2 Wafalme 9

2 Wafalme 9

Kutawazwa kwa Yehu

1Nabii Elisha akamwita mmojawapo wa wana wa manabii, akamwambia, Jikaze viuno, ukachukue chupa hii ya mafuta mkononi mwako, ukaende Ramoth-Gileadi.[#1 Fal 20:35; Yer 1:9,10,17; 2 Fal 4:29; 8:28]

2Utakapofika huko, mtafute Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, ukaingie, ukamtoe miongoni mwa ndugu zake, ukamchukue katika chumba cha ndani.

3Kisha, ukatwae ile chupa ya mafuta, ukayamimine juu ya kichwa chake, ukaseme, BWANA asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Kisha ufungue mlango ukakimbie, wala usikawie.[#1 Fal 19:16]

4Basi yule kijana, yule nabii kijana, akaenda Ramoth-Gileadi.

5Naye alipofika, tazama, majemadari wa jeshi walikuwa wamekaa; naye akasema, Nimetumwa na neno kwako, Ee jemadari; Yehu akasema, Kwa yupi miongoni mwetu sote? Akasema, Kwako wewe, Ee jemadari.

6Akainuka akaingia nyumbani; naye akayamimina yale mafuta kichwani mwake, akamwambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa BWANA, yaani, juu ya Israeli.[#1 Sam 2:7,8; 2 Nya 22:7; Zab 75:6,7; 83:18; Yer 27:5; Dan 2:21; 4:17,25; 5:21]

7Nawe utawapiga nyumba ya Ahabu, bwana wako, ili nijilipize kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii, na damu ya watumishi wote wa BWANA, mkononi mwa Yezebeli.[#Zab 58:10,11; 116:15; 1 Fal 18:4; 21:15]

8Kwa maana nyumba yote ya Ahabu wataangamia; nami nitamkatilia mbali kila mwanamume wa nyumba ya Ahabu, yeye aliyefungwa, na yeye asiyefungwa, katika Israeli.[#1 Fal 14:10; 21:21; Zab 76:8-12; 110:5; 1 Sam 25:22; Kum 32:36]

9Nami nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.[#1 Fal 14:10; 15:29; 21:22; 16:3]

10Na mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli, wala hapatakuwa na mtu wa kumzika. Akaufungua mlango, akakimbia.[#1 Fal 14:10,11; 21:23; 2 Fal 9:35-37; Yer 15:3; 36:30]

11Ndipo Yehu akatoka akawaendea watumishi wa bwana wake. Mmoja wao akamwuliza, Je! Ni amani? Huyu mwenye wazimu amekujia kwa nini? Akawaambia, Ninyi mnamjua mtu huyu na habari ya maneno yake.[#Yer 29:26; Hos 9:7; Mk 3:21; Yn 10:20; Mdo 17:18; 26:24; 1 Kor 4:10; 2 Kor 5:13]

12Wakasema, Ni uongo; haya, tuambie. Akasema, Aliniambia haya na haya, akisema, BWANA asema hivi, Nimekutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli.

13Basi wakafanya haraka, kila mtu akalitwaa vazi lake, na kulitia chini yake juu ya madaraja, wakapiga baragumu wakasema, Yehu ni mfalme.[#Mt 21:7; Mk 11:7,8]

Yoramu wa Israeli auawa

14Hivyo Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akamfitinia Yoramu.

Basi Yoramu alikuwa akiulinda Ramoth-Gileadi, yeye na Israeli wote, kwa sababu ya Hazaeli mfalme wa Shamu.

15Lakini mfalme Yoramu mwenyewe alikuwa amerudi, apate kupona majeraha yake aliyotiwa na Washami, alipokuwa akipigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Yehu akasema, Kama hii ndiyo nia yenu, basi, msimwache hata mtu mmoja atoke mjini, ili aende kupeleka habari Yezreeli.[#2 Fal 8:29; 2 Nya 22:6]

16Basi Yehu akapanda gari lake kwenda Yezreeli; kwa maana Yoramu alikuwa amelala huko; na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameshuka ili kumtazama Yoramu.

17Basi mlinzi alikuwa anasimama juu ya mnara wa Yezreeli, akaliona lile kundi la watu wa Yehu, alipokuwa akija, akasema, Naona kundi la watu. Yoramu akasema, Haya! Mtwae mpanda farasi mmoja, ukampeleke aende kuwalaki, na kuwauliza, Je! Ni amani?

18Basi mpanda farasi mmoja akatoka awalaki, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Yule mjumbe amewafikia, lakini harudi tena.

19Ndipo akapeleka mpanda farasi wa pili, naye akawafikia, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate.

20Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Amewafikia wala harudi tena; na mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; maana analiendesha gari kwa kasi.

21Yoramu akasema, Tandika gari. Wakalitandika gari lake. Yoramu mfalme wa Israeli akatoka, na Ahazia mfalme wa Yuda, kila mtu katika gari lake. Wakatoka ili kumlaki Yehu, wakamkuta katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli.[#2 Fal 8:29; 10:13,14; 2 Nya 22:7]

22Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?[#1 Fal 14:30-31; Isa 47:9,11; Nah 3:4; Ufu 2:20; 17:1-5; 18:3]

23Yoramu akageuza mikono yake, akakimbia, akamwambia Ahazia, Ni uhaini, Ahazia.

24Yehu akavuta upinde wake kwa nguvu zake zote, akampiga Yoramu kati ya mikono yake, hata mshale ukamtoka penye moyo wake, akaanguka katika gari lake.

25Ndipo Yehu akamwambia Bidkari, msaidizi wake, Mtwae ukamtupe katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli; maana kumbuka, hapo mimi na wewe tulipokuwa tumepanda farasi zetu, na kumfuata Anabu baba yake, BWANA alimwekea mzigo huu, akasema;[#1 Fal 21:29; Yer 23:33-38; Nah 1:1; Mt 11:30]

26Hakika, jana nimeiona damu ya Nabothi, na damu ya wanawe, asema BWANA; nami nitakulipa katika kiwanja hiki, asema BWANA. Basi sasa mtwae huyu ukamtupe katika kiwanja hicho, sawasawa na neno la BWANA.[#1 Fal 21:19; 22:38; Est 7:10]

Ahazia wa Yuda auawa

27Na Ahazia mfalme wa Yuda alipoona hayo, akakimbia kwa njia ya nyumba ya bustanini. Yehu akamfuatia, akasema, Mpigeni huyu naye katika gari lake; wakampiga hapo penye kupandia Guri, karibu na Ibleamu. Akakimbilia Megido, akafa huko.[#Amu 1:27; 5:19; 1 Fal 9:15; 2 Nya 22:9; 35:22; Zek 12:11]

28Na watumishi wake wakamchukua garini mpaka Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake pamoja na baba zake katika mji wa Daudi.

29Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda.

Malkia Yezebeli auawa kikatili

30Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani.[#Yer 4:30]

31Hata Yehu alipoingia lango la mji, alisema, Je! Ni amani, Ewe Zimri, mwenye kumwua bwana wako?[#1 Fal 16:9-20]

32Akainua uso wake kulielekea dirisha, akasema, Aliye upande wangu ni nani? Matowashi wawili watatu wakachungulia.

33Akasema, Mtupeni chini. Basi wakamtupa chini; na damu yake ikamwagika nyingine juu ya ukuta, na nyingine juu ya farasi, naye akamkanyagakanyaga.

34Alipoingia, akala, na kunywa; kisha akasema, Haya! Mwangalieni mwanamke huyu aliyelaaniwa, mkamzike; kwa maana ni binti mfalme.[#Mit 10:7; Isa 65:15; 1 Fal 16:31]

35Wakaenda ili kumzika; lakini hawakuona kitu ila kifuvu cha kichwa chake, na miguu yake, na vitanga vya mikono yake.

36Basi wakarudi, wakampasha habari. Akasema, Hili ndilo neno la BWANA, alilolinena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya, Mtishbi, kusema, Katika kiwanja cha Yezreeli mbwa wataila nyama ya Yezebeli.[#Nah 1:2; Hab 2:4; 1 Fal 21:23]

37Na mzoga wa Yezebeli utakuwa kama mavi juu ya uso wa mashamba, katika kiwanja cha Yezreeli; hata wasipate kusema, Huyu ni Yezebeli.[#Zab 83:10; Yer 8:2; 16:4]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya