1 Wamakabayo 6

1 Wamakabayo 6

Siku za mwisho za Antioko Epifani

1Mfalme Antioko alipokuwa akisafiri katika nchi za juu alisikia habari za Elimaisi, mji wa Uajemi, uliosifiwa sana kwa utajiri wake, fedha yake na dhahabu yake.

2Hekalu lake lilikuwa na mali nyingi, na humo mlikuwa na ngao za dhahabu, na dirii, na silaha za vita ambazo ziliwekwa humo na Iskanda, mwana wa Filipo, kuwatawala Wagiriki.

3Basi, alifika huko, akitaka kuutwaa mji na kuuteka nyara. Lakini haikuwezekana, kwa sababu shauri lake lilijulikana kwa watu wa mjini,

4wakajipanga kufanya vita naye. Akakimbia, akaondoka kwa moyo mzito kurudi Babeli.

5Akaletewa habari huko Uajemi ya kuwa majeshi waliokwenda kuipiga nchi ya Uyahudi wameshindwa;

6tena Lisia, aliyekwenda kwao na jeshi la nguvu sana, alikimbizwa mbele yao; nao wamepata nguvu nyingi kwa sababu ya silaha na zana za vita na nyara walizoziteka kwa majeshi waliyoyashinda.

7Zaidi ya hayo, wamelibomoa lile chukizo alilolijengesha juu ya madhabahu Yerusalemu, na kupazungushia patakatifu kuta ndefu, kama zamani, na mji wake Bethsura pia.[#1 Mak 1:54]

8Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno hayo, alishikwa na bumbuazi akafadhaika mno.

9Akakaa huko siku nyingi, maana alilemewa na huzuni nyingi hata alidhani atakufa.

10Akawaita rafiki zake wote, akawaambia, usingizi umefarakana na macho yangu, hata moyo wangu umevunjika kwa taabu.

11Nasema ndani yangu, Jinsi nilivyoteseka! Ninazama katika maji mengi! Katika enzi yangu nilikuwa mstahiki, mwenye kupendwa.

12Lakini sasa nayakumbuka mabaya niliyoyafanya Yerusalemu, jinsi nilivyovichukua vyombo vyote vya fedha na dhahabu vilivyokuwapo, na kupeleka majeshi kuwaharibu wenyeji wa Yerusalemu bila sababu.

13Nafahamu ya kuwa kwa sababu hiyo maovu haya yamenipata, hata, tazama ninakufa kihoro katika nchi ya kigeni.

Mwanzo wa utawala wa Antioko wa Tano

14Akamwita Filipo, mmoja wa rafiki zake, akamkabidhi ufalme wake wote.

15Akampa taji yake na vazi lake na pete yake ya mhuri, na amri ya kumlea mwanawe Antioko na kumwelimisha awe mfalme.

16Naye mfalme Antioko alikufa pale, mwaka mia mmoja arubaini na tisa.

17Lisia aliposikia ya kuwa mfalme amekufa, alimtawaza mwanawe Antioko, ambaye amemlea tangu utoto wake, akampa jina la Eupatori.

Mashambulizi kutoka Ashuru

18Basi, wale waliokuwamo ngomeni walikuwa wakiwaotea Waisraeli huko hekaluni, wakajaribu kuwapiga kila mara na kuwasaidia mataifa.

19Yuda akanuia kuwaharibu, akawakusanya watu wake wote kusudi awazingire.

20Wakakutanika wakawahusuru, mwaka mia moja na hamsini; akafanya minara ya vita na mitambo ya kutupia silaha.

21Lakini wengine wao waliponyoka, hata Waisraeli wengine waasi walijiunga nao.

22Wakamwendea mfalme wakasema, Hata lini utaacha kutekeleza hukumu na kuwapatia haki ndugu zetu?

23Sisi tulikubali kumtumikia baba yako na kuyashika maagizo yake na kuzifuata amri zake.

24Kwa sababu hiyo watu wetu wamefarakana nasi na kutuhusuru ngomeni; hata kama wakikamata watu wa kwetu huwaua na kuchukua mali yao.

25Si kama wamenyosha mkono wao juu yetu tu, ila pia juu ya wote waliomo mipakani mwao.

26Hata leo wanaizingira ngome ya Yerusalemu ili kuitwaa, tena wamepaimarisha patakatifu na Bethsura.

27Usipowazuia upesi watafanya zaidi kuliko hayo, nawe hutaweza kuwapinga.

Antioko wa Tano na Lisia wanapigana na Wayahudi mapigano ya Beth-zakaria

28Aliposikia haya, mfalme alikasirika sana. Akawakusanya rafiki zake wote, maofisa wa jeshi lake na wale waliokuwa juu ya wapanda farasi.

29Askari wa mshahara walikuja kwake toka falme nyingine na visiwa vya baharini,

30hata hesabu ya jeshi lake ilikuwa askari elfu mia moja, wapanda farasi elfu ishirini, na tembo hodari kwa vita thelathini na wawili.

31Walipitia Idumia wakapiga kambi kuelekea Bethsura, wakaipiga siku nyingi na kufanya mitambo ya vita. Nao waliokuwamo walitoka wakaichoma moto na kupigana kwa ushujaa.

Vita vya Beth-zakaria

32Yuda akaiacha ngome, akapiga kambi Beth Zakaria kulielekea kambi la mfalme.

33Mfalme akaondoka asubuhi na mapema, akapeleka jeshi lake upesi katika njia ya Beth Zakaria. Huko majeshi walijiweka tayari kwa vita wakapiga tarumbeta.

34Wakawaonesha tembo damu ya zabibu na forsadi ili kuwachochea.

35Wakawaeneza tembo katika vikosi vya askari, kila tembo askari elfu moja wenye deraya ya chuma na chapeo cha shaba nyeupe kichwani; na kwa kila tembo wapanda farasi wateule mia tano.

36Hao hufuatana na tembo; kokote aendako yeye, wao huenda vile vile bila kufarakana naye.

37Mgongoni mwa tembo kulikuwa na minara imara ya mti, iliyokazwa kwa ukanda maalumu, naye alipandwa na askari hodari wawili na Mhindi wake.

38Baki ya wapanda farasi waliwekwa mbavuni mwa jeshi, huku na huko, tayari kuwashambulia adui na kuwalinda askari wa vikosi.

39Jua lilipoziangaza ngao za dhahabu na shaba, milima ilirudisha nuru yake ikimetameta kama mienge ya moto.

40Baadhi ya jeshi la mfalme walienezwa juu ya milima mirefu, na baadhi yao walikuwa uwandani chini, wakaenda mbele kwa taratibu na mpango mzuri.

41Wote waliosikia mshindo wa miguu yao na magongano ya silaha zao walitetemeka, maana jeshi lilikuwa kubwa sana, lenye nguvu.

42Yuda na jeshi lake wakakaribia wakajitia vitani, na watu mia sita wa jeshi la mfalme waliuawa.

43Eleazari Avarani aliona tembo mmoja aliyevikwa deraya ya kifalme kifuani, tena amewapita wengine wote kwa ukubwa; akadhani huyu amepandwa na mfalme mwenyewe.

44Akatoa maisha yake kwa watu wake,

45maana alijitia kwa ujasiri katika kikosi cha askari akamwendea kasi, akiua watu huku na huko, hata wakamwepa kila upande.

46Akaingia chini ya tembo akamchoma tumboni akamwua. Tembo akamwangukia, akafa pale pale.

47Lakini Wayahudi walipoiona nguvu ya ufalme, na mashambulio makali ya majeshi yake walirudi nyuma.

Kuzingirwa kwa hekalu

48Watu wa jeshi la mfalme wakapanda Yerusalemu kukutana nao, mfalme akapiga kambi yake kuelekea Uyahudi na mlima Sayuni.

49Watu wa Bethsura wakatoka mjini kwa sababu hawakuwa na chakula cha kutosha, kwa kuwa ni mwaka wa Sabato, akafanya mapatano nao;

50akashika Bethsura, akaweka humo kikosi cha askari walinzi.

51Akapahusuru patakatifu kwa siku nyingi, akiweka pale zana za kubomolea ukuta, na mitambo ya vita, na vyombo vya kutupia moto na mawe, na vya kutupia vikuki, na makombeo.

52Nao pia waliohusuriwa walifanya mitambo ya kuipinga mitambo yao, wakapigana kwa siku nyingi.

53Lakini hawakuwa na chakula cha kutosha katika maghala, kwa sababu ni mwaka wa Sabato, tena wale waliokimbilia Uyahudi ili kujisalimisha na mataifa walikuwa wamekimaliza chakula kilichobaki.

54Kwa hiyo ni watu wachache tu waliobaki katika patakatifu, maana njaa ilikuwa kali, nao wametawanyika kila mtu kwake.

Ashuru watoa mapatano

55Lisia akasikia ya kuwa Filipo (ambaye mfalme Antioko, kabla ya kufa kwake, alimkabidhi kazi ya kumlea mwanawe Antioko hata awe mfalme)

56amerudi kutoka Uajemi na Umedi pamoja na majeshi yaliyokwenda na mfalme naye yu tayari kujifanya mkuu wa nchi.

57Basi aliona afadhali kuondoka upesi. Akawaambia mfalme na wakuu wa jeshi lake na askari, Kila siku tunazidi kudhoofika; chakula chetu kimepungua, na mahali tunapopahusuru pana nguvu sana; tena mambo ya ufalme yanatushurutisha.

58Basi, tupeane yamini na watu hawa, tukafanye amani nao na taifa lao lote.

59Tuagane nao wazifuate amri zao wenyewe, kama zamani, maana wamechukizwa na kufanya matata haya kwa ajili ya amri zao tulizozitangua.

60Shauri hili liliwapendeza mfalme na wakuu wake. Akawapelekea maneno ya amani wakayakubali.

61Mfalme na wakuu wake waliwapa yamini yao, nao wakatoka katika ngome yao.

62Lakini mfalme alipoingia katika ngome ya mlima Sayuni na kuona jinsi ilivyokuwa imara alivunja kiapo chake akatoa amri ukuta ulioizunguka ubomolewe.

63Ndipo akatoka kwa haraka akarudia Antiokia, akamkuta Filipo ameushika mji; akafanya vita naye akautwaa mji kwa nguvu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya