2 Mambo ya Nyakati 26

2 Mambo ya Nyakati 26

Utawala wa Uzia

1Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, naye alikuwa mwenye miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa Amazia babaye.[#2 Fal 14:21,22; 15:1]

2Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.

3Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.

4Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye.

5Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha.[#2 Nya 24:2; Mwa 41:15; Dan 1:17; 2:19; 10:1]

6Akatoka akapigana na Wafilisti, akauvunja ukuta wa Gathi, na ukuta wa Yabne, na ukuta wa Ashdodi; akajenga miji katika Ashdodi na katikati ya Wafilisti.[#2 Nya 21:16; Isa 14:29]

7Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni.[#1 Nya 5:20; 2 Nya 14:11; 21:16; Mdo 26:22]

8Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka Misri; alipata nguvu nyingi.[#Mwa 19:38; 1 Sam 11:1; 2 Sam 8:2; 2 Nya 17:11]

9Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye Lango la Pembeni, na penye Lango la Bondeni, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu.[#2 Fal 14:13; Neh 3:13,19,32; Zek 14:10]

10Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabwawa mengi, maana alikuwa na ng'ombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima.[#2 Nya 21:16]

11Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, kulingana na hesabu walivyohesabu na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa makamanda wa mfalme.

12Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita.

13Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, elfu mia tatu na saba, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui.

14Uzia akawapatia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo.

15Huko Yerusalemu akatengeneza mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu mastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kurusha mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.

Kiburi na ukaidi

16Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia.[#Kum 32:15; 2 Nya 25:19; 32:25; Hab 2:4; Kol 2:18; Kum 8:14; 2 Fal 16:12,13]

17Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini wa BWANA, mashujaa;[#1 Nya 6:10]

18wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia, Si haki yako, Uzia, kumfukizia BWANA uvumba, ila ni haki ya makuhani wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba; toka katika patakatifu; kwa kuwa umekosa; wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa BWANA, Mungu.[#2 Nya 19:2; Yer 13:18; Mt 14:4; Gal 2:11; Hes 16:40; 18:7; Kut 30:7]

19Uzia akakasirika; naye alikuwa na chetezo mkononi cha kufukizia uvumba; naye hapo alipowakasirikia makuhani, ukoma ukamtokea katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa BWANA karibu na madhabahu ya kufukizia.[#Hes 12:10; 2 Fal 5:27]

20Azaria kuhani mkuu na makuhani wote wakamtazama, na angalia, alikuwa na ukoma pajini mwa uso, wakamtoa humo upesi; hata na yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu BWANA amempiga.[#Est 6:12]

21Uzia mfalme akawa na ukoma hadi siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya BWANA; na Yothamu mwanawe alikuwa kiongozi wa nyumba ya mfalme, akiwatawala watu wa nchi.[#2 Fal 15:5; Law 13:46; Hes 5:2]

22Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, aliyaandika Isaya nabii, mwana wa Amozi.[#Isa 1:1]

23Basi Uzia akalala na babaze; wakamzika karibu na babaze katika eneo la kuzikia la wafalme; kwa kuwa walisema, Huyu ni mwenye ukoma. Na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.[#Isa 6:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya