The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.[#2 Fal 13:10; 2 Nya 25:1; #14:1 Au, Yoashi.]
2Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na tisa katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
3Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi.
4Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.[#2 Fal 12:3; 1 Fal 15:14; 22:43]
5Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake;
6ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe.[#Kum 24:16; Eze 18:4,20]
7Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.[#2 Nya 25:11; 2 Sam 8:13; Yos 15:38]
8Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.[#2 Nya 25:17,18; Mit 17:14]
9Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.[#Amu 9:8; 1 Fal 4:33]
10Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?[#Kum 8:14; 2 Nya 32:25; Eze 28:2,17; Hab 2:4; 2 Nya 35:21; Mit 26:17; Lk 14:31,32]
11Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda.[#Yos 21:16]
12Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.
13Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, dhiraa mia nne.[#2 Nya 25:23; Neh 8:16; 12:39; Yer 31:38; Zek 14:10]
14Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.[#1 Fal 7:51; 2 Fal 24:13]
15Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?[#2 Fal 13:12]
16Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake.
17Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano.[#2 Nya 25:25]
18Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?
19Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.[#2 Fal 12:20,21; 2 Nya 25:27; Yos 10:31]
20Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi.
21Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia.[#2 Fal 15:13; 2 Nya 26:1; #14:21 Au, Azaria.]
22Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.[#1 Fal 9:26; 2 Fal 16:6; Kum 2:8]
23Katika mwaka wa kumi na tano wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala katika Samaria; akatawala miaka arubaini na mmoja.
24Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; wala hakuyaacha makosa yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
25Yeye akaurudisha mpaka wa Israeli toka kuingia kwa Hamathi hata bahari ya Araba, sawasawa na neno la BWANA, Mungu wa Israeli, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, aliyekuwa wa Gath-heferi.[#Hes 13:21; 34:8; Eze 47:16-18; Amo 6:14; Kum 3:17; Yon 1:1; Mt 12:39; Yos 19:13]
26Kwani BWANA akayaona mateso ya Israeli, kwamba yalikuwa machungu sana; maana hakukuwa na mfungwa wala asiyefungwa, wala msaidizi kwa ajili ya Israeli.[#Kut 3:7,9; Amu 10:16; 2 Fal 13:4; Kum 32:36]
27Wala BWANA hakusema ya kwamba atalifuta jina la Israeli litoke chini ya mbingu; lakini akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.[#2 Fal 13:5]
28Basi mambo yote ya Yeroboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana, akawapatia tena Israeli Dameski na Hamathi, iliyokuwa kwanza ya Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?[#2 Sam 8:6; 1 Fal 11:24]
29Yeroboamu akalala na babaze, yaani, na wafalme wa Israeli. Na Zekaria mwanawe akatawala mahali pake.[#2 Fal 15:8]