1 Samweli 25

1 Samweli 25

Kufa kwa Samweli

1Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama.[#1 Sam 28:3; Isa 57:1,2; Mwa 50:11; Hes 20:29; Kum 34:8; Mdo 8:2; Mwa 14:6; Hes 12:16; Zab 120:5]

Kisha Daudi akaondoka, akashuka mpaka nyikani mwa Maoni.

Daudi na Mke wa Nabali

2Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa tajiri sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu moja; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake huko Karmeli.[#1 Sam 23:24; Yos 15:55; Mwa 38:13; 2 Sam 13:23]

3Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa mkosa adabu na mwovu; naye alikuwa wa ukoo wa Kalebu.[#Rut 4:11; Mit 14:1; 24:3,4; 31:10; Isa 32:5,7]

4Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake.[#Mwa 38:13; 2 Sam 13:23]

5Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mkampe salamu zangu;[#1 Sam 12:22; Mwa 37:14]

6na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao.[#2 Sam 18:28; 1 Nya 12:18; Zab 122:7; Mt 10:12,13; Lk 10:5]

7Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo wako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.

8Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, chochote kitakachokujia mkononi, uwape watumishi wako na mwanao Daudi.[#Neh 8:10; Est 9:19]

9Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali kama walivyoambiwa na Daudi, kisha wakanyamaza.

10Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake![#Amu 9:28; Zab 73:7,8; 123:3,4]

11Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao kondoo wangu manyoya, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?[#Amu 8:6]

12Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia kama walivyoambiwa.

13Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wakiwa kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao.[#1 Sam 30:24]

14Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, akasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana.

15Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu chochote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako malishoni;

16watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.[#Kut 14:22; Ayu 1:10; Zek 2:5]

17Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.

18Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliotayarishwa, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia moja vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.[#Mwa 32:13; 2 Sam 17:28,29; Mit 18:16; 21:14]

19Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.[#Mwa 32:16]

20Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kuteremka akiwa amekingwa na mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.

21Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu chochote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema.[#Mwa 44:4; Zab 35:12; 109:5; Mit 17:13; Yer 18:20; 1 Pet 2:20; 3:17]

22Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka.[#Rut 1:17; 1 Sam 3:17; 20:13,16]

23Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifudifudi, akainama mpaka chini.[#Yos 15:18; Amu 1:14]

24Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.

25Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.[#25:25 kwa maana ya mpumbavu.]

26Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.[#2 Fal 2:2; Mwa 20:6; Rum 12:19; 2 Sam 18:32]

27Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu.[#Mwa 33:11]

28Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote.[#2 Sam 7:11; 1 Fal 9:5; 1 Nya 17:16; 1 Sam 24:11]

29Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya kombeo.[#Kum 33:29; Zab 66:9; Mt 10:29,30; Mdo 17:28; Yer 10:18]

30Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli;

31hili halitakuwa kikwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako.

32Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;[#Mwa 24:27; Kut 18:10; Ezr 7:27; Zab 41:12,13; 72:18; Lk 1:68; 2 Kor 8:16]

33na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.

34Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba usingalifanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka.

35Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimelikubali ombi lako.[#1 Sam 20:42; 2 Sam 15:9; 2 Fal 5:19; Lk 7:50; Mwa 19:21]

36Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hadi kulipopambazuka.[#2 Sam 13:23; Mit 20:1; 23:29; Isa 5:11; 28:1-3; Hos 4:11; Lk 21:34; Efe 5:18]

37Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe.[#Kum 28:28; Ayu 15:21]

38Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hadi akafa.[#Kut 12:29; 2 Sam 6:7; Ayu 12:10; 34:14,15; Zab 104:29; Mdo 12:23]

39Naye Daudi aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.[#Mit 22:23; 2 Sam 3:28,29; 1 Fal 2:44; Est 7:10; Zab 7:16]

40Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe.

41Naye akainuka na kujiinamisha kifudifudi mpaka chini, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumishi wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.[#Rut 2:10,13; Mit 15:33; 18:12]

42Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe.

43Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wote wawili wakawa wake zake.[#Yos 15:56; 2 Sam 3:2; Mwa 2:24; 1 Sam 30:5; Mt 19:5,8]

44Lakini Sauli alikuwa amemposa Mikali, binti yake aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti, mwana wa Laisha aliyekuwa mtu wa Galimu.[#2 Sam 3:14-16; Isa 10:30]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya