The chat will start when you send the first message.
1Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu.[#1 Sam 8:5; 10:24; 11:14]
2Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo.[#Hes 27:17; 1 Sam 8:20]
3Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za BWANA, na mbele ya masihi wake, nilitwaa ng'ombe wa nani? Au nilitwaa punda wa nani? Au ni nani niliyemdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi.[#Hes 16:15; Mdo 20:33; 1 The 2:5; Kum 16:19; #12:3 Au mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]
4Nao wakasema, Hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote.
5Akawaambia, BWANA ni shahidi juu yenu, na masihi wake ni shahidi leo, ya kuwa hamkuona kitu mkononi mwangu. Nao wakasema, Yeye ni shahidi.[#Yn 18:38; Mdo 23:9; 24:16; 2 Kor 1:12; Kut 22:4; Zab 17:3; #12:5 Au mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]
6Samweli akawaambia watu, Ni yeye BWANA aliyewaweka Musa na Haruni, yeye ndiye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.[#Kut 6:26; Neh 9:9-14; Zab 77:19,20; Hos 12:13; Mik 6:4]
7Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za BWANA, kwa kutaja matendo yote ya haki ya BWANA, aliyowatendea ninyi na baba zenu.[#Isa 1:18; 5:3; Mik 6:2,3; Amu 5:11]
8Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia BWANA, ndipo BWANA akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa.[#Kut 2:23]
9Lakini wakamsahau BWANA, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao.[#Amu 3:12; 4:2; 13:1]
10Nao wakamlilia BWANA, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha BWANA, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa tuokoe kutoka kwa mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe.[#Amu 10:10-15]
11BWANA akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi kutoka kwa mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama.[#1 Sam 3:20; Amu 4:6; 7:1; 11:29]
12Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa BWANA, Mungu wenu, ni mfalme wenu.[#1 Sam 8:7,19; 10:19; Amu 8:23; Mwa 17:7]
13Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, BWANA ameweka mfalme juu yenu.[#Hos 13:11]
14Kama mkimcha BWANA, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya BWANA, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata BWANA, Mungu wenu, vema![#Kum 6:13; 10:12; 13:4; Yos 24:14; Zab 81:13; Mhu 8:12; Isa 3:10]
15Bali msipoisikia sauti ya BWANA, mkiiasi amri ya BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.[#Law 26:14; Kum 28:15; Yos 24:20]
16Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, BWANA atakalolitenda mbele ya macho yenu.
17Je! Leo si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA, kwamba atume ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu mlioufanya machoni pa BWANA, ni mwingi sana, kwa kujitakia mfalme.[#Mit 26:1; Yos 10:12; 1 Sam 7:9; Yak 5:16; 1 Sam 8:7; Hos 13:10]
18Basi Samweli akamwomba BWANA, naye BWANA akatuma ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa BWANA sana, na Samweli pia.[#Kut 14:31; Ezr 10:9]
19Watu wote wakamwambia Samweli, Tuombee watumishi wako kwa BWANA, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme.[#Mwa 20:7; Kut 9:28; 10:17; Zab 78:34,35; Mdo 8:24; Yak 5:15; 1 Yoh 5:16]
20Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa mioyo yenu yote.
21Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili,[#Yer 16:19; Hab 2:18; 1 Kor 8:4]
22visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana BWANA hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza BWANA kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe.[#Zab 106:8; Yer 14:21; Mal 1:2; Mt 11:26; Yn 15:16]
23Lakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka[#1 Kor 9:16; Mdo 12:5; Rum 1:9; Kol 1:9; 2 Tim 1:3; 1 Fal 8:36; 2 Nya 6:27; Yer 6:16]
24Mcheni BWANA tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu.[#Ezr 9:13]
25Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.[#Yos 24:20; Kum 28:36]