2 Wakorintho 1

2 Wakorintho 1

Salamu

1Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya.[#Mdo 18:1; 1 Kor 1:1]

2Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.[#Rum 1:7]

Shukrani za Paulo baada ya dhiki

3Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;[#Rum 15:5; Efe 1:3; 1 Pet 1:3]

4atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.

5Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.[#Zab 34:19; 94:19]

6Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi.[#2 Kor 4:15,17]

7Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.

8Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.[#1 Kor 15:32; Mdo 19:23]

9Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,

10aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kuwa atazidi kutuokoa;[#2 Tim 4:18]

11ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu.

Kuahirishwa kwa ziara ya Paulo

12Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi.[#2 Kor 2:17; Ebr 13:18; 1 Kor 1:17]

13Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami natarajia ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho;

14vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kuwa sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu.[#2 Kor 5:12; Flp 2:16]

15Nami nikiwa na tumaini hilo nilitaka kufika kwenu hapo kwanza, ili mpate karama ya pili;

16na kupita kwenu na kuendelea mpaka Makedonia; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Yudea.[#Mdo 19:21; 1 Kor 16:5,6]

17Basi, nilipokusudia hayo, je! Nilitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo?[#2 Kor 5:16]

18Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na Siyo.

19Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na Siyo; bali katika yeye ni Ndiyo.[#Mdo 18:5]

20Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.[#Ufu 3:14]

21Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu,[#1 Yoh 2:27]

22naye ndiye aliyetutia mhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.[#2 Kor 5:5; Rum 8:16; Efe 1:13,14]

23Lakini mimi namwita Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho.[#2 Kor 11:31; Rum 1:9]

24Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama.[#1 Pet 5:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya