2 Wafalme 15

2 Wafalme 15

Uzia atawala Yuda

1Katika mwaka wa ishirini na saba wa Yeroboamu mfalme wa Israeli Uziaf mwana wa Amazia mfalme wa Yuda akaanza kutawala.[#2 Fal 14:21; #15:1 Au, Azaria.]

2Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.

3Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia.

4Ila mahali pa juu hapakuondolewa, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.[#2 Fal 12:3]

5BWANA akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi.[#2 Nya 26:19; Law 13:46]

6Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, nayo yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?

7Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi; na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.[#2 Nya 26:23]

Zekaria atawala Israeli

8Katika mwaka wa thelathini na nane wa Uzia mfalme wa Yuda Zekaria mwana wa Yeroboamu akatawala juu ya Israeli katika Samaria miezi sita.

9Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyofanya babaze; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

10Na Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya fitina juu yake, akampiga mbele ya watu, akamwua, akatawala mahali pake.[#Hos 1:4; Amo 7:9; Ayu 18:5,11-21; 20:4-29; Zab 1:4; 37:37; Mit 2:22; 3:33; Mhu 8:12,13]

11Basi mambo yote ya Zekaria yaliyosalia, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli.

12Hilo ndilo neno la BWANA alilomwambia Yehu, akisema, Wana wako watakaa kitini mwa Israeli hata kizazi cha nne. Ikawa vivyo hivyo.[#2 Fal 10:30; Ayu 23:13; Zab 33:11; Isa 14:27; 40:8; Mt 24:35; 1 Pet 1:25]

Shalumu atawala Israeli

13Huyo Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda; akatawala muda wa mwezi mmoja katika Samaria.[#2 Nya 26:1; Mt 1:8]

14Menahemu mwana wa Gadi akapanda kutoka Tirza, akaja Samaria, akampiga Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamwua, akatawala mahali pake.[#Yos 12:24; 1 Fal 14:17; 15:21,33; Wim 6:4]

15Basi mambo yote ya Shalumu yaliyosalia, na njama alizozifanya, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli.

16Ndipo Menahemu akapiga Tifsa, na wote waliokuwamo, na mipaka yake, toka Tirza; kwa sababu hawakumfungulia, kwa hiyo akaupiga; nao wanawake wote waliokuwamo wenye mimba akawapasua.[#1 Fal 4:24; 2 Fal 8:12; 2 Nya 36:17; Isa 13:16,18; Eze 9:5,6,10; Hos 13:16]

Menahemu atawala Israeli

17Katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi katika Samaria.

18Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha siku zake zote makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

19Akaja Pulu mfalme wa Ashuru juu ya nchi; naye Menahemu akampa Pulu talanta elfu moja za fedha, ili kwamba mkono wake uwe pamoja naye, na ufalme uwe imara mkononi mwake.[#1 Nya 5:26; Isa 9:1; Hos 8:9; 2 Fal 14:5]

20Na Menahemu akawatoza Israeli fedha hiyo, yaani, matajiri wote wenye mali, kila mtu shekeli hamsini za fedha, ili ampe huyo mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akarejea, wala hakukaa huko katika nchi.

21Basi mambo yote ya Menahemu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?

22Menahemu akalala na babaze; na Pekahia mwanawe akatawala mahali pake.

Pekahia atawala Israeli

23Katika mwaka wa hamsini wa Uzia mfalme wa Yuda Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala juu ya Israeli hatika Samaria; akatawala miaka miwili.[#1 Fal 15:25; 16:8; 22:51; Ayu 20:5]

24Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

25Na Peka mwana wa Remalia, jemadari wake, akamfanyia uhaini, akampiga huko Samaria, katika ngome ya nyumba ya mfalme, pamoja na Argobu na Arie; na pamoja naye walikuwako watu hamsini wa Wagileadi. Akamwua, akatawala mahali pake.

26Basi mambo yote ya Pekahia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli.

Peka atawala Israeli

27Katika mwaka wa hamsini na mbili wa Uzia mfalme wa Yuda Peka mwana wa Remalia alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka ishirini.[#2 Nya 28:6; Isa 7:1]

28Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

29Katika siku za Peka mfalme wa Israeli akaja Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akatwaa Iyoni, na Abel-beth-maaka, na Yanoa, na Kedeshi, na Hazori, na Gileadi, na Galilaya, nchi yote ya Naftali; akawahamisha hao watu mpaka Ashuru.[#1 Nya 5:26; Isa 9:1; 1 Fal 15:20]

30Na Hoshea mwana wa Ela akamfitinia Peka mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, akatawala mahali pake, katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.

31Basi mambo yote ya Peka yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika Iitabu cha Kumbukumbu cha Wafalme wa Israeli.

Yothamu atawala Yuda

32Katika mwaka wa pili wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.[#1 Nya 3:12; 2 Nya 27:1; Mt 1:9]

33Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.

34Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA; akafanya kama yote aliyoyafanya Uzia baba yake.

35Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu walikuwa wakitoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya BWANA.[#2 Fal 15:4; 2 Nya 27:3]

36Basi mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?

37Zamani hizo akaanza BWANA kumtuma juu ya Yuda Resini mfalme wa Shamu, na Peka mwana wa Remalia.[#2 Fal 10:32; 2 Nya 28:6; 2 Fal 16:5; Isa 7:1]

38Yothamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi baba yake. Na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya