2 Mambo ya Nyakati 27

2 Mambo ya Nyakati 27

Utawala wa Yothamu

1Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.[#2 Fal 15:32; 1 Nya 3:12; Isa 1:1; Hos 1:1; Mik 1:1]

2Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, kama alivyofanya Uzia babaye; isipokuwa hakuingia hekaluni mwa BWANA. Lakini watu waliendelea kufanya maovu.[#2 Nya 26:16-21; Zab 119:120; 2 Fal 15:35]

3Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya BWANA, na juu ya ukuta wa Ofeli akajenga sana.[#2 Nya 33:14; Neh 3:26]

4Tena akajenga miji katika milima ya Yuda, na mwituni akajenga ngome na minara.

5Kisha akapigana na mfalme wa Waamoni, akawashinda. Na Waamoni wakampa mwaka ule ule talanta mia moja za fedha, na kori elfu kumi za ngano, na elfu kumi za shayiri. Hayo ndiyo waliyomtolea Waamoni, mwaka wa pili pia, na mwaka wa tatu.[#2 Nya 20:1; 26:8; 2 Fal 3:4; Yer 49:1-6]

6Basi Yothamu akawa na nguvu, kwa kuwa alizitengeneza njia zake mbele za BWANA, Mungu wake.[#1 Sam 2:30; 1 Nya 12:14; 19:3; Zab 34:8; 40:4]

7Na mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na vita vyake vyote, na njia zake, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda.

8Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita huko Yerusalemu.

9Yothamu akalala na babaze, wakamzika katika mji wa Daudi; na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya