The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, mataifa waliozunguka waliposikia ya kuwa madhabahu imejengwa, na patakatifu pamewekwa wakfu kama zamani, walikasirika sana.
2Wakafanya shauri kuuharibu ukoo wa Yakobo uliokuwako katikati yao, wakaanza kuwaua na kuwaangamiza.
3Yuda akapigana na wana wa Esau huko Akrabimu katika Idumia, kwa sababu walikuwa wakiwaudhi Waisraeli kwa mashambulio yao. Akawapiga pigo kubwa sana, akawavunja kabisa, akawateka nyara.
4Akayakumbuka matata ya wana wa Baea, ambao walikuwa mtego na kikwazo kwa watu, wakiwaotea njiani.
5Akawazingira katika ngome zao, akawahusuru, akawaangamiza kabisa na kuiteketeza minara yao pamoja na wote waliokuwamo.
6Akavuka kuwaendea Waamoni, akakuta jeshi kubwa la nguvu na watu wengi, na viongozi wao Timotheo.
7Akapigana nao vita vingi, wakapondwa mbele yake na kushindwa kabisa.
8Akashika Yazeri na miji yake, akarudi Uyahudi.
9Watu wa mataifa waliokaa Gileadi wakajipanga juu ya Waisraeli waliokuwamo mipakani mwao ili kuwaua; nao waliikimbilia ngome ya Dathema,
10Akapeleka barua kwa Yuda na ndugu zake kusema, Mataifa wanaotuzunguka wamejiunga pamoja ili kutuua.
11Wanajiweka tayari kuja kuishika ngome tuliyoikimbilia. Kiongozi wao ni Timotheo.
12Njoni, basi, mtuopoe mikononi mwao, maana wengi wetu wamekwisha kufa,
13na ndugu wote waliokuwamo katika nchi ya Tobu wameuawa. Wamechukua mateka wake zao na watoto wao na mali yao, na kuua watu wapatao elfu moja.
14Walipokuwamo katika kuzisoma barua hizi, wajumbe wengine walifika kutoka Galilaya na nguo zao zimeraruliwa,
15wakileta habari kwamba Watu wa Tolemaisi na Tiro na Sidoni, na Galilaya yote ya mataifa, wamejikusanya pamoja ili kutuua.
16Yuda na watu wake walipoyasikia maneno hayo walifanya baraza kubwa ili kushauriana pamoja juu ya njia ya kuwasaidia ndugu zao waliokuwamo katika taabu kubwa na hatari ya kushambuliwa na adui.
17Yuda akamwambia Simoni ndugu yake, Chagua watu, uende kuwaokoa ndugu zetu huko Galilaya, na mimi na ndugu yangu Yonathani tutakwenda Gileadi.
18Akawaacha Yusufu mwana wa Zakaria na Azaria wawe juu ya watu katika Uyahudi, pamoja na baki ya jeshi wailinde nchi.
19Akawaagiza akisema, Mwe juu ya watu hawa, lakini msipeleke vita juu ya mataifa mpaka sisi tutakaporudi.
20Simoni akatwaa watu elfu tatu kwenda nao Galilaya, na Yuda elfu nane kwenda Gileadi.
21Simoni akaenda Galilaya, akapigana mara nyingi na mataifa, akawashinda.
22Akawafuatia mpaka mlango wa Tolemaisi; watu wa mataifa wapatao elfu tatu walianguka, akawateka nyara.
23Akawachukua Wayahudi waliokuwako Galilaya na Arabata, pamoja na wake zao na watoto wao, na vyote walivyokuwa navyo, akarudi nao Uyahudi kwa furaha kuu.
24Nao Yuda Makabayo na nduguye Yonathani walivuka Yordani wakaenda safari ya siku tatu jangwani,
25wakakutana na Wanebayothi, nao waliwapokea kwa amani, wakawapa habari za yote yaliyowapata ndugu zao katika Gileadi,
26kwamba wengi wao wamefungiwa katika Bozra na Beseri na Alema na Kasfori na Makedi na Karnaimu, ambayo yote ni miji mikubwa na yenye ngome;
27na kwamba wamefungiwa katika miji mingine ya Gileadi pia. Hata wameiweka kesho iwe siku ya kuzizingira ngome hizo, wapate kuzitwaa na kuwaharibu watu wote kwa siku moja.
28Basi, Yuda na jeshi lake wakageuka mara wakapitia njia ya jangwani mpaka Bozra. Akautwaa mji, akawaua wanaume wote kwa upanga, akateka nyara akauchoma mji moto.
29Akaondoka huko usiku akaendelea mpaka ngomeni,
30hata asubuhi walipotazama, kumbe! Watu wengi wasiohesabika wanaleta ngazi na mitambo ya vita ili kuitwaa ngome, maana mapigano yameanza.
31Yuda alipoona ya kuwa vita vimeanza, na makelele ya mjini yanapanda mbinguni pamoja na sauti za tarumbeta na milio ya vita,
32aliwaambia watu wa jeshi lake, Wapiganieni ndugu zenu leo.
33Akawaendea na vikosi vitatu, wakipiga tarumbeta na kusali kwa sauti kuu.
34Watu wa jeshi la Timotheo wakatambua ya kuwa ni Makabayo, wakakimbia mbele yake. Akawapiga kwa pigo kubwa, wakaanguka siku ile watu kama elfu nane.
35Akaugeukia Mizpa akaupiga, akautwaa, akawaua wanaume wote waliokuwamo, akachukua mateka akauchoma mji moto.
36Akaondoka hapo, akashika Kasfori, Makedi, Beseri, na miji mingine ya Gileadi.
37Baada ya hayo, Timotheo akaunda jeshi jingine, akapiga kambi kuelekea Rafoni ng'ambo ya mto.
38Yuda akatuma watu walipeleleze jeshi lake, wakamletea habari ya kuwa, Watu wote wa mataifa ya jirani wamejiunga nao, jeshi kubwa mno!
39Tena, wameajiri Waarabu kuwasaidia. Wamepiga kambi ng'ambo ya mto, tayari kukushambulia. Yuda akaenda kukutana nao,
40hata, walipofika karibu na mto, Timotheo aliwaambia maofisa wake, Kama yeye akitangulia kuvuka ili kutujia hatutaweza kumpinga; bila shaka atatushinda.
41Lakini kama akiona hofu na kukaa upande ule, sisi tutavuka kwa kumwendea na kumshinda.
42Yuda akaufikia mto, akaweka maofisa wa jeshi lake ukingoni mwa mto akawaagiza, Msimwache mtu yeyote atue; sharti kila mtu ajitie vitani.
43Naye mwenyewe alivuka kwanza, na jeshi lake lote nyuma yake; watu wote wa mataifa wakapondwa mbele yao, hata walitupa silaha zao wakavikimbilia vitalu vya hekalu ya Karnaimu.
44Nao waliutwaa mji, wakiteketeza kitalu cha hekalu, na wote waliokuwamo. Karnaimu ikatiishwa kabisa, wala haikuweza kusimama tena mbele ya Yuda.
45Yuda akakusanya pamoja Waisraeli wote waliokuwako Gileadi, tangu wadogo mpaka wakubwa, pamoja na wake zao na watoto wao, na vyombo vyao, jamii kubwa mno, ili kuwapeleka kwenye nchi ya Uyahudi.
46Wakafika Efroni, mji mkubwa njiani, wenye nguvu. Haikuwezekana kupita kwa upande wa kulia wala wa kushoto, ila lazima kuupitia katikati.
47Nao wa mjini wakatoka wakaiziba milango yake kwa mawe.
48Yuda akatuma mtu kwao kwa maneno ya amani, kusema, Twaomba ruhusa kuipitia nchi yenu ili tufike kwetu. Hakuna mtu kwao atakayewadhuru, ila tutapita tu kwa miguu yetu. Lakini walikataa kumfungulia.
49Yuda akaagiza ipigwe mbiu katika jeshi, kwamba kila mtu atue mahali alipo.
50Watu wa jeshi wakatua. Akaupiga mji kutwa kucha, ukatiwa mikononi mwake.
51Akawaua wanaume wote kwa upanga, akaubomoa mji na kuuteka nyara, akaupitia juu ya miili ya wale waliouawa.
52Wakavuka Yordani mpaka uwanda mkubwa kuelekea Beth-sheani.
53Njiani mwote Yuda alikuwa akiwachunga wale waliokuwa nyuma, na kutia watu moyo, mpaka walipofikia nchi ya Uyahudi.
54Wakaupandia mlima Sayuni kwa furaha na shangwe, wakatoa sadaka za kuteketezwa, kwa kuwa wamerudi kwa amani wala hakuna hata mmoja aliyekufa njiani.
55Wakati Yuda na Yonathani walipokuwako Gileadi, na nduguye Simoni alikuwako Galilaya mbele ya Tolemaisi,
56Yusufu mwana wa Zakaria na Azaria, wakuu wa jeshi lililoachwa Uyahudi, walisikia habari za matendo yao ya ushujaa, na za vita walivyovipigana,
57wakasema, Tujipatie jina na sisi pia; tuende tupigane na mataifa yanayotuzunguka.
58Wakawapa amri watu wa jeshi lao, wakashika njia ya Yamnia.
59Gorgia na watu wake wakatoka mjini kupigana nao,
60Yusufu na Azaria wakakimbizwa, wakafuatiwa hata kwenye mipaka ya Uyahudi, na siku ile walianguka Waisraeli wapatao elfu mbili.
61Hasara kubwa hii iliwapata kwa sababu hawakuwatii Yuda na ndugu zake, wakidhani wataweza kuonesha ushujaa wao.
62Bali hao hawakuwa wa ukoo wa watu wale waliojaliwa kuiokoa Israeli kwa mikono yao.
63Mtu huyo Yuda na ndugu zake walitukuzwa mno machoni pa Israeli na pa mataifa yote, kila lilipotajwa jina lao,
64hata watu wengi waliwajia kuwapa pongezi.
65Kisha, Yuda na ndugu zake wakaondoka wakapigana na wana wa Esau katika nchi ya kusini, wakapiga Hebroni na miji yake, wakizivunja ngome zake na kuiteketeza minara iliyoizunguka.
66Akaondoka kwenda nchi ya Wafilisti akipitia Marisa.
67Siku ile kulikufa vitani makuhani kadha wa kadha waliokwenda kupigana kwa jinsi isiyofaa, wakitumaini kufanya mambo ya ujasiri.
68Yuda akaugeukia Ashdodi katika nchi ya Wafilisti, akazivunja madhabahu zao na kuziteketeza sanamu za miungu yao. Akateka nyara miji yao, akarudia Uyahudi.