2 Mambo ya Nyakati 34

2 Mambo ya Nyakati 34

Utawala wa Yosia

1Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.[#1 Fal 3:7-9; 13:2; 2 Fal 22:1; 1 Nya 3:14,15; 2 Nya 35:25]

2Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kulia wala kwa kushoto.

3Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akiwa bado mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa Maashera, na sanamu za kuchonga, na za kusubu.[#1 Sam 1:24; Zab 119:9; Mit 8:17; Mhu 12:1; 2 Tim 3:15; 2 Nya 15:2; 1 Fal 13:2; 2 Nya 33:17,22]

4Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikatakata; Maashera, sanamu za kuchonga, na za kusubu, akazivunjavunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu.[#Law 26:30; 2 Fal 23:4; Kut 32:20]

5Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu.[#1 Fal 13:2]

6Na katika miji ya Manase, Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote.

7Akazibomoa madhabahu, akazipondaponda Maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikatakata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.[#Kum 9:21]

Kitabu cha Sheria chagunduliwa

8Hata katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake, alipokwisha kuisafisha nchi, na nyumba, akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, na Maaseya, mkuu wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, mwandishi wa kumbukumbu, waitengeneze nyumba ya BWANA, Mungu wake.[#2 Fal 22:3]

9Wakamjia Hilkia kuhani mkuu, wakampa fedha, iliyoletwa nyumbani mwa Mungu, waliyoikusanya Walawi, mabawabu, mikononi mwa Manase na Efraimu, na mabaki yote ya Israeli, na Yuda yote na Benyamini, na wenyeji wa Yerusalemu.[#2 Fal 12:4]

10Wakaitia mikononi mwa watenda kazi walioisimamia nyumba ya BWANA; na hao mafundi waliotenda kazi nyumbani mwa BWANA wakaitoa kwa kuitengeneza na kuifanya upya nyumba;

11wakawapa maseremala na waashi, ili wanunue mawe ya kuchonga, na miti ya kuungia, na kuitengeneza boriti kwa nyumba zile walizoziharibu wafalme wa Yuda.

12Nao watu wakatenda kazi kwa uaminifu; na wasimamizi wao walikuwa Yahathi na Obadia, Walawi, wa wana wa Merari; na Zekaria na Meshulamu, wa wana wa Wakohathi, ili kuihimiza kazi; na wengine katika Walawi, wote waliokuwa mastadi wa kupiga vinanda.[#2 Fal 12:15; 22:7; Neh 7:2; Mit 28:20; 1 Kor 4:2]

13Tena walikuwa juu ya wachukuzi wa mizigo, wakawahimiza wote waliotenda kazi ya huduma yoyote; na miongoni mwa Walawi kulikuwa na waandishi, na wasimamizi, na mabawabu.[#1 Nya 23:4,5; Ezr 7:6; Yer 8:8; Mt 26:3]

14Nao walipotoa ile fedha iliyoletwa nyumbani mwa BWANA, Hilkia kuhani akakiona kitabu cha Torati ya BWANA iliyotolewa kwa mkono wa Musa.[#Kum 31:24-26; 2 Fal 22:8]

15Akajibu Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, Kitabu cha Torati nimekiona nyumbani mwa BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu.

16Shafani akampelekea mfalme hicho kitabu, tena akampasha mfalme habari, akisema, Yote waliyokabidhiwa watumishi wako, wanayafanya.

17Nao wameimimina fedha iliyoonekana nyumbani mwa BWANA, nayo wameitia mikononi mwa wasimamizi, na mikononi mwa watenda kazi.

18Shafani mwandishi akamweleza mfalme, akisema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akasoma ndani yake mbele ya mfalme.[#Kum 17:19; Yos 1:8]

19Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya torati, aliyararua mavazi yake.[#Kum 28:1-68; Rum 3:20; 7:7-14; Gal 2:19; 3:10-13; Mwa 37:29; 2 Fal 19:1; Neh 8:9; Zab 94:12,13; 119:120; Yer 23:9,29; Yoe 2:13; Hab 3:16]

20Mfalme akawaamuru Hilkia, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Abdoni, mwana wa Mika, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, kusema,[#2 Fal 22:12]

21Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa hao waliosalia wa Israeli na wa Yuda, kuhusu habari za maneno ya kitabu kilichoonekana; maana ghadhabu ya BWANA ni nyingi iliyomwagika juu yetu, kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la BWANA, kutenda sawasawa na yote yaliyoandikwa kitabuni humo.[#2 Fal 17:6]

Nabii Hulda aombwa ushauri

22Basi Hilkia, na hao waliotumwa na mfalme, wakamwendea Hulda, nabii mwanamke, mkewe Shalumu, mwana wa Tohathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi; (naye alikuwa akikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili); wakasema naye kama hayo.[#Kut 15:20; Amu 4:4; Lk 2:36; Mdo 21:9; 2 Fal 22:14]

23Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,

24BWANA asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakazi wake, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda;[#Yos 23:16; 2 Fal 21:12; 23:26,27; 2 Nya 36:6,21; Isa 5:5; Yer 25:9; Dan 9:11-16; Amo 3:6; Zek 1:6]

25kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike.

26Lakini kwa mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kuhusu uliyoyasikia,

27kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakazi wake, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA.[#Zab 51:17; 86:5; Dan 9:9]

28Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari.

Agano lafanywa upya

29Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.[#2 Fal 23:1]

30Akapanda mfalme nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya Kitabu cha Agano kilichoonekana nyumbani mwa BWANA.

31Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo.[#2 Fal 11:14]

32Akawafanya wote walioonekana katika Yerusalemu na Benyamini walikubali. Na wenyeji wa Yerusalemu wakafanya kulingana na agano la Mungu, Mungu wa baba zao.

33Naye Yosia akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi zote zilizokuwa milki ya wana wa Israeli, akawafanya wote walioonekana katika Israeli kutumika, naam, wamtumikie BWANA, Mungu wao. Siku zake zote hawakuacha kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.[#1 Fal 11:5; Yer 3:10; 2 Nya 24:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya