The chat will start when you send the first message.
1Huyu Simoni aliyezitoa habari za ile fedha na kuisaliti nchi yake alianza sasa kumsingizia Oniasi, akisema kwamba ni yeye aliyempatia Heliodoro mambo hayo ya kuyachochea matata.
2Alithubutu hata kumshtakia fitina yule aliyekuwa mfadhili wa mji na mlinzi wa raia wenzake, mwenye kuzishika amri kwa bidii.
3Uadui huu ulipozidi sana, hata watu wakauawa na msiri mmoja wa Simoni, Oniasi alianza kufahamu hatari yake.
4Akaona ya kuwa Apolonio, mwana Menestheo, kiongozi wa Koele-Shamu na Foinike, alikuwa akiongeza ukorofi wa Simoni.
5Basi, alimwendea mfalme, si kwa kutaka kuwashtaki wenzake, ila kwa nia ya kuihifadhi hali njema ya watu wote, serikali na raia pia.
6Alijua ya kuwa, mfalme asipojitia mwenyewe katika mambo hayo, haitawezekana nchi ipate amani, wala Simoni hatauacha upuzi wake.
7Lakini Seleuko alipokufa, na Antioko aitwaye Epifani alipopokea ufalme wake, Yasoni, nduguye Oniasi, alimnyang'anya nduguye cheo chake cha kuhani mkuu,[#1 Mak 1:10]
8akiahidi, katika maombi yake kwa mfalme, kutoa talanta za fedha mia tano na sitini, na talanta themanini katika akiba nyingine.
9Zaidi ya hizo, aliahidi kutoa nyingine mia moja na hamsini kama akipewa ruhusa kufanya kiwanja cha michezo ya Kigiriki na chama chake cha vijana, na kuwaandika wenyeji wa Yerusalemu kuwa raia za Antiokia.
10Mfalme alipokubali jambo hilo, Yasoni, mara aliposhika kazi, alianza kushawishi wenzake wazikubali kawaida za Kigiriki.
11Aliziachilia mbali sharti za kifalme zilizotolewa kwa ajili ya Wayahudi, alizozipata Yohana, baba wa Eupolemo, alipotumwa kwa Warumi kutaka urafiki na kufanya mapatano; akazivunja kawaida halali za maisha akaingiza desturi mpya zilizokatazwa na sheria.[#1 Mak 8:17]
12Alifurahi kuweka kiwanja cha michezo ya Kigiriki chini ya ngome yenyewe; akawashawishi vijana walio bora wavae kofia za Kigiriki.
13Tamaa ya kufuatisha desturi za Kigiriki na mila za kigeni ilizidi mno, kwa sababu ya kufuru ya Yasoni – si kuhani kabisa huyu! –
14Hata makuhani hawakuifurahia tena ibada ya madhabahuni, bali walilidharau hekalu na kuziacha dhabihu ili kuyakimbilia mambo ya haramu kiwanjani, mara michezo ya kutupa diska ilipotangazwa.
15Hivyo walizifanya desturi zilizoheshimiwa na baba zao kuwa si kitu, wakahesabu mambo ya Kigiriki tu kuwa ndiyo bora.
16Kwa hiyo misiba mikubwa iliwapata, maana watu wale wale ambao walipenda sana kuzifuatisha desturi zao na kutaka kufanana nao sawasawa – hao waligeuka kuwa adui zao na kuwatesa.
17Kuzivunja amri za Mungu si jambo dogo; haya yataonekana kwa wakati wake.
18Basi, michezo iliyofayika kila miaka mitano ilipokuwa ikichezwa Tiro mbele ya mfalme,
19huyu mwovu Yasoni alituma wajumbe, Waantiokia wa Yerusalemu, kupeleka drakma elfu tatu za fedha kwa dhabihu itakayotolewa kwa Herakleo. Lakini hata wao walioipeleka fedha hiyo waliona haifai itumiwe kwa dhabihu, bali iwekwe kwa kazi nyingine.
20Hivyo, ingawa yule aliyeitoa alikusudia itumiwe kwa dhabihu kwa Herakleo lakini kwa shauri la hao wajumbe ilikwenda kwa mahitaji ya majahazi.
21Apolonio, mwana wa Menestheo, alipotumwa Misri kwenye kutawazwa kwake mfalme Filometo, Antioko alipata habari kwamba mfalme ameonesha uadui juu yake. Basi, kusudi ailinde nchi yake, alikwenda Yafa akashukia Yerusalemu.
22Akapokewa na Yasoni kwa heshima nyingi, akakaribishwa mjini kwa maandamano ya taa na mashangilio. Kisha alikwenda Foinike na jeshi lake.
23Miaka mitatu baadaye Yasoni alimtuma Menelao nduguye Simoni aipeleke fedha kwa mfalme na kutoa taarifa kadha wa kadha za mambo muhimu.
24Naye alipoingia mbele ya mfalme alijipendekeza kwake kwa maneno laini, hata akajipatia mwenyewe kazi ya kuhani mkuu, akiahidi kutoa talanta mia tatu za fedha zaidi kuliko Yasoni.
25Baada ya kupewa maagizo ya mfalme akarudi kwao, hana lolote la kuustahili ukuhani mkuu, bali ana moyo mkatili wa udhalimu na tabia ya hayawani mkali.
26Hivyo Yasoni, aliyemnyang'anya ndugu yake mwenyewe, alinyang'anywa yeye na mtu mwingine na kulazimika kuikimbilia nchi ya Waamoni.
27Basi, sasa Menelao alikuwa na mamlaka, lakini ile fedha aliyomwahidia mfalme hakuitoa kabisa,
28ingawa Sostrato, jemadari wa ngome, alimdai kila mara, maana ilikuwa kazi yake kutoza fedha za ufalme. Mwishowe waliitwa wote wawili mbele ya mfalme.
29Menelao alimwacha nduguye Lisimako awe wakili wake katika kazi ya kuhani mkuu, na Sostrato alimwacha Krete, jemadari wa askari za Kipro, awe badala yake.
30Wakati huo, watu wa Tarso na Malo walifanya uasi kwa sababu ilikusudiwa kuzitoa nchi zao zawadi kwa Antiokisi, suria wa mfalme.
31Kwa hiyo mfalme akaondoka kwa haraka kutengeneza mambo ya huko, akimwacha Androniko, mtu wa cheo kikuu, mahali pake.
32Menelao akaona amepata nafasi ya kufaa, akampa Androniko zawadi ya vyombo vya dhahabu alivyoviiba katika hekalu; vyombo vingine alikuwa amekwisha kuviuza Tiro na katika miji ya jirani.
33Oniasi, alipopata hakika ya jambo hilo, alimkemea kwa ukali, akikimbilia Dafne, mahali patakatifu pa sala karibu na Antiokia.
34Basi, Menelao alisema na Androniko faraghani, akimwomba amwue Oniasi. Androniko akamwendea Oniasi, akinuia kufanya hila, akapokewa naye kwa urafiki, akampa yamini yake. Hivyo, ingawa Oniasi alikuwa na shaka moyoni, aliweza kumvuta atoke katika mahali pa salama, na mara alimwua bila haki.[#Dan 9:26]
35Si Wayahudi tu, ila watu wa mataifa mengine pia, waliokasirishwa na kuchukizwa kwa kuuawa mtu huyu kwa udhalimu.
36Hata mfalme aliporudi kutoka katika nchi ya Kilikia, Wayahudi wa mjini pamoja na Wagiriki, waliolikirihi pia tendo hili la uovu, walisema naye, wakikaza ya kuwa Oniasi aliuawa pasipo haki.
37Antioko alisikitika sana, akaona huruma na kutoka machozi, kwa kuwa alijua maisha ya kiasi na utaratibu ya huyu marehemu.
38Akajaa hasira, akamnyang'anya Androniko vazi lake la urujuani, akamrarulia kanzu yake, akamtembeza mjini mwote mpaka mahali pale alipomtenda Oniasi uovu huo, akamwua pale pale. Hivyo Bwana alimpatiliza Androniko adhabu ya haki.
39Huko nyuma matendo mabaya mengi ya kuiba vyombo vitakatifu yametendwa na Lisimako kwa ridhaa ya Menelao. Hata habari hizi zilipojulikana watu walijipanga juu ya Lisimako, kwa kuwa vyombo vya dhahabu vingi vilikuwa vimetawanywa.
40Ikawa makutano walipofanya matata na kujaa hasira, Lisimako aliwapa silaha watu kama elfu tatu akawashambulia. Kiongozi wa kikosi hicho alikuwa mzee mmoja, Haurano, mwenye kuchakaa kwa umri na kwa akili pia.
41Watu walipoona ya kuwa Lisimako anawashambulia, wengine waliokota mawe, wengine kuni, na wengine konzi za majivu yaliyokuwako karibu, wakawatupia kwa wingi Lisimako na wale waliokuwa pamoja naye.
42Hivyo walijeruhi wengi na kuangusha wengine; wote wakakimbizwa, na yule mwizi wa hekalu yeye aliuawa karibu na hazina.
43Menelao alishtakiwa juu ya mambo hayo,
44hata mfalme alipofika Tiro watu watatu waliotumwa na baraza waliitetea kesi yao mbele yake.
45Lakini Menelao, akiona ameshindwa, alimpa Tolemayo mwana wa Dorimene fedha nyingi ili kumbembeleza mfalme.
46Tolemayo akamchukua mfalme kwenye roshani, kana kwamba wapunge hewa, akambembeleza hata akaghairi.
47Menelao, aliyekuwa asili ya matatizo yote, aliondolewa hatiani, na wale watatu, ambao hata kama wangalijitetea mbele ya washenzi wangalionekana kuwa hawana hatia, aliwahukumu kufa.
48Hao waliokuwa wateteaji wa mji na watu na vyombo vitakatifu, waliadhibiwa mara adhabu ile isiyo haki.
49Ndiyo sababu Watiro wengine, kwa jinsi walivyochukizwa na uovu huo, walitoa fedha nyingi ili kuwapatia maziko ya heshima.
50Naye Menelao, kwa sababu ya tamaa ya fedha ya mwenye mamlaka, aliendelea katika kazi yake, akijiongezea uovu na kujithibitisha kuwa msaliti mkubwa wa raia wenzake.