The chat will start when you send the first message.
1Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme katika Yerusalemu mahali pa babaye.[#2 Fal 23:30; 2 Nya 26:1; 33:25]
2Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu.
3Naye mfalme wa Misri akamwondoa katika Yerusalemu, akaitoza nchi talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu.
4Mfalme wa Misri akamtawaza Eliakimu nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye, akamchukua mpaka Misri.[#Eze 19:3]
5Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, Mungu wake.[#2 Fal 23:36,37; Yer 36:1,27-32]
6Juu yake akakwea Nebukadneza, mfalme wa Babeli, akamfunga kwa pingu, amchukue mpaka Babeli.[#2 Fal 24:1,6; Eze 19:8,9; Dan 1:1,2; Hab 1:6,10; #36:6 Au, Nebukadreza.]
7Nebukadneza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya BWANA mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.[#Dan 1:1]
8Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na machukizo yake aliyoyafanya, nayo yaliyoonekana kwake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda; na Yekonia mwanawe akatawala mahali pake.[#1 Nya 3:16; #36:8 Au, Yehoyakini.]
9Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi; akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA.[#2 Fal 24:8]
10Mwaka ulipokwisha, Nebukadneza akatuma wajumbe, akamchukua mpaka Babeli; pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya BWANA; akamtawaza Sedekia nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu.[#Dan 1:1]
11Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;[#2 Fal 24:17; Yer 52:1]
12akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, Mungu wake; wala hakujinyenyekeza mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha BWANA.
13Tena akamwasi mfalme Nebukadneza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini akajifanyia shingo ngumu, akajitia moyo nguvu asimgeukie BWANA, Mungu wa Israeli.[#Kut 17:15; Yer 52:3; Eze 17:11-20; 2 Fal 17:14; Neh 8:16,17]
14Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno wakifuata machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya BWANA aliyoitakasa katika Yerusalemu.
15Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;[#Yer 25:3; Hos 11:8]
16lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.[#2 Nya 30:10; Zab 35:16; 74:1; Yer 5:12; 32:3; Mit 1:25; Lk 16:14]
17Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mnyonge; akawatia wote mkononi mwake.[#Kum 28:49; 2 Nya 33:11; Ezr 9:7]
18Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.[#2 Fal 25:13]
19Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani.[#2 Fal 25:9; Zab 74:6,7; Omb 4:1]
20Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;[#2 Fal 25:11; Yer 27:7]
21ili kulitimiza neno la BWANA kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.[#Yer 25:9; Law 26:34; 25:4,5]
22Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,[#Yer 29:10; Isa 44:28]
23Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.[#Dan 2:21]