1 Samweli 3

1 Samweli 3

Mungu amtokea Samweli na kumfanya nabii

1Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.[#Zab 74:9; Amo 8:11]

2Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),

3na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la BWANA, palipokuwa na sanduku la Mungu;[#Kut 27:21; 30:7,8; Law 24:3]

4basi, wakati huo BWANA akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.

5Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.

6BWANA akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.

7Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.[#Yer 9:24; Mdo 19:2]

8BWANA akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa BWANA ndiye aliyemwita yule mtoto.

9Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli, Nenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.

10BWANA akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.[#Zab 85:8; Mdo 9:6]

11BWANA akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.

12Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli kuhusu nyumba yake, tangu mwanzo hadi mwisho.[#1 Sam 2:30]

13Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.[#1 Sam 2:12]

14Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.[#Hes 15:30; Isa 22:14; Yer 7:16; Ebr 10:26-31]

15Naye Samweli akalala hadi asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya BWANA. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo.

16Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa.

17Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lolote katika hayo yote BWANA aliyosema nawe.[#Rut 1:17; Mt 26:63]

18Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lolote. Naye akasema, Ndiye BWANA; na afanye alionalo kuwa ni jema.[#Mwa 18:25; 1 Sam 16:10-12; Ayu 1:21; 2:10; Zab 39:9; Isa 39:8; 1 Pet 5:6]

19Samweli akakua, naye BWANA alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lolote lianguke chini.[#Mwa 39:2; 1 Sam 18:14; 2 Tim 4:22; 1 Sam 9:6]

20Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA.[#Amu 20:1]

21Naye BWANA akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.[#Mwa 12:7; 15:1; Hes 12:6; Amo 3:7; Ebr 1:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya