The chat will start when you send the first message.
1Basi hayo yote yalipokwisha, Israeli wote waliokuwako wakatoka waende miji ya Yuda, wakazivunjavunja nguzo, wakayakatakata Maashera, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu katika Yuda yote na Benyamini, katika Efraimu pia na Manase, hadi walipoviharibu vyote. Ndipo wana wa Israeli wote wakarudi, kila mtu kwa milki yake, mijini kwao.[#2 Fal 18:4; 2 Nya 13:14]
2Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa kambi ya BWANA.[#1 Nya 23:6,30,31]
3Tena akaweka sehemu ya mfalme ya mali zake kwa sadaka za kuteketezwa, yaani, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na sadaka za kuteketezwa za sabato, na za mwezi mpya, na sikukuu, kama ilivyoandikwa katika Torati ya BWANA.[#Hes 28:1; 29:1]
4Tena akawaamuru watu waliokaa Yerusalemu, watoe sehemu ya makuhani na Walawi, ili hao wajibidiishe katika Torati ya BWANA.[#Hes 18:8; Neh 13:10; 1 Kor 9:13; Mal 2:7]
5Mara amri ilipovavagaa, wana wa Israeli wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, divai, mafuta, asali, na mazao yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta kwa wingi.[#Kut 22:29; 23:19; Law 25:23; Hes 18:12; Neh 13:12; Mit 3:9; Eze 20:40; 44:30; 1 Kor 15:20; Yak 1:18]
6Nao wana wa Israeli na Yuda, waliokaa mijini mwa Yuda, wakaleta pia zaka za ng'ombe na kondoo, na zaka za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyowekewa BWANA, Mungu wao, wakaviweka katika mafungu.[#Law 27:30; Kum 14:28]
7Katika mwezi wa tatu wakaanza kupanga mafungu hayo, wakayamaliza katika mwezi wa saba.
8Hata walipokuja Hezekia na wakuu, na kuyaona yale mafungu, wakamhimidi BWANA, na watu wake Israeli.[#Mwa 14:19; Kum 33:29; 2 Sam 6:18; 1 Fal 8:55,56; 2 Nya 6:3; Zab 33:12; 144:15]
9Ndipo Hezekia akauliza makuhani na Walawi kuhusu mafungu hayo.
10Azaria kuhani mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa BWANA, tumekula na kushiba, na kusaza tele; kwa kuwa BWANA amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.[#Hag 2:19; Mal 3:10]
11Ndipo Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa BWANA; wakavitengeneza.
12Wakayaingiza matoleo na zaka na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu; Konania, Mlawi aliwekwa kuwa mkuu na Shimei nduguye akawa masaidizi wake.[#Neh 13:13]
13Na Yehieli, Azaria, Nahathi, Asaheli, Yerimothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi, na Benaya, walikuwa wasimamizi chini ya mkono wa Konania na Shimei nduguye, kwa amri ya Hezekia mfalme, na Azaria mkuu wa nyumba ya Mungu.
14Na Kore, mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa mlango wa mashariki, alizisimamia sadaka za hiari za Mungu; ili kugawa matoleo ya BWANA, na vitu vilivyokuwa vitakatifu sana.
15Na chini yake walikuwa Edeni, na Minyamini, na Yeshua, na Shemaya, na Amaria, na Shekania, mijini mwa makuhani, kwa walivyoaminiwa, ili kuwagawia ndugu zao kwa zamu, wakuu na wadogo sawasawa;[#Yos 21:9; 1 Nya 9:22]
16zaidi ya wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wanaume, wenye miaka mitatu na zaidi, kila mmoja aliyeingia nyumbani mwa BWANA, kama ilivyopasa kazi ya kila siku, kwa huduma zao katika sehemu yao, kwa kadiri ya zamu zao;
17na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya makuhani kufuata nyumba za baba zao, na Walawi, wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, katika sehemu yao, kwa kadiri ya zamu zao;[#1 Nya 23:24,27]
18na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wadogo wao wote, wake zao, na wana wao, na binti zao, katika kusanyiko lote; kwani kwa vile walivyoaminiwa, wakajitakasa katika utakatifu;
19tena kwa ajili ya wana wa Haruni makuhani, waliokuwamo mashambani mwa malisho ya miji yao, mji kwa mji, kulikuwa na watu waliotajwa majina yao, ili kuwagawia sehemu wanaume wote miongoni mwa makuhani, na wote waliohesabiwa kwa nasaba miongoni mwa Walawi.[#Law 25:34; Hes 35:2; 2 Nya 31:12-15]
20Na hivyo ndivyo alivyofanya Hezekia katika Yuda yote; akatenda yaliyo mema, na ya adili, na uaminifu, mbele za BWANA, Mungu wake.[#1 Fal 15:5; 2 Fal 20:3; 22:2; Yn 1:47; 1 The 2:10]
21Na katika kila kazi aliyoanza kwa utumishi wa nyumba ya Mungu, na kwa torati, na kwa amri, ili kumtafuta Mungu wake, aliifanya kwa moyo wake wote, akafanikiwa.[#Kum 29:9; Yos 4:7; Zab 1:3; Mit 3:9; Mal 3:10; 1 Tim 4:8]