2 Wakorintho 13

2 Wakorintho 13

Maonyo zaidi

1Hii ndiyo mara yangu ya tatu kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.[#Kum 17:6; 19:15; Mt 18:16; 1 Tim 5:19]

2Nimetangulia kuwaambia; na, kama vile nilipokuwapo mara ya pili, vivyo hivyo sasa nisipokuwapo, nawaambia wazi wao waliotenda dhambi tangu hapo, na wengine wote, ya kwamba, nikija, sitahurumia;

3kwa kuwa mnatafuta dalili ya Kristo, asemaye ndani yangu, ambaye si dhaifu kwenu, bali ana uweza ndani yenu.

4Maana, alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Maana sisi nasi tu dhaifu katika yeye; lakini tutaishi pamoja naye kwa uweza wa Mungu ulio kwenu.[#Flp 2:7,8]

5Jichunguzeni wenyewe muone kama mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa iwe mmekataliwa.[#1 Kor 11:28]

6Lakini natumaini kama mtajua ya kuwa sisi hatukukataliwa.

7Nasi tunamwomba Mungu, msifanye lolote lililo baya; si kwamba sisi tuonekane tumekubaliwa, lakini ninyi mfanye lile lililo jema, ijapokuwa sisi tu kama waliokataliwa.

8Maana hatuwezi kutenda neno lolote kinyume cha kweli, bali kwa ajili ya kweli.[#1 Kor 13:6]

9Maana twafurahi, iwapo sisi tu dhaifu, nanyi mmekuwa hodari. Tena twaomba hili nalo, kutimilika kwenu.

10Kwa sababu hiyo, naandika haya nikiwa mbali nanyi, ili, nikija, nisiwe na ukali wa kadiri ya uwezo ule niliopewa na Bwana, kwa kujenga wala si kwa kubomoa.[#2 Kor 2:3; 10:8,11]

Salamu za mwisho na baraka

11Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.[#Flp 4:4; Rum 15:33]

12Salimianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wanawasalimu.[#1 Kor 16:20]

13Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya