2 Wamakabayo 12

2 Wamakabayo 12

Matukio katika Yafa na Yamnia

1Mapatano hayo yakiisha kufanywa, Lisia alirejea kwa mfalme, na Wayahudi walishughulika na kazi zao za shambani.

2Lakini viongozi wengine wa pande zile, Timotheo na Apolonio mwana wa Geneo, pamoja na Hieronimo na Demofono, na Nikano, kiongozi wa Kipro, hawakuwaacha watulie na kukaa kwa amani.

3Watu wa Yafa walitenda jambo baya kabisa. Waliwaalika Wayahudi waliokaa nao mjini, pamoja na wake zao na watoto wao, waingie katika mashua walizoziweka tayari, kana kwamba hawana nia mbaya yoyote kwao.

4Wayahudi walikubali wakitegemea sheria ya mji; maana walitaka kukaa kwa amani, wala hawakushuku neno lolote. Lakini walipofika kilindini watu wa Yafa walizamisha watu wasiopungua mia mbili na kuwafisha majini.

5Yuda aliposikia habari za ukatili huo waliofanyiwa Wayahudi wenzake, aliwakusanya watu wake.

6Akamwomba Mungu, Mwamuzi mwenye haki, akawaendea wale wauaji wa ndugu zake. Usiku akaichoma moto bandari na kuviteketeza vyombo, akaua kwa upanga wale waliojificha huko.

7Watu wakamfungia milango ya mji, akaondoka, akikusudia kuja tena na kuwaangamiza kabisa watu wa Yafa wote.

8Akapata habari kama watu wa Yamnia wanakusudia kuwamaliza Wayahudi wa kwao vivyo hivyo,

9akawashambulia usiku akateketeza bandari yao na vyombo vyao, hata mng'ao wa moto ulionekana Yerusalemu, mbali ya maili thelathini.

Shughuli za vita katika Gileadi

10Ikawa walipofika kiasi cha maili moja na zaidi kidogo kutoka pale, njiani kwenda kwa Timotheo, walishambuliwa na kundi la Waarabu wasiopungua tano elfu, pamoja na wapanda farasi mia tano.

11Mapigano yalikuwa makali sana, lakini Yuda na watu wake walishinda kwa msaada wa Mungu. Wale wahamaji waliposhindwa, walimwomba Yuda afanye urafiki nao, wakiahidi kumpa wanyama na kuwasaidia kwa njia nyinginezo.

12Yuda akaona ya kuwa wataweza kumfaa kwa mambo mengi, akakubali kufanya mpatano nao. Wakapeana mikono, kisha wakaenda zao mahemani kwao.

13Alishambulia mji mwingine pia, uliozungukwa maboma na kuta, walimokaa watu wa mataifa mbalimbali, jina lake Kaspini.

14Wenyeji wake, wakizitegemea kuta zao imara na akiba yao kubwa ya chakula, waliwadhihaki Yuda na watu wake, wakikufuru na kulaumu vibaya sana.

15Lakini Yuda na watu wake walimwomba Mfalme mkuu wa ulimwengu, yule ambaye aliuangusha mji wa Yeriko zamani za Yoshua bila mitambo ya kubomolea au silaha nyinginezo.

16Wakazishambulia kuta kwa ukali, wakautwaa mji kwa mapenzi ya Mungu. Wakaua watu wengi wasio hesabika, hata ziwa lililokuwapo karibu, lenye upana wa robo maili, lilionekana limejaa kwa wingi wa damu.

Yuda ashinda jeshi la Timotheo

17Wakaendelea mbele kiasi cha maili tisini, wakafika Karaka, walipokaa Wayahudi waitwao Watobu.

18Hawakumkuta Timotheo huko; alikuwa ameondoka bila kufanya kitu, akiacha kikosi kikubwa cha askari katika ngome fulani.

19Dositheo na Sosipatro, majemadari wa Makabayo, wakaenda huko wakawaua wale walioachwa na Timotheo ngomeni, zaidi ya elfu kumi.

20Makabayo naye alipanga jeshi lake vikosi vikosi, akaweka mkuu juu ya kila kikosi, akaenda mbio kumfuatia Timotheo, ambaye alikuwa na askari elfu mia moja na ishirini na wapanda farasi elfu mbili na mia tano.

21Timotheo alipopata habari za kuja kwake Yuda, aliwaondoa wanawake na watoto, pamoja na mizigo, akawapeleka mbele kwenye mahali paitwapo Karnaimu, ngome iliyokuwa ngumu ya kuhusuriwa au kukaribiwa kwa sababu njia za kuiendea pande zote zilikuwa nyembamba sana.

22Lakini kikosi cha kwanza cha Yuda kilipotokea, adui walishikwa na woga mkubwa kwa sababu ya kutokewa na maono ya Yule mwenye kuona yote, wakakimbiana kasi huku na huko, hata mara nyingi waliumizana na kuchomana kwa panga zao wenyewe.

23Yuda akawafuatia hima, akawaua wale wabaya kwa upanga na kuangamiza watu wapatao elfu thelathini.

24Timotheo mwenyewe alikutwa na vikosi vya Dositheo na Sosipatro. Akawabembeleza kwa ujanja mwingi wamwache aende zake, akisema kwamba wazazi wa wengi wao, na ndugu za wengine, wamo mikononi mwake, na kama yeye haachiliwi wao hawatahurumiwa.

25Basi, akiisha kuapa kwa maneno mengi kwamba atawaacha hao waende zao salama, walimweka huru ili kuwaokoa ndugu zao.

Yuda aendelea kujipatia ushindi

26Kisha Yuda alishambulia Karnaimu na hekalu la Atergati, akaua watu elfu ishirini na tano.

Wayahudi warudi kupitia Efroni na Skithapoli

27Na baada ya maangamizi hayo na uuaji aliuendea Efroni, mji wenye boma, alipokaa Lisia na watu wengi wa mataifa mbali mbali. Vijana wenye nguvu waliopangwa ukutani wakawazuia kwa juhudi, na ndani mlikuwa na akiba kubwa ya mitambo na silaha.

28Lakini Wayahudi walimwomba Mfalme ambaye avunja nguvu ya adui kwa uweza wake, wakautwaa mji, wakaangamiza watu elfu ishirini na tano katika wale waliokuwamo.

29Kutoka huko wakaenda Skithapoli kwa haraka, mwendo wa maili sabini na tano kutoka Yerusalemu.

30Lakini Wayahudi waliokaa huko waliishuhudia nia njema ya Waskithapoli, na hisani yao wakati wa shida;

31kwa hiyo waliwashukuru tu, wakawasihi waendelee kuliangalia taifa lao kwa wema hata wakati ujao. Ndipo wakaenda Yerusalemu kwa kuwa Idi ya Majuma ilikuwa karibu.

Yuda amshinda Gorgia

32Baada ya sikukuu iitwayo Pentekoste walifanya haraka kumwendea Gorgia, kiongozi wa Idumia, ili kupigana naye.[#Kut 23:16]

33Akatoka kuwalaki na askari elfu tatu na wapanda farasi mia nne.

34Katika vita hivyo, Wayahudi wachache walianguka.

35Lakini Dositheo, mmoja wa Watobu, mpanda farasi hodari sana, alimshika Gorgia, akalikamata vazi lake na kumkokota kwa nguvu, akitaka kumtwaa huyu mlaaniwa yu hai. Lakini mpanda farasi mmoja wa Thraka alimjia kwa nguvu akamtia jeraha begani, na hivyo Gorgia aliokoka akakimbilia Marisa.

36Ezri na watu wake walipoanza kuchoka kwa vita virefu, Yuda alimwita BWANA ajioneshe kuwa yu msaidizi wao na kiongozi wao katika mapigano.

37Ndipo alipaza mlio wa vita na nyimbo, kwa lugha yao wenyewe, akawashambulia askari za Gorgia kwa ghafla akawakimbiza.

Maombi kwa ajili ya waliouawa vitani

38Baada ya hayo Yuda akaondoka na jeshi lake akaenda mji wa Abdulamu, wakajitakasa kama kawaida kwa kuwa siku ya saba ilikuwa karibu; wakaishika Sabato pale.

39Asubuhi yake, askari wa Yuda walikwenda kuziokota maiti (jambo lililowapasa wafanye bila kukawia zaidi) na kuwaleta wazikwe na jamaa zao katika makaburi ya baba zao.

40Ndipo walipoona talasimu chini ya nguo za kila mmoja, yaani sanamu ndogo za miungu ya Yamnia, ambazo zilikatazwa kabisa kwa Wayahudi kwa sheria.[#Kum 7:25]

41Wote wakaona dhahiri sababu ya kuuawa kwao, wakamhimidi BWANA, Mwamuzi mwenye haki, afunuaye yaliyo ya siri,

42wakajitia katika sala, wakiomba ile dhambi iliyotendwa ifutwe kabisa. Yuda, mtu mwadilifu, akawaonya watu wajitenge na dhambi, madhali wameona kwa macho yao wenyewe matokeo ya ile dhambi ya wale waliokufa.

43Akachanga fedha kwa kila mtu jumla drakma elfu mbili, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi. Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki, kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu.

44Maana kama asingalitumanini ya kuwa wale waliokufa watafufuka, ingalikuwa kazi bure isiyo na maana kuwaombea wafu.

45Lakini kwa kuwa aliufikiri utukufu wa thawabu waliyowekewa wale wafao katika utauwa, wazo lake lilikuwa takatifu na la kicho.

46Ndiyo sababu alifanya upatanisho kwa wafu ili wafunguliwe dhambi yao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya