2 Wafalme 22

2 Wafalme 22

Yosia atawala Yuda

1Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.[#1 Fal 13:2; 1 Nya 3:14; 2 Nya 34:1; Yer 1:2; Sef 1:1; Mt 1:10; Yos 15:39]

2Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kulia wala wa kushoto.[#Kum 5:32; Yos 1:7; Mit 4:27; Eze 18:14-17]

Hilkia agundua Kitabu cha Sheria

3Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema,[#2 Nya 34:8]

4Nenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu;[#2 Fal 12:4,9; 2 Nya 24:8-14; Mk 12:41,42; Neh 11:19; Zab 84:10]

5tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba;[#2 Fal 12:11-14]

6wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba.

7Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu.[#2 Fal 12:15; Neh 7:2; 1 Kor 4:2]

8Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha Torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma.[#Kum 31:24; 2 Nya 34:14]

9Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA.

10Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme.[#Yer 36:21]

11Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake.[#2 Nya 34:20]

12Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema,

13Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.[#Zab 25:14; Mit 3:6; Kum 29:27]

14Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii wa kike, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye.[#Kut 15:20; Amu 4:4; Lk 2:36; 1 Kor 11:5; 2 Nya 34:22]

15Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu,

16BWANA asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda;[#Kum 29:27; Dan 9:11-14]

17kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike.[#Zab 115:4; Isa 2:8,9; 44:17-20; 46:5-8; Mik 5:13]

18Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia,[#2 Nya 34:26; Mhu 8:12]

19kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekeza mbele za BWANA, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema BWANA.[#Zab 51:17; Isa 57:15; 66:2; Kut 10:3; Law 26:26-41; 1 Fal 21:29; 2 Nya 33:12; Zab 34:18; 51:17; Lk 14:11; 1 Pet 5:5,6; Yak 4:6,7; Yer 26:6; 44:22]

20Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani; wala macho yako hayatauona uovu huo wote nitakaouleta juu ya mahali hapa. Basi wakamletea mfalme habari tena.[#Zab 37:37; Isa 57:1,2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya