1 Samweli 24

1 Samweli 24

Daudi amhurumia Sauli

1Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi.[#1 Sam 23:28]

2Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.[#Zab 38:12]

3Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kwenda haja. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana.[#Amu 3:24; #24:3 Katika Kiebrania ni kufunika miguu.]

4Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yoyote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri.[#1 Sam 26:8]

5Lakini baadaye, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli.[#2 Sam 24:10]

6Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.[#1 Sam 26:11; 2 Sam 1:14; Ayu 31:29,30; #24:6 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]

7Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaruhusu kumshambulia Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake.[#Zab 7:4; Mt 5:44; Rum 12:17]

8Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hadi chini, akamsujudia.

9Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru?[#Zab 141:6; Mit 16:28; 17:9]

10Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.[#24:10 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]

11Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.[#Zab 7:3; 35:7; 1 Sam 26:20]

12BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako.[#Mwa 16:5; Amu 11:27; Ayu 5:8]

13Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako.

14Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto.[#1 Sam 26:20; Ayu 32:9; Mit 5:23; 1 Sam 17:43; 2 Sam 9:8]

15Basi BWANA atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe kutokana na mkono wako.[#2 Nya 24:22; Zab 35:1; 43:1; Mik 7:9]

16Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia.[#1 Sam 26:17]

17Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya.[#Mwa 38:26; Kut 9:27; Mt 5:44]

18Nawe umeonesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani BWANA aliponitia mikononi mwako, hukuniua.

19Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama? Basi BWANA na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo.

20Na sasa, angalia, ninajua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako.[#1 Sam 23:17; 2 Sam 3:17; Ayu 15:25; Mt 2:3-6,13,14]

21Basi sasa, uniapie kwa BWANA, ya kwamba hutawakatilia mbali wazao wangu baada yangu, wala hutaliharibu jina langu katika ukoo wa baba yangu.

22Naye Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akaenda zake kwao; lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya