1 Wafalme 9

1 Wafalme 9

Mungu Amtokea Sulemani Tena

1Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya,[#2 Nya 7:11; 1 Fal 7:1; 2 Nya 8:1,6; Mhu 2:4]

2basi, BWANA akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni.[#1 Fal 3:5; 2 Fal 20:5; Zab 10:17; 34:17; Dan 9:23; 1 Fal 8:29; Kum 11:12]

3BWANA akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote;

4na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu,[#Mwa 5:22; 6:9; 17:1; 1 Fal 2:4; 3:6; 2 Fal 20:3; Zab 16:8; 128:1; Mik 6:8; Mal 2:6]

5ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.[#2 Sam 7:12; 1 Fal 2:4; 6:12; 1 Nya 22:10]

6Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,[#2 Sam 7:14; 2 Nya 17:19; Zab 89:30]

7basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote.[#Kum 4:26; 2 Fal 17:23; 25:21; Yer 7:14; Kum 28:37; Zab 44:14]

8Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atashtuka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini BWANA ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?[#Kum 29:24; 2 Nya 7:21; Yer 22:8]

9Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu BWANA ameleta mabaya haya yote juu yao.

10Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme,

11(basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya.

12Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala hakupendezwa.

13Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo.[#9:13 Katika Kiebrania ni kama ‘nyangarika au ovyo’.]

14Hiramu alikuwa amemletea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu.[#9:14 Talanta moja ina uzito kama kilo 34.]

Matendo mengine ya Sulemani

15Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hasori, na Megido, na Gezeri.[#1 Fal 5:13; 2 Sam 5:9; Yos 19:36; 17:11; Amu 1:29]

16Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani.[#Yos 16:10]

17Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini,[#Yos 16:3; 21:22; 2 Nya 8:5]

18na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi;[#Yos 19:44]

19na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.

20Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli;

21watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.[#Amu 1:21; 3:1; Mwa 9:25; Ezr 2:55; Neh 7:57; 11:3]

22Lakini kwa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu yeyote shokoa; ila wao walikuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maafisa wake, makamanda wa magari yake na wapanda farasi wake.[#Law 25:39; Yer 34:14]

23Hao maofisa wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowasimamia watu watendao kazi.

24Lakini binti Farao akapanda toka mji wa Daudi, mpaka hiyo nyumba yake Sulemani, aliyomjengea; kisha, aliijenga Milo.[#1 Fal 3:1; 7:8; 2 Nya 8:11; 32:5; 2 Sam 5:9; 1 Fal 11:27]

25Na mara tatu kila mwaka Sulemani alikuwa akitoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu aliyomjengea BWANA akafukiza uvumba pamoja nazo juu ya madhabahu iliyokuwako mbele za BWANA. Hivyo akaimaliza nyumba.

Shughuli za Biashara ya Sulemani

26Tena, mfalme Sulemani akaunda merikebu huko Ezion-geberi, ulioko karibu na Elothi, pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu.[#Hes 33:35; Kum 2:8; 1 Fal 22:48; 2 Nya 20:36]

27Naye Hiramu akatuma merikebuni watumishi wake, wanamaji wenye kuijua bahari, pamoja na watumishi wake Sulemani.[#1 Fal 5:6,7; 10:11]

28Wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu, talanta mia nne na ishirini, wakamletea mfalme Sulemani.[#Mwa 10:2; 1 Fal 10:11; 2 Nya 8:18; Ayu 22:24; Zab 45:9; Isa 13:12; #9:28 Tazama 1 Fal. 9:14.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya