1 Timotheo 6

1 Timotheo 6

1Wote walio chini ya nira ya utumwa, wawachukulie bwana zao kama wanaostahili heshima yote, ili jina la Mungu na mafundisho yetu yasitukanwe.[#Efe 6:5; Tit 2:9,10]

2Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao wapatao faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa.[#Flm 1:16]

Mafundisho ya uongo na utajiri halisi

Mambo hayo uyafundishe na kuyahimiza.

3Mtu awaye yote akitoa mafundisho mengine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa,[#Gal 1:6-9; 2 Tim 1:13]

4amejivuna; wala hafahamu neno lolote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matusi, na shuku mbaya;

5na kuzozana miongoni mwa watu waliopotoka katika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.[#2 Tim 3:8; 4:4; Tit 1:14]

6Lakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.[#1 Tim 4:8; Ebr 13:5; Flp 4:11,12]

7Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;[#Mhu 5:14; Ayu 1:21]

8ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.[#Mit 30:8]

9Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na mtego, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, zinazowaingiza watu katika upotevu na uharibifu.[#Mit 23:4; 28:22]

10Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.[#Efe 5:5]

Vita vizuri vya imani

11Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, subira, upole.[#2 Tim 2:22]

12Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.[#1 Kor 9:25,26; 2 Tim 4:7]

13Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,[#Yn 18:36,37; 19:11]

14kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;

15ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;[#1 Tim 1:11; Ufu 17:14; Kum 10:17]

16ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyewahi kumwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.[#Kut 33:20]

17Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.[#Zab 62:10; Lk 12:20; Rum 12:16]

18Waamuru watende mema, wawe matajiri katika kutenda mema, wawe wakarimu na wawe tayari kushiriki na wengine;

19huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.[#Mt 6:20]

Maagizo kwa Timotheo na baraka

20Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na mazungumzo yasiyo ya kimungu, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo;[#1 Tim 4:7; 2 Tim 1:14]

21ambayo wengine kwa kuikiri wamepoteza Imani. Neema na iwe pamoja nanyi.[#1 Tim 1:6; 2 Tim 2:18]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya