2 Wamakabayo 3

2 Wamakabayo 3

3. HABARI ZA HELIODORO

Heliodoro afika Yerusalemu

1Zamani mji mtakatifu ulikaliwa kwa amani kabisa, na sheria ilishikwa sawasawa, kwa sababu ya wema wa Oniasi, kuhani mkuu, na jinsi alivyochukia uovu.

2Hata wafalme walipastahi mahali patakatifu na kulitukuza hekalu kwa zawadi bora sana.

3Hivyo, Seleuko, mfalme wa Asia, alilipa gharama zote za matoleo ya dhabihu kwa fedha ya hazina yake mwenyewe.

4Lakini mtu mmoja wa ukoo wa Benyamini, Simoni, aliyekuwa msimamizi wa hekalu, alikosana na kuhani mkuu juu ya madaraka ya soko la mji.

5Alipoona hawezi kumshinda Oniasi, alimwendea Apolonio wa Tarso, ambaye wakati huo alikuwa jemadari mkuu wa Koele-Shamu na Foinike,

6akamwambia ya kuwa hazina ya Yerusalemu imejaa mali, hata fedha iliyopo haihesabiki kwa wingi wake. Alisema fedha hiyo haimo katika hesabu iliyowekwa kwa gharama za dhabihu, na huenda ingewezekana kuchukuliwa na mfalme.

7Naye Apolonio, alipozungumza na mfalme, alimpa habari alizozisikia juu ya fedha hiyo Mfalme akamwita Heliodoro, waziri wake, akampeleka na amri ya kuishika mali hiyo.

8Heliodoro akaondoka mara, akifanya kama anataka kuikagua miji ya Koele-Shamu na Foinike, lakini nia yake kwa kweli ilikuwa kulitimiza kusudi la mfalme.

9Alipofika Yerusalemu alipokewa vizuri na kuhani mkuu na watu wa mji. Akawaambia habari alizozipata na sababu ya kuja kwake. Akauliza kama habari hiyo ni kweli.

10Kuhani mkuu akamweleza ya kuwa ni kweli kuna fedha iliyowekwa kwake, lakini ni mali ya wajane na yatima.

11Sehemu nyingine ni mali ya Hirkano mwana wa Tobia, mtu wa cheo kikuu (si kama alivyosingiziwa na yule mtovu wa dini, Simoni). Nayo yote pamoja haizidi talanta mia nne za fedha na mia mbili za dhahabu.

12Tena, haiwezekani kabisa kuwadhulumu watu walioweka tumaini lao kwa utakatifu wa mahali na kwa enzi na salama ya hekalu lililothaminiwa duniani kote.

Mpango wa Heliodoro wa kuibia hekalu

13Lakini Heliodoro, aliyekuwa amepewa amri na mfalme, alijibu kwamba hata hivyo ni lazima fedha hizo zichukuliwe kwa hazina ya mfalme.

14Basi, akiisha kuweka siku, aliingia ili kuiangalia hesabu ya mali. Kulikuwa na huzuni nyingi mjini mwote.

15Makuhani, hali wamevaa mavazi yao ya kikuhani, walianguka kifudifudi mbele ya madhabahu, wakapaza sauti zao mbinguni wakimsihi Yeye aliyekuwa ameitoa sheria juu ya vitu vilivyowekwa akiba, na kumwomba ailinde mali hiyo kwa ajili yao walioiweka.

16Hakuna aliyeweza kuutazama uso wa kuhani mkuu bila kuchomwa moyoni. Sura yake ilivyobadilika rangi ilionesha uchungu wa roho yake.

17Hofu na tetemeko la mwili lililomshika liliwadhihirishia wale waliomtazama huzuni aliyokuwa nayo moyoni.

18Nao watu wa mjini walitoka mbio nyumbani mwao kwa wingi ili kushirikiana katika sala, wakiomba mahali pasiaibishwe.

19Wanawake, hali wamejifunga gunia kifuani, walisongana njiani. Na wanawali wasioruhusiwa kutoka nje walikwenda mbio, wengine kuchungulia madirishani.

20Wote waliinua mikono yao kuelekea mbinguni wakitoa dua zao.

21Hakuna budi kuwahurumia makutano waliokuwa wameanguka kifudifudi wote, na kuhani mkuu katika fadhaa yake na hofu yake ya mambo yatakayotendeka.

Bwana alinda hekalu lake

22Basi, hapo watu walikuwa wakimsihi Mwenyezi Mungu, ailinde salama salimini ile mali iliyowekwa kwake kwa ajili yao walioiweka;

23na hapo Heliodoro amejiweka tayari kuitimiza amri aliyopewa.

Adhabu ya Heliodoro

24Lakini yeye na kikosi chake wakiisha fika mbele ya nyumba ya hazina, mara BWANA wa roho zote na wa mamlaka yote alileta maono ya ajabu, hata wote waliothubutu kufuatana naye waliushtukia uweza wa Mungu wakazimia kwa hofu nyingi.

25Maana waliona farasi mwenye mpandaji wa kutisha na matandiko ya fahari, naye alimwelemea Heliodoro na kumshambulia kwa miguu yake ya mbele. Mpandaji wake alionekana kama amevaa deraya ya dhahabu.

26Vijana wengine wawili walitokea mbele yake, wenye nguvu za ajabu, wazuri mno, wamevaa nguo za fahari; wakisimama kando yake, mmoja huku na mmoja huko, wakampiga bila kukoma, wakimpa mapigo mabaya mengi.

27Akaanguka chini ghafla, giza nene likamfunika. Watu wake wakamwinua, wakamweka katika machela, wakamchukua.

28Huyu aliyekuwa anaingia sasa hivi katika nyumba ya hazina pamoja na wafuasi wake na kundi zima la askari walinzi, sasa yu hoi, amedhihirishiwa waziwazi enzi ya Mungu.

Oniasi amwombea Heliodoro

29Kwa kazi ya Mungu ameangushwa, hana uwezo wa kusema, wala tumaini la kupona.

30Wayahudi wakamsifu Mungu aliyepatukuza kwa ajabu mahali pake, hata hekalu, ambalo sasa hivi lilijaa hofu na wasiwasi, lilikuwa limejaa furaha na shangwe kwa ufunuo wa BWANA Mwenyezi.

31Basi, bila kukawia, sahibu zake Heliodoro walimsihi Oniasi amsihi Aliye Juu ili kwa rehema zake amjalie uzima huyu aliye kufani.

32Naye kuhani mkuu, akidhani moyoni mwake ya kuwa mfalme aweza kuwashuku Wayahudi kama ndio waliomtenda Heliodoro mabaya, alitoa dhabihu kwa kupona kwake.

33Ikawa, wakati kuhani mkuu alipokuwa akifanya kipatanisho, wale vijana walimtokea Heliodoro tena wamevaa nguo zile zile, wakasimama pale wakasema, Mpe kuhani mkuu Oniasi shukrani nyingi, maana ni kwa ajili yake tu BWANA kwa rehema zake amekujalia uzima.

34Wewe umepigwa kutoka mbinguni, basi, watangazie watu wote utukufu wa enzi ya Mungu. Wakiisha sema hayo walitoweka.

Heliodoro Aongoka

35Heliodoro akamtolea BWANA dhabihu, akaweka nadhiri kubwa sana kwake Yeye aliyemponya maisha yake. Akamwaga Oniasi kwa urafiki, akaondoka na jeshi lake kumrudia mfalme,

36akiwashuhudia watu wote matendo ya Mungu Mkuu aliyoyaona kwa macho yake mwenyewe.

37Mfalme alipomwuliza Heliodoro ni mtu wa namna gani afaaye kupelekwa Yerusalemu kwa safari ya pili,

38alisema, Kama una adui au mfanya fitina katika ufalme, mpeleke huko, naye, kama akijaliwa kurudi, atakuwa amepigwa sana, kwa sababu bila shaka mahali patakatifu hukaliwa na uweza wa Mungu.

39Yeye anayekaa juu mbinguni ana macho yake juu ya mahali pale akipalinda, nao wanaopakaribia kwa mabaya huwapiga na kuwaharibu.

40Ndizo habari za Heliodoro na ulinzi wa hazina.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya