The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupiga kambi juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia.[#Amu 21:8; 1 Sam 31:11-13; Mwa 26:28; Kut 23:32; 1 Fal 20:34; Ayu 41:4; Eze 17:13; #11:1 Au hivi, Lakini yeye akanyamaa Kimya, ndipo Nahashi…]
2Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hili mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kulia; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia.[#Mwa 34:14; 1 Sam 17:26]
3Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende kote mipakani mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutajisalimisha kwako.
4Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.[#1 Sam 10:26; 14:2; 2 Sam 21:6; Amu 2:4; 21:2; Rum 12:15]
5Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6Na Roho ya Mungu ikamjia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana.[#Amu 3:10; 6:34; 11:29; 13:25; 14:6; 1 Sam 10:10; 16:13]
7Akachukua fahali wawili waliofungwa nira, akawakatakata vipande, kisha akawatuma wajumbe kuvipeleka vile vipande kote katika Israeli, wakisema, Yeyote ambaye hatamfuata Sauli na Samweli, ng'ombe wake watafanyiwa vivi hivi. Basi utisho wa BWANA ukawaangukia wale watu, wakatoka kwa pamoja.[#Amu 19:29; 21:5; Mwa 35:5; 2 Nya 14:14; 17:10; Mit 14:26; Amu 20:1]
8Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa elfu mia tatu, na Wayuda elfu thelathini.[#Amu 1:5; 2 Sam 24:9]
9Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao wakafurahi.
10Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.
11Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya kambi kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hadi wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.[#1 Sam 31:11; Amu 7:16; Yak 2:13]
12Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue.[#1 Sam 10:27; Zab 21:8; Lk 19:27]
13Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israeli.[#2 Sam 19:22; Kut 14:13,30; 1 Sam 14:45; 19:5; 1 Nya 11:14; Zab 44:4-8; Ebr 2:3]
14Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuanzishe ufalme upya huko.[#1 Sam 10:8]
15Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za BWANA huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za BWANA; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.