The chat will start when you send the first message.
1Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei;[#2 Kor 3:6; 1 Kor 7:25]
2lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu.[#2 Kor 2:17; 1 The 2:5]
3Lakini ikiwa Injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;[#1 Kor 1:18]
4ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, wasiione nuru ya Injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.[#Ebr 1:3; Efe 2:2; 2 The 2:11; Kol 1:15]
5Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.[#2 Kor 1:24]
6Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.[#Mwa 1:3; 2 Kor 3:18; Isa 9:1]
7Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.[#2 Kor 5:1; Mdo 9:15]
8Pande zote twateseka, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;[#2 Kor 1:8; 7:5]
9twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;
10siku zote twabeba katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.[#1 Kor 15:31]
11Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.[#Rum 8:36]
12Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu.
13Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Niliamini, na kwa sababu hiyo nilinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena;[#Zab 116:10]
14tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuweka mbele yake pamoja nanyi.[#1 Kor 6:14]
15Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.[#2 Kor 1:3-6]
16Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.[#Efe 3:16]
17Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda mfupi tu, yatuandalia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;[#Rum 8:17,18]
18tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.[#Ebr 11:1,3; Kol 1:16]