The chat will start when you send the first message.
1Mfalme wa Misri akaunda jeshi kubwa mno, kama mchanga ulioko ufukoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na merikebu nyingi, akajitahidi kujipatia ufalme wa Iskanda kwa hila, na kufunga na ufalme wake.
2Akaingia Shamu kwa maneno ya amani, nao watu wa mijini walimfungulia milango wakamkaribisha, maana ilikuwa amri ya mfalme Iskanda wampokee kwa kuwa ni mkwewe.
3Naye alipoingia katika miji ya Tolemaisi aliacha kikosi cha askari wake katika kila mji.
4Alipofika Ashdodi alioneshwa hekalu la Dagoni lililoteketezwa, na magofu ya Ashdodi na viunga vyake, na mizoga iliyotawanyika kila mahali, na maiti za wale waliokufa kwa moto, ambao walichomwa moto katika mapigano, zilizolundikwa chungu chungu njiani.
5Wakamsimulia mfalme matendo ya Yonathani, kusudi wamtie hatiani, lakini mfalme hakusema neno.
6Yonathani alikutana na mfalme kwa fahari huko Yafa, wakaamkiana, wakalala huko.
7Yonathani akamsindikiza mfalme mpaka mto uitwao Eleuthero, kisha akarejea Yerusalemu.
8Huko nyuma, mfalme Tolemayo aliishika miji ya pwani hata Seleukia kando ya bahari, akawa anabuni hila nyingi juu ya Iskanda.
9Alituma wajumbe kwa mfalme Demetrio kusema, Na tufanye maagano wewe na mimi. Nitakupa binti yangu, yule aliyepo kwa Iskanda, nawe utamiliki ufalme wa baba yako.
10Maana najuta sasa kumwoza kwa Iskanda kwa sababu alijaribu kuniua.
11Alimlaumu kwa kuutaka ufalme wake, akamnyang'anya binti yake akampa Demetrio:
12akakosana na Iskanda, hata uadui wao ulikuwa dhahiri kwa wote.
13Tolemayo akaingia Antiokia, akajivika taji la Asia, hata alivaa taji mbili, taji la Misri na taji la Asia.
14Wakati huo mfalme Iskanda alikuwako Kilikia kwa sababu wenyeji wa huko walikuwa wakifanya matata.
15Basi, Iskanda alipopata habari alimpelekea vita. Tolemayo akatoka, akakutana naye na jeshi kubwa akamshinda.
16Iskanda alikimbilia Bara Arabu, naye Tolemayo akatukuka.
17Mwarabu Zabdieli alimkata Iskanda kichwa akampelekea Tolemayo.
18Baada ya siku tatu mfalme Tolemayo naye alikufa, ndipo askari walinzi wa ngome zake waliuawa na wenyeji waliokaa ngomeni.
19Demetrio akajitawaza katika mwaka wa mia moja sitini na saba.
20Siku zile Yonathani alikusanya watu wa Uyahudi ili kuitwaa ngome ya Yerusalemu, akaunda mitambo mingi ya kuipigia.
21Lakini watu fulani, waliolichukia taifa lao wenyewe, waasi wa sheria, wakamwendea mfalme wakamwarifu ya kwamba Yonathani anaihusuru ngome.
22Aliposikia hayo alikasirika, lakini baadaye akaondoka akaenda Tolemaisi, akamwandikia Yonathani kumwambia aache kuihusuru, tena, aje upesi awezavyo kuonana naye Tolemaisi.
23Yonathani, aliposikia hayo, alitoa amri waendelee kuihusuru. Akachagua wazee wengine wa Israeli, pamoja na makuhani, asiogope hatari.
24Akachukua fedha na dhahabu na nguo, na zawadi nyingine nyingi za urafiki, akaondoka, akamwendea mfalme huko Tolemaisi.
25Akapata kibali kwake. Watu kadha wa kadha wa taifa lake, wafitini, walimsingizia,
26lakini mfalme alimtendea kama wale waliomtangulia walivyomtendea, akamtukuza machoni pa rafiki zake wote.
27Alimthibitisha katika cheo chake cha kuhani mkuu, na katika madaraka yote aliyokuwa nayo kwanza, akamkuza katika rafiki zake wakuu.
28Yonathani akamwomba mfalme aiachilie Uyahudi na ile mitaa mitatu iliyotoka katika Samaria isitozwe kodi, akaahidi kutoa talanta mia tatu.
29Mfalme akakubali, akamwandikia Yonathani barua juu ya mambo hayo yote, kama hivi:
30Mfalme Demetrio kwa nduguye Yonathani na kwa taifa la Wayahudi, salamu.
31Nakala ya barua tuliyomwandikia Lastheni, ndugu yetu, juu yenu tumewaandikieni ninyi pia ili mjue yaliyomo.
32Mfalme Demetrio kwa baba yake Lastheni, salamu.
33Sisi tumekusudia kulitendea mema taifa la Wayahudi kwa sababu ya nia yao njema kwetu; maana wao ni rafiki zetu wanaotuangalia kwa mema.
34Tumewayakinishia mipaka ya Uyahudi na mitaa mitatu ya Efraimu, Lida na Ramathaimu, iliyojumlishwa na Uyahudi kutoka kwa Samaria, pamoja na mambo yote yanayoihusu, kwa faida yao watoao dhabihu Yerusalemu. Pamoja na hayo, tumewaachilia mapato ya kila mwaka aliyoyachukua mfalme zamani katika mazao ya ardhi na matunda.[#1 Mak 10:30]
35Kwa habari za mambo mengine yaliyo haki yetu – zaka na ada zinazotuhusu, kodi ya machimbo ya chumvi, na fedha zimhusuzo mfalme – hayo yote tangu sasa tunawapa wao.
36Wala hakuna neno lolote katika hayo litakalobatiliwa tangu sasa hata milele.
37Basi, angalia mfanye nakala ya maneno hayo apewe Yonathani, nayo iwekwe katika mlima mtakatifu mahali pa kufaa itakapoonekana vema.
38Mfalme Demetrio alipoona nchi imetulia mbele yake, wala hakuna wa kufanya matata, aliwapa askari wake ruhusa, kila mtu aende kwao, ila askari wa mshahara aliowaajiri kutoka visiwa vya mataifa. Kwa hiyo askari wa baba zake walimchukia.
39Trifoni ni mtu aliyekuwa kwanza upande wa Iskanda, ikawa, alipoona jinsi askari wote wanavyomnung'unikia Demetrio alimwendea Imalkue, Mwarabu, aliyekuwa akimlea Antioko, mwana mdogo wa Iskanda,
40akamshawishi ampe huyu mtoto ili amtawalishe mahali pa babaye. Akamsimulia yote aliyoyafanya Demetrio, na jinsi askari wake walivyomchukia, akakaa huko siku nyingi.
41Yonathani akapeleka kumwomba mfalme Demetrio awaondoe wale askari waliokuwamo katika ngome ya Yerusalemu na katika maboma mengine, maana walikuwa wakipigana na Waisraeli kila mara.
42Demetrio akampelekea Yonathani jibu hili: Si haya tu nitakayokufanyia wewe na taifa lako, ila pia nitakukuza sana, wewe na taifa lako, nitakapoona nafasi ya kufaa.
43Nawe, tafadhali, niletee watu wa kunipigania, maana askari wangu wote wameniasi.
44Yonathani akampelekea mfalme watu hodari elfu tatu huko Antiokia; wakafika kwake, naye alifurahi kwa kuja kwao.
45Wenyeji wa mji walikutana katikati ya mji, watu wapatao elfu mia moja na na ishirini, wakitaka kumwua mfalme.
46Mfalme akakimbilia nyumbani kwake, watu wa mji wakazishika njia kuu wakaanza kufanya ghasia.
47Mfalme akawaita Wayahudi wamsaidie nao wote wakamwitikia mara, wakaenda huku na huko mjini, hata siku ile waliua watu kama elfu mia moja,
48wakautia mji moto. Siku ile waliteka nyara nyingi na kumwokoa mfalme.
49Watu wa mjini walipoona ya kuwa Wayahudi wana nguvu ya kufanya wapendavyo walikufa moyo, wakamwambia mfalme,
50Tupeni yamini, uwaambie Wayahudi waache mapigano yao juu yetu na juu ya mji.
51Wakatupa silaha zao chini wakafanya amani. Wayahudi walitukuka machoni pa mfalme na machoni pa wote wa milki yake, wakarejea Yerusalemu na mateka wengi.
52Lakini mfalme Demetrio alipoketi tena katika kiti cha enzi cha ufalme wake, na nchi yote ilikuwa imetulia mbele yake,
53alijionesha kuwa mwongo katika yote aliyoyasema, maana aliuvunja urafiki wake na Yonathani, wala hakumfanyia yale mema aliyomwahidi, bali alimwudhi vibaya sana.
54Basi, baada ya hayo, Trifoni alirudi, akimleta yule mtoto Antioko. Akafanywa kuwa mfalme na kutiwa taji;
55na wale askari wote walioondolewa na Demetrio walijiunga naye. Wakapigana na Demetrio, akashindwa kabisa, akakimbia.
56Trifoni akawachukua wale tembo, akaushika mji wa Antiokia.
57Yule kijana Antioko alimwandikia Yonathani akisema, Nakuthibitishia cheo chako cha kuhani mkuu, na kukuweka juu ya zile milki nne, nawe utakuwa mmoja wa rafiki za mfalme.
58Akampelekea vyombo vya dhahabu, na vingine vya kutumia mezani, akampa idhini kunywa katika vyombo vya dhahabu na kuvaa urujuani na bizimu ya dhahabu.
59Akamfanya nduguye Simoni kuwa Mkuu wa nchi, toka mlima uitwao Ngazi ya Tiro hata mipaka ya Misri.
60Yonathani akaondoka, akashika njia ng'ambo ya mto akipitia miji ya huko, na majeshi yote ya Shamu yalimwendea ili kufanya urafiki naye. Akafika Ashkeloni, watu wa mjini wakampokea kwa heshima.
61Kutoka hapo akaenda Gaza, bali watu wa Gaza walimfungia asiingie. Akauhusuru mji, akavitia moto viunga vyake akaviteka.
62Ndipo watu wa Gaza wakamwomba Yonathani, akawapa yamini. Akashika wana wa wakuu wao wawe wadhamini akawapeleka Yerusalemu. Akaipitia nchi hata Dameski.
63Yonathani akasikia ya kuwa wakuu wa Demetrio wamefika Kadeshi ya Galilaya pamoja na jeshi kubwa ili kumwondoa katika kazi yake.
64Akaenda kukutana nao, ila nduguye Simoni alimwacha huko aliko.
65Simoni akapiga kambi kuelekea Bethsura, akaipiga siku nyingi na kuihusuru, wakamwomba amani, akakubali.
66Lakini aliwatoa humo akaushika mji, akaweka humo kikosi cha askari.
67Yonathani na jeshi lake wakapiga kambi penye ziwa la Genesareti, hata asubuhi na mapema wakaondoka kwenda uwanda wa Hazori.
68Jeshi la mataifa likakutana naye uwandani. Wengine wao walikuwa wakimwotea milimani, hali jeshi lenyewe lilipambana naye uso kwa uso.
69Nao waliomwotea wakaondoka wakajitia katika vita,
70na wote wa upande wa Yonathani walikimbia, asibaki hata mmoja ila Matathia mwana wa Absalomu na Yuda mwana wa Kalfi, wakuu wa vikosi.
71Yonathani akararua nguo zake akajitia mchanga kichwani akasali.
72Akaingia tena vitani, akawarudisha nyuma, hata wakakimbia.
73Watu wake walipoona hivi walimrudia, wakafuatana naye wakiwakimbiza mpaka Kadeshi kwenye kambi yao, wakatua.
74Siku ile katika wageni walianguka watu kama elfu tatu. Yonathani akarudi Yerusalemu.