2 Mambo ya Nyakati 35

2 Mambo ya Nyakati 35

Pasaka yaadhimishwa

1Naye Yosia akamfanyia BWANA Pasaka huko Yerusalemu; wakachinja Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.[#2 Fal 23:21; Kut 12:6; Hes 9:3; Ezr 6:19; Eze 45:21]

2Akawaweka makuhani katika kazi zao, akawatia moyo kutumika katika nyumba ya BWANA.[#2 Nya 23:18; Ezr 6:18; 1 Nya 22:19; 2 Nya 29:5,11]

3Akawaambia Walawi, waliowafundisha Israeli wote, waliotakasika kwa BWANA, Wekeni sanduku takatifu katika nyumba aliyoijenga Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli; hamtakuwa tena na mzigo mabegani; sasa mtumikieni BWANA, Mungu wenu, na watu wake Israeli.[#Kum 33:10; 2 Nya 30:22; 34:14; Mal 2:7; 2 Nya 5:7; 1 Nya 23:26]

4Mkajiweke tayari kwa kadiri ya nyumba za baba zenu, kwa zamu zenu, kama alivyoandika Daudi mfalme wa Israeli, na kama alivyoandika Sulemani mwanawe.[#1 Nya 9:10; 23:1; 24:1; 2 Nya 8:14]

5Mkasimame katika patakatifu, kama ndugu zenu wana wa watu walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, kadiri ya mgawanyiko wa kila nyumba ya baba, ya Walawi.[#Zab 134:1; #35:5 Katika Kiebrania maana yake sio dhahiri.]

6Mkachinje Pasaka, mkajitakase, mkawatengenezee ndugu zenu, kutenda sawasawa na neno la BWANA kwa mkono wa Musa.[#Kut 19:10; 2 Nya 29:5; 30:3,15; Ezr 6:20; Ayu 1:5; Zab 51:7; Yoe 2:16; Ebr 9:13,14]

7Tena Yosia akawapa watu, matoleo ya makundi, wana-kondoo na wana-mbuzi, yote yawe kwa ajili ya matoleo ya Pasaka, wote waliokuwako, wakiwa elfu thelathini, na ng'ombe elfu tatu; hao walitoka katika mali za mfalme.[#Mik 6:7; 2 Nya 30:24]

8Na wakuu wake wakawapa watu, na makuhani na Walawi matoleo ya hiari. Hilkia na wana na Yehieli, wakubwa wa nyumba ya Mungu, wakawapa makuhani, kuwa matoleo ya Pasaka, wana-kondoo elfu mbili na mia sita, na ng'ombe mia tatu.[#2 Kor 9:7]

9Konania naye, na Shemaya, na Nethaneli, ndugu zake, na Hashabia, na Yeieli, na Yozabadi, wakuu wa Walawi, wakawapa Walawi, kuwa matoleo ya Pasaka, wana-kondoo elfu tano na ng'ombe mia tano.

10Hivyo huduma ikatengenezwa, wakasimama makuhani mahali pao, na Walawi kwa zamu zao, kama alivyoamuru mfalme.[#Ezr 6:18]

11Wakachinja Pasaka, nao makuhani wakamimina damu waliyopokea mikononi mwao, Walawi wakachuna.[#Law 1:5,6; 2 Nya 29:22,34]

12Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape watu kama makundi yalivyo kwa kufuata nyumba za nasaba zao, ili wamtolee BWANA, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo.[#Law 3:3]

13Wakaioka moto Pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote.[#Kut 12:8; Kum 16:7; 1 Sam 2:13-15]

14Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni.

15Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.[#1 Nya 25:1; 9:17,18; 26:14]

16Basi huduma yote ya BWANA ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya Pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya BWANA, kama alivyoamuru mfalme Yosia.

17Wana wa Israeli waliokuwapo wakafanya Pasaka wakati ule, na sikukuu ya mikate isiyochachwa muda wa siku saba.[#Kut 12:15; 13:6; Law 23:5,8; Hes 28:16,17; Kum 16:3-8; 2 Nya 30:21; 1 Kor 5:7,8]

18Wala haikufanyika Pasaka kama ile katika Israeli tangu siku za nabii Samweli; wala wafalme wa Israeli hawakufanya hata mmoja wao Pasaka kama ile Yosia aliyoifanya, pamoja na makuhani, na Walawi, na Yuda wote na Israeli waliokuwapo, na wenyeji wa Yerusalemu.[#2 Fal 23:22,23]

19Katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Yosia ikafanyika Pasaka hiyo.

Kushinda kwa Farao Neko na kifo cha Yosia

20Baada ya hayo yote, alipokwisha Yosia kulitengeneza hekalu, Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana Karkemishi karibu na Frati; naye Yosia akatoka juu yake.[#2 Fal 23:29; Yer 46:2]

21Lakini Neko akatuma kwake wajumbe, kusema, Ni nini niliyo nayo mimi na wewe, Ee mfalme wa Yuda? Sikuja juu yako leo, lakini juu ya nyumba niliyo na vita nayo; naye Mungu ameniamuru nifanye haraka; acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu.[#2 Fal 18:25; Isa 36:10; Dan 4:35; #35:21 Katika Kiebrania hakuna jina Neko.]

22Lakini Yosia hakukubali kumwachia, akajibadilisha apate kupigana naye, asiyasikilize maneno ya Neko, yaliyotoka kinywani kwa Mungu, akaja kupigana bondeni mwa Megido.[#1 Fal 14:2; 22:30; 2 Nya 18:29]

23Nao wapiga upinde wakampiga Yosia; naye mfalme akawaambia watumishi wake, Niondoeni; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.[#1 Fal 22:34]

24Basi watumishi wake wakamtoa garini, wakamtia katika gari la pili alilokuwa nalo, wakamleta Yerusalemu; naye akafa, akazikwa makaburini mwa babaze. Watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakamlilia Yosia.[#2 Fal 23:30; Zek 12:11]

25Naye Yeremia akamlilia Yosia; na waimbaji wote wanaume kwa wawanawake wakamtaja Yosia katika maombolezo yao, hadi leo; hata wakayafanya kuwa ada kwa Israeli; nayo, tazama, yameandikwa katika Maombolezo.[#Yer 22:10; Omb 4:20; Mhu 12:5; Yer 9:17; Amo 5:16; Mt 9:23; Yer 22:20]

26Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na matendo yake mema, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika Torati ya BWANA,[#Zab 112:6; Mit 10:7; 22:1]

27na mambo yake, ya kwanza hadi ya mwisho, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya