

18Hivyo akazitengeneza nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji la pili.

19Na mataji yaliyokuwa juu ya nguzo ukumbini yalikuwa ya kazi ya mayungi, mikono minne.

20Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji la pili.[#2 Fal 25:17; 2 Nya 3:16; 4:13; Yer 52:23]

21Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kulia, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi.[#2 Nya 3:17; Wim 3:10; Gal 2:9; Ufu 3:12; 1 Fal 6:3; #7:21 maana yake imedhaniwa kuwa Atathibitisha.; #7:21 maana yake imedhaniwa kuwa ‘imo nguvu.’]

22Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.

23Tena akatengeneza bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.[#2 Fal 25:13; 2 Nya 4:2; Yer 52:17; #7:23 Tangi kubwa lililotumiwa na makuhani kwa kuoga walipokuwa wakihudumu katika hekalu.]

24Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa katika kalibu hapo bahari ilipofanywa.[#2 Nya 4:3; #7:24 Tazama 7:23.]

25Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.[#2 Nya 4:4,5; Yer 52:20; Eze 1:10; Ufu 4:6,7; #7:25 Tazama 7:23.]

26Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili.[#2 Nya 4:5; #7:26 Bathi moja inakadiriwa kuwa huingia kama lita ishirini na mbili.]

27Akavifanya vile vitako kumi vya shaba; mikono minne urefu wa kitako kimoja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.

28Na kazi ya vitako ndiyo hii; vilikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio;

29na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng'ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na kitako; na chini ya simba na ng'ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza.[#Mwa 3:24; 1 Fal 6:27; Zab 18:10; Eze 1:10; 10:14; Ufu 4:6-8]

30Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni.

31Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya vitako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana.

32Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya vitako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu.

33Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu.

34Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za kitako kimoja; mataruma hayo ni kitu kimoja na kitako chenyewe.

35Na juu ya kitako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya kitako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo.

36Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote.

37Hivyo akavifanya vile vitako kumi; vyote vilikuwa vya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja.

38Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arubaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya kitako kimoja, katika vile vitako kumi.[#Kut 30:17; 2 Nya 4:6; Zek 13:1; Tit 3:5; #7:38 Tazama 7:26.]

39Akaviweka vile vitako, vitano upande wa kulia wa nyumba, na vitano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kulia wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini.

40Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli.

Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA;

41zile nguzo mbili, na mabakuli mawili ya mataji yalikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuvifunika hivyo viumbe viwili vya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo;

42na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuyafunika nayo mabakuli mawili ya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo;

43na vile vitako kumi, na birika kumi juu ya vitako;

44na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari;

45na masufuria, na majembe, na mabeseni; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.[#Kut 27:3; 38:8; 2 Nya 4:16; Zek 14:20,21]

46Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani.[#2 Nya 4:17; Mwa 33:17; Yos 3:16; 13:27]

47Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana.[#1 Nya 22:14]

48Sulemani akavitengeneza vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu;[#Kut 37:10,25; 25:30; Law 24:5]

49na vinara vya taa, vitano upande wa kulia, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu;

50na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu.

51Hivyo kazi yote aliyoifanya mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA ikamalizika. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya