The chat will start when you send the first message.
1Yuda akasikia sifa ya Warumi, ya kuwa ni watu wenye nguvu, wanaowapenda wale waliojiunga nao na kupokea kwa urafiki wote wawajiao, tena ni watu wenye nguvu.
2Alisimuliwa habari za vita vyao na matendo yao kwa Wagalata, jinsi walivyowashinda na kuwatoza kodi,
3na mambo waliyoyafanya katika nchi ya Spania walipojipatia machimbo ya fedha na dhahabu;
4na jinsi walivyoipata nchi yote kwa akili yao na bidii yao, ingawa ni nchi ya mbali sana. Alisikia habari za wafalme waliowajia kwa vita toka miisho ya dunia, jinsi walivyopondwa na kupigwa vibaya sana, hata wengine kuwatolea kodi kila mwaka.
5Na habari za Filipo, na Perseo, mfalme wa Kitimu, na wengine waliojiinua juu yao, jinsi walivyopigwa vitani na kushindwa.
6Antioko pia, yule mfalme mkubwa wa Asia, aliwajia vitani na tembo mia moja na ishirini, na farasi, na magari, na jeshi kubwa sana, naye alishindwa akakamatwa, akalazimishwa kutoa fedha nyingi kila mwaka, yeye na wale watakaomfuata.
7Alipasiwa pia kupeleka wadhamini wakae kwao, na kutoa sehemu ya milki yake,
8yaani nchi za Hindi na Umedi na Lida, na nchi nyingine zilizo nzuri. Hizo walipozipokea walimpa mfalme Eumene.
9Zaidi ya hayo, alisikia jinsi watu wa Ugiriki walivyofanya shauri kuja kuwapiga;
10shauri lao likajulikana kwao, wakapeleka jemadari kupigana nao, na wengi walianguka, wametiwa jeraha za mauti, Wakachukua utumwani wake zao na watoto wao, wakateka nyara, wakaitwaa nchi yao na kuzivunja ngome na kuwatumikisha hata leo.
11Falme nyingine pia, na visiwa, vilivyojiinua juu yao wakati wowote, waliziharibu na kuvitumikisha.
12Bali walikuwa waaminifu kila mara kwa rafiki zao na kwa wale waliowategemea. Walikuwa wameshinda wafalme, walio karibu na walio mbali, na wote waliosikia sifa zao waliwaogopa.
13Kama wakinuia kumsaidia mtu na kumtawaza, hutawazwa; kama wakinuia kumshusha mtu, hushushwa. Nao wametukuka sana.
14Ingawa ni hivi, hakuna yeyote miongoni mwao aliyejitia taji, wala kujivika vazi la urujuani ili kujitukuza nafsi yake.
15Katika nyumba yao ya baraza waliyoijenga, watu mia tatu na ishirini hukusanyika kila siku kushauriana daima kwa ajili ya watu wao, ili watawaliwe vema.
16Huaminisha mtu mmoja kila mwaka kazi ya utawala, awe juu ya nchi yao yote. Wote humtii huyo, wala hakuna wivu au husuda miongoni mwao.
17Basi, Yuda alimchagua Eupolemo, mwana wa Yohana, mwana wa Hakosi, na Yasoni, mwana wa Eleazari, akawatuma Rumi wafanye mapatano ya urafiki na umoja,[#2 Mak 4:11]
18na kuwashawishi kuwaondolea nira, maana waliona ya kuwa utawala wa Wagiriki unaitia Israeli utumwani.
19Wakaenda Rumi, safari ndefu sana, wakaingia barazani, wakasema,
20Tumetumwa kwenu na Yuda Makabayo na ndugu zake na taifa la Wayahudi, ili tufanye nanyi mapatano na amani, tuandikwe kuwa washirika wenu na rafiki zenu.
21Walikubali maombi yao,
22na hii ndiyo nakala ya barua waliyoiandika juu ya vipande vya shaba ili kuwajibu, ambayo ilipelekwa Yerusalemu kuwekwa huko iwe kumbukumbu ya amani na umoja:[#1 Mak 14:18]
23Ufanisi uwe kwa Warumi na kwa taifa la Wayahudi baharini na barani daima; mkuki na adui wawapitie mbali.
24Lakini, ikiwa vita vitaletwa juu ya Warumi au juu ya rafiki zao mahali popote.
25Wayahudi watawasaidia kama rafiki kwa jinsi itakavyoonekana kufaa, kwa moyo wao wote.
26Na kwa habari za wale waletao vita, Wayahudi hawatawapa wala kuwapatia chakula, silaha, fedha au merikebu, kama Warumi watakavyoagiza. Watatimiza masharti yao bila kupewa kitu.
27Tena, vivyo hivyo, kama vita vitaliangukia taifa la Wayahudi. Warumi watawasaidia kwa urafiki, kwa moyo wao wote, kwa jinsi itakavyoonekana kufaa.
28Na kwa habari za wale waletao vita, hawatawapa nafaka, silaha, fedha au merikebu, kama Warumi watakavyoagiza. Watayashika masharti haya bila hila.
29Kwa masharti hayo Warumi wamefanya mapatano na Wayahudi.
30Kama katika siku zijazo watu wa upande mmoja watataka kuongeza au kupunguza neno wataruhusiwa, na lolote watakaloongeza au kupunguza litathibitika.
31Tena, juu ya maovu mnaotendwa na mfalme Demetrio tumemwandikia kusema, Kwa nini umefanya nira yako kuwa nzito juu ya rafiki zetu na washirika wetu, Wayahudi?
32Basi, kama wakija kututakia msaada tena juu yenu tutawapatia haki, na kupigana nanyi baharini na barani.