2 Wafalme 20

2 Wafalme 20

Kuugua kwa Hezekia

1Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.[#2 Nya 32:24; Isa 38:1; 2 Sam 17:23]

2Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA akasema,

3Nakusihi, BWANA, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.[#Neh 13:22; Zab 132:1-5; Isa 38:3; Mwa 5:22,24; 17:1; 1 Fal 3:6]

4Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la BWANA likamjia, kusema,

5Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa BWANA.[#1 Fal 18:37; 2 Fal 19:20; 2 Nya 32:20,21; Zab 65:2; 69:18,19; Lk 11:9,10; Mdo 10:31; Ayu 16:20; Zab 39:12; 56:8; Ufu 7:17]

6Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.[#2 Fal 19:34; 2 Nya 32:22]

7Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.

8Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba BWANA ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa BWANA.

9Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kwamba BWANA atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?[#Isa 38:7]

10Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.

11Isaya nabii akamlilia BWANA; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi.[#Yos 10:12-14; 2 Nya 32:24,31; Isa 38:8]

Wajumbe kutoka Babeli

12Wakati huo Merodak-baladani mwana wa Baladani, Mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana alipata habari kwamba Hezekia ameugua.[#Isa 39:1]

13Hezekia akawasikiliza, akawaonesha nyumba yote yenye vitu vyake vya thamani, fedha, na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yenye silaha zake, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake. Wala hapakuwa na kitu asichowaonesha Hezekia, katika nyumba yake, wala katika ufalme wake wote.[#2 Nya 32:27,31]

14Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Wasemaje watu hawa? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, yaani Babeli.

15Ndipo akasema, Wameona nini nyumbani mwako? Hezekia akajibu, Vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu wameviona; hapana kitu nisichowaonesha katika hazina zangu.

16Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la BWANA,

17Angalia, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hakitasalia kitu, asema BWANA.[#Law 26:33; 2 Fal 24:13; Yer 27:21; 52:17]

18Na baadhi ya wanao watakaotoka kwako, utakaowazaa, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi jumbani mwake mfalme wa Babeli.[#2 Fal 24:12,14; Dan 1:3]

19Ndipo Hezekia akamwambia Isaya, Neno la BWANA ulilolinena ni jema. Tena akasema, Je! Sivyo, ikiwapo amani na kweli katika siku zangu?[#1 Sam 3:18; Ayu 1:21; Zab 39:9; Omb 3:22,39]

Kifo cha Hezekia

20Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na ushujaa wake wote, tena alivyolifanya birika na mfereji, akaleta maji ndani ya mji, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?[#Neh 3:16]

21Hezekia akalala na baba zake; na Manase mwanawe akatawala mahali pake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya