The chat will start when you send the first message.
1Basi, Yuda aitwaye Makabayo, na wale waliokuwa pamoja naye, walipitia katika miji kwa siri, wakiwaita jamaa zao na kuwachukua wale waliokuwa wamedumu katika dini ya Kiyahudi; hata wakakusanya watu wapatao elfu sita.
2Nao walikuwa wakimwitia BWANA, wakimsihi awatazame watu wanaoonewa na wote, na kulihurumia hekalu lililotiwa unajisi na watu waovu,
3na kuurehemu mji pia ulioachwa ukiwa, karibu na kuangushwa chini. Aiangalie damu inayomlilia,
4na kuyakumbuka maangamizi mabaya ya watoto wachanga wasio na hatia, na makufuru juu ya jina lake, na kuonesha jinsi anavyochukia uovu.
5Makabayo akiisha kuyaratibisha mambo ya kikosi chake, watu wa mataifa walimwona hashindiki. Maana sasa hasira ya Mungu ilikuwa imegeuka rehema.
6Alishambulia miji na vijiji bila kutazamiwa, akavichoma moto. Alijitwalia mahali penye maana akishinda adui si wachache.
7Kwa mashambulio hayo alitumia hasa wakati wa giza. Sifa za ushujaa wake zilivuma sana kila mahali.
8Basi Filipo, alipomwona huyu anaendelea kujichukulia ardhi kidogo kidogo na kuzidi kufanikiwa, alimwandikia Tolemayo, kiongozi wa Koele-Shamu na Foinike, kumtaka ampelekee mfalme msaada.
9Mara Tolemayo alimchagua Nikano mwana wa Patroklo, mmoja wa rafiki wakuu, akamtuma pamoja na watu wasiopungua elfu ishirini wa mataifa yote, ili aliharibu taifa lote la Wayahudi. Na pamoja naye alimpeleka Gorgia, jemadari mwenye mazoea mengi katika mambo ya vita.
10Lakini nia ya Nikano mwenyewe ilikuwa kuwauza Wayahudi utumwani apate kuzitimiza zile talanta elfu mbili mfalme alizodaiwa na Warumi.
11Basi, bila kukawia, alipeleka kwenye miji ya pwani kuwataka wanunue watumwa wa Kiyahudi, akiahidi kuuza watumwa tisini kwa talanta moja, asiitazamie hukumu itakayomwangukia kutoka kwa Mwenyezi.
12Yuda alipopata habari za mashambulio ya Nikano na kuwapa wafuasi wake habari za kukaribia jeshi lake,
13wale waliokuwa waoga na wenye shaka juu ya uamuzi wa haki wa Mungu walitoroka wakaenda zao.
14Wengine waliuza yote yaliyowasalia, wakamwomba Mungu awaokoe na yule mpotovu Nikano, aliyewauza kabla hajawakamata.
15Wakamsihi afanye hivyo, ikiwa si kwa ajili yao wenyewe, lakini kwa ajili ya maagano aliyoyafanya na babu zao, na kwa kuwa wameitwa kwa Jina lake takatifu la kutukuzwa.
16Makabayo alipowakusanya watu wake, jumla yao elfu sita aliwaambia wasiuogope wingi wa watu wa mataifa wanaowashambulia bila sababu, bali wapigane nao kwa ushujaa,
17wakiweka mbele ya macho yao mambo ya jeuri yaliyotendwa pasipo haki juu ya mahali patakatifu, na ukorofi uliofanyiwa mji uliodhihakiwa, na tena, utawala waliourithi kwa wazee wao ulivyoondolewa.
18Akasema, Wao, kwa upande wao, wanategemea silaha na matendo hodari; bali sisi tunamtegemea Mwenyezi Mungu ambaye, kwa mwinamo wa kichwa tu, aweza kuangusha si wao peke yao wanaotushambulia, ila na walimwengu wote pia.
19Kisha aliwakumbusha habari za msaada uliotolewa mara kwa mara zamani za wazee wao. Jinsi katika siku za Senakeribu, watu mia moja themanini na elfu tano walikufa;
20na katika mapigano yaliyofanyika huko Babeli juu ya Wagalata, walipigana watu elfu tano tu pamoja na Wamakedonia elfu nne, na Wamakedonia walipokuwa katika hatari ya kushindwa wale elfu nane waliwaangamiza wale elfu mia moja na ishirini, kwa msaada uliotoka mbinguni, wakateka nyara nyingi sana.
21Baada ya kuwatia moyo kwa maneno hayo, wawe tayari kufa kwa ajili ya sheria yao na nchi yao, aligawanya jeshi lake katika vikosi vinne,
22akawaweka ndugu zake Simoni, Yusufu na Yonathani pamoja naye kuwa wakuu wa vikosi, akimpa kila mtu watu elfu moja na mia tano;
23na pamoja nao Eleazari, ili akisome kitabu kitakatifu mbele ya watu. Akawapa neno la shime, “Msaada wa Mungu”, akatoka akiongoza kikosi cha kwanza, akazusha vita na Nikano.[#1 Mak 3:48]
24Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, waliua adui zaidi ya elfu tisa. Wakajeruhi na kuchangua wengi zaidi wa jeshi la Nikano, wakawafukuza wote.
25Wakaipata hata ile fedha ya watu waliokuja kuwanunua. Lakini, baada ya kuwafuatia kitambo, walisimama, kwa kuwa mchana unakwisha.
26Ilikuwa mkesha wa Sabato, ndiyo sababu hawakuweza kuwafuatia zaidi.
27Basi, baada ya kuzikusanya silaha za adui na kuwanyang'anya mali yao, walishughulika na mambo ya Sabato, wakimhimidi BWANA na kumshukuru sana aliyewaokoa siku hiyo na kuwawekea chanzo cha rehema zake.
28Sabato ilipokwisha, waliwagawia majeruhi na wajane na yatima sehemu ya nyara, na baki yake waligawana wao na watoto wao.
29Walipokwisha kufanya hivyo, walimsihi BWANA mwenye rehema akubali kupatanishwa kabisa na watumishi wake.
30Katika mapigano mengine na majeshi ya Timotheo na Bakide, waliua watu zaidi ya elfu ishirini, wakakamata ngome ndefu sana, wakapata mateka wengi mno. Wakawapa majeruhi na wajane na yatima, na wazee pia, sehemu sawasawa na sehemu zao.
31Wakazikusanya silaha za adui wakazipanga kwa uangalifu katika ngome kuu, na mali iliyobaki wakaileta Yerusalemu.
32Walimwua jemadari wa jeshi la Timotheo, mtu mwovu sana aliyewatenda Wayahudi mabaya mengi.
33Tena, walipokuwa wakiushangilia ushindi wao katika mji wa babu zao, waliwachoma moto wale walioiteketeza milango mitakatifu, pamoja na Kalisthene na wengine waliokuwa wamekimbilia kibanda kidogo kujisalimisha. Hivyo watu hao walipewa malipo ya haki ya kukufuru kwao.
34Naye Nikano, mwenye kulaaniwa mara tatu, aliyewaleta wachuuzi elfu moja kuwanunua Wayahudi,
35kwa msaada wa BWANA alidhiliwa na wale aliowahesabu kuwa si kitu kabisa. Ikambidi avue nguo zake rasmi na kwenda pekee kama mtumwa mtoro, akipitia njia za kandokando hata akafika Antiokia, bahati yake maangamizo ya jeshi lake tu!
36Yeye aliyeahidi kukusanya fedha iliyodaiwa na Warumi kwa kuwakamata watu wa Yerusalemu, alitangaza kwamba Wayahudi wana shujaa anayewapigania, na kwa sababu hiyo Wayahudi hawashindiki wakizifuata amri alizozitoa.