1 Wamakabayo 9

1 Wamakabayo 9

1Demetrio aliposikia kwamba Nikano na jeshi lake wameanguka vitani, aliwapeleka Bakide na Alkimo mara ya pili katika nchi ya Uyahudi pamoja na vikosi vya upande wa kulia wa jeshi lake.

2Wakashika njia ya Galgala, wakapiga kambi katika Arbela kuelekea Mesalothi; wakaitwaa, wakaua watu wengi.

3Katika mwezi wa kwanza wa mwaka mia moja hamsini na mbili walipiga kambi kuelekea Yerusalemu.

4Kutoka hapo wakaondoka wakaenda Berea na askari elfu ishirini na farasi elfu mbili.

5Naye Yuda alikuwa amepiga kambi Elasa, pamoja na watu wateule elfu tatu.

6Ikawa, walipoliona lile jeshi kubwa, na wingi wa askari, walishikwa na hofu, hata wengi walitoka kambini kwa siri wakaenda zao, wasibaki zaidi ya watu mia nane.

7Yuda alipoona jinsi watu wake walivyopungua, na vita vitaanza sasa hivi, alifadhaika rohoni, kwa kuwa hakuna nafasi ya kuwakusanya tena.

8Tumaini lake likapotea; lakini, hata hivi, aliwaambia wale waliosalia, Tuondoke kupambana na adui zetu, kama labda tutaweza kupigana nao.

9Wakajaribu kumzuia, wakisema, Kabisa hatutawaweza. Afadhali tujiokoe nafsi zetu. Tutarudi tena na ndugu zetu kupigana nao, lakini kwa sasa tu wachache mno.

10Yuda akajibu, Hasha! Isiwe kwangu kuwakimbia! Kama ajali yetu imetimia, tufe kwa ushujaa kwa ajili ya ndugu zetu, utukufu wetu usilaumiwe.

Vita vya mwisho vya Yuda

11Jeshi la adui likatoka kambini, na Wayahudi wakasimama tayari kupambana nao. Wapanda farasi walitengwa katika vikosi viwili, na wenye makombeo na wapiga mishale walitangulia mbele ya jeshi, pamoja na askari hodari wa kufanya mashambulio;

12Bakide mwenyewe alikuwa kando, upande wa kulia. Pande zote mbili zilisonga mbele pamoja na jeshi lote, wakipiga tarumbeta.

13Nao wa jeshi la Yuda walipiga tarumbeta zao, hata nchi ilitikisika kwa makelele ya majeshi. Wakapambana vitani tangu asubuhi hata jioni.

14Yuda alipoona ya kuwa Bakede yupo upande wa kulia, na ndipo ilipo nguvu hasa ya jeshi,

15yeye na wafuasi wake walimkazania, hata walivishinda vikosi vya kulia wakavifuatia mpaka mlima Azota.

16Nao wa upande wa kushoto walipoona vikosi vya upande wa kulia vimeshindwa, waligeuka kuwafuatia Yuda na wenzake.

17Mapigano yakazidi kuwa makali, na wengi wa kila upande waliuawa;

18naye Yuda akaanguka na watu wake wakakimbia.

Maziko ya Yuda Makabayo

19Yonathani na Simoni walimtwaa ndugu yao Yuda wakamzika katika kaburi la baba zake Modini.

20Wakamwombolezea, hata Waisraeli walifanya kilio kikubwa, wakimlilia siku nyingi, wakisema,

21Jinsi shujaa alivyoanguka! Mwokozi wa Israeli!

22Basi, mambo mengine ya Yuda – vita vyake na matendo yake ya ushujaa, na ukuu wake – hayakuandikwa, maana yalikuwa mengi mno.

YONATHANI KIONGOZI NA KUHANI MKUU WA WAYAHUDI (160-142 K.K.)

Yonathani mfuata Yuda

23Ikawa, baada ya kufa kwake Yuda, wasio haki walianza kuinua vichwa vyao katika mipaka ya Israeli, na watenda mabaya wote walijitokeza.

24Wakati ule njaa kubwa iliingia, hata ardhi yenyewe ilijiweka upande wao.

25Bakide alichagua watu waliokuwa wameiacha dini yao, akawafanya wakuu wa nchi.

26Wakawatafuta rafiki za Yuda kwa bidii, wakawaleta kwa Bakide, naye aliwatesa na kuwaudhi.

27Ikawa huzuni kubwa katika Israeli kuliko wakati wowote tangu manabii walipokoma.

28Marafiki wote wa Yuda walikutana, wakamwambia Yonathani,

29Tangu ndugu yako Yuda amekufa, hakuna mtu kama yeye wakupigana na adui zetu na Bakide na wale wa taifa letu wanaotuchukia.

30Basi, tumekuchagua leo uwe kiongozi wetu na mkubwa wetu mahali pake, kuvipiga vita vyetu.

31Yonathani akakubali kuwa kiongozi wao akatwaa mahali pa nduguye Yuda.

Yonathani katika nyika ya Tekoa. Matendo ya kikatili huko Medaba

32Bakide alipotambua hayo, alimtafuta ili amwue.

33Lakini Yonathani na nduguye Simoni na watu wao wote wakapata habari wakaikimbilia nyika ya Tekoa, wakapiga kambi karibu na maji ya Ziwa Asfari.

34Yonathani akampeleka ndugu yake Yohana pamoja na vikosi vya watu waliojiunga nao,

35kuwaomba rafiki zake Wanebayothi wampe ruhusa kuacha vitu vyao kwao, maana vilikuwa vingi sana.

36Lakini wana wa Ambri waliotoka Medaba walimkamata Yohana na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavichukua.

37Baada kitambo, Yonathani na nduguye Simoni waliletewa habari ya kuwa wana wa Ambri wanasherehekea arusi kubwa, na bibi arusi, binti wa mtu mkuu wa Kanaani,

38analetwa kutoka Nadabathi na jamii kubwa ya watu. Wakaikumbuka damu ya Yohana ndugu yao, wakaenda kujificha chini ya mlima.

39Wakainua macho yao wakatazama, wakaona ghasia nyingi, na mali nyingi; maana bwana arusi ametoka na rafiki zake na jamaa zake kuwalaki na matari na waimbaji na silaha nyingi.

40Wakatoka katika maoteo yao wakawapiga. Wengi waliuawa, na waliosalia walikimbia milimani, wakateka mali yao yote.

41Hivyo arusi iligeuka matanga, na sauti za waimbaji zikawa maombolezo.

42Nao baada ya kutoza kisasi cha damu ya ndugu yao, walirudi kwenye nchi ya matope kando ya Yordani.

Kuvuka Yordani

43Bakide alipopata habari, alifika ukingoni pa Yordani siku ya Sabato na jeshi lake lote.

44Yonathani akawaambia watu wake, Tusimame sasa, tujipiganie nafsi zetu, maana leo si kama jana au juzi.

45Hapa pana vita mbele yetu na nyuma yetu. Upande mmoja pana maji ya Yordani; upande mwingine mabwawa na msitu. Hakuna mahali pa kugeukia.

46Basi, zililieni mbingu, ili mwokolewe katika nguvu ya adui zetu.

47Vita vikaanza, Yonathani akanyosha mkono wake kumpiga Bakide, naye alirejea nyuma.

48Basi, Yonathani na watu wake walijitumbukiza katika Yordani wakaogelea mpaka ng'ambo; bali wao hawakuvuka kuwafuatia.

49Watu wa Bakide wasiopungua elfu moja waliuawa siku ile.

Bakide ajenga ngome

50Bakide na jeshi lake wakarudi Yerusalemu. Wakajenga miji yenye maboma katika Uyahudi, yaani ngome za Yeriko, Emao, Beth-horoni, Betheli, Timnathi, Farathoni na Tefoni, zenye kuta ndefu na malango na mapingo.

51Akaweka vikosi vya askari humo kupigana na Israeli.

52Akaimarisha mji wa Bethsura, na Gazara, na ngome ya Yerusalemu; akaweka askari humo, na akiba ya chakula.

53Akashika wana wa wakuu wa nchi wawe wadhamini, akawaweka katika ngome ya Yerusalemu chini ya ulinzi wa askari.

54Katika mwaka wa mia moja hamsini na tatu, mwezi wa pili, Alkimo alitoa amri kuubomoa ukuta wa ua wa ndani wa patakatifu, na hivyo aliiharibu kazi ya manabii.

55Wakati ule ule Alkimo alipigwa, asiweze kujimudu wala kusema sawasawa; mwili wake ukapoozwa, hata hakuweza kusema neno lolote wala kuagiza mambo ya nyumbani mwake.

56Akafa wakati huo na maumivu mengi.

57Naye Bakide, alipoona ya kuwa Alkimo amekufa, aliondoka akarudi tena kwa mfalme. Nchi ya Yuda ikatulia kwa muda wa miaka miwili.

Mwisho wa vita

58Kisha waasi wote walishauriana pamoja wakisema, Tazameni, Yonathani na watu wake wanastarehe sasa bila hofu. Basi, tumwite Bakide aje huku tena, awakamate wote kwa usiku mmoja.

59Wakaenda kufanya shauri naye.

60Akaondoka, akaja na jeshi kubwa; akapeleka barua kwa siri kwa rafiki zake wote waliokuwako Uyahudi kuwaagiza wamkamate Yonathani na wote waliokuwa pamoja naye. Lakini hawakuweza, kwa sababu shauri hili lilipata kujulikana.

61Basi, watu wa Yonathani walikamata watu wa nchi wapatao hamsini ambao walikuwa viongozi katika shauri baya hilo, wakawaua.

62Yonathani na Simoni na watu wao waliondoka wakaenda Bethbasi katika jangwa, wakajenga magofu yake iwe ngome imara.

63Bakide alipopata habari aliwakusanya watu wake wote, na kuwapelekea habari wale waliokuwako Uyahudi.

64Akaenda akapiga kambi yake kuelekea Bethbasi, akatengeneza mitambo ya vita, akaihusuru siku nyingi.

65Yonathani akamwacha nduguye Simoni humo mjini, naye mwenyewe akaondoka pamoja na kikosi kidogo akaenda mahali pengine.

66Akawapiga Odomera na jamaa zake, na Bani Fasironi katika mahema yao. Akawa akipigana nao na kufanya mashambulio kwa kikosi chake.

67Naye Simoni na watu wake walitoka mjini wakaiteketeza mitambo ya vita,

68akapigana na Bakide wakamshinda na kumsumbua sana; maana maandalio yake na mashambulio yake yalikuwa bure.

69Akawakasirikia sana wale waasi waliompa shauri aondoke airudie nchi yake.

70Yonathani alipopata habari hiyo, alituma wajumbe kwake kuomba afanye nao amani na kurudisha wafungwa wao.

71Akakubali, akafanya kama alivyosema, akamwapia ya kuwa hatamtenda mabaya siku zote za maisha yake.

72Akamrudishia wafungwa aliokuwa amewakamata zamani katika nchi ya Yuda.

73Akaondoka, akairudia nchi yake mwenyewe, wala hakuja tena mipakani kwao. Upanga ukakoma katika Israeli. Yonathani akafanya makao yake Mikmashi, akaanza kuamua watu, akawafutia wasio haki mbali na Israeli.

Uasi wa Iskanda Epifa ni

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya