The chat will start when you send the first message.
1Ikatokea ya kuwa wakati huo Antioko alirudishwa kwa fujo kutoka nchi ya Shamu.
2Alikuwa ameingia katika mji wa Persepoli akajaribu kuiteka mali ya hekalu na kuushika mji. Mara watu wakachukua silaha wakamshambulia, hata Antioko alikimbizwa na wenyeji akalazimishwa kwenda zake kwa fedheha.
3Alipokuwa Ekbatana aliletewa habari za mambo yaliyompata Nikano na majeshi ya Timotheo.
4Akahamaki mno, akakusudia kuwalipa Wayahudi kisasi cha ubaya wa wale waliomkimbiza. Kwa hiyo alimwagiza mwendeshaji wa gari lake akaze mwendo bila kupumzika mpaka wafike huko. Hakika hukumu ya Mungu ilikuwa ikimfuatia! Maana alisema kwa kiburi. Nitakapofika Yerusalemu nitaujaza mji mizoga ya Wayahudi.
5Lakini BWANA aonaye yote, Mungu wa Israeli, alimpiga pigo la mauti lisiloonekana, na mara alipotaja maneno hayo alishikwa na maumivu makali ya tumboni yasiyotulizika, na uchungu wa ndani mkali sana.
6Ndiyo mateso ya haki kwake aliyekuwa ameumiza matumbo ya watu kwa mateso mengi ya kutisha!
7Lakini hakuacha jeuri yake kamwe. Kwa jinsi alivyofidhulika, hasira yake juu ya Wayahudi iliwaka kama moto. Akazidi kuhimiza mwendo. Ikawa gari lake linapokwenda kasi, aliponyoka akaanguka chini, akaumia vibaya sana katika viungo vyote vya mwili wake.
8Hata yeye aliyewaza kuyatawala mawimbi ya bahari – kwa jinsi alivyojivuna kupita kiasi cha binadamu – na kuweza kuvipima vilele vya milima kwa mizani, huyu sasa ameangushwa chini, na kuchukuliwa katika machela, ishara dhahiri kwa wote kwa uweza wa Mungu.
9Kisha funza walijaa katika mwili wa mtu huyu mkufuru, hata alipokuwa angali yu hai na katika maumivu na uchungu mwingi, nyama yake ikavurugika. Hata, kwa ajili ya uvundo, askari wote wa jeshi lake walimwonea kinyaa.
10Mtu huyu, ambaye zamani kidogo alijiona aweza kuzigusa nyota za mbinguni, sasa hana atakaye kumchukua kwa sababu ya mnuko wake.
11Basi, hapo kiburi chake kilianza kupungua, maana moyo wake ulivunjika; akapata ufahamu chini ya mapigo ya Mungu, hali maumivu yake yanazidi kila dakika.
12Hata yeye mwenyewe asipoweza kuistahimili harufu yake, alisema kwamba, Ni haki binadamu ajidhili chini ya Mungu, wala asijihesabu kuwa sawa naye.
13Zaidi ya hayo, huyu mwovu aliweka nadhiri kwa BWANA Mwenyezi, ambaye sasa haoneshi huruma kwake,
14akisema kama mji mtakatifu, ambao alikuwa akiuendea kwa haraka kuuangusha chini na kuufanya mahali pa mizoga, atauweka huru.
15Nao Wayahudi, ambao aliwahesabu kuwa hawastahili kuzikwa (ila kutupiwa pamoja na watoto wao kwa wanyama, na kuliwa na ndege), hao wote atawafanya sawasawa na raia wa Athene.
16Na hekalu takatifu, ambalo alikuwa kwanza ameliteka, aliahidi kulipamba kwa matoleo mazuri sana, na kurudisha vyombo vitakatifu, akivizidisha mara nyingi, na kulipa gharama za dhabihu kwa fedha yake mwenyewe.
17Hata pamoja na hayo yote, aliahidi kuifuata dini ya Kiyahudi, na kwenda kotekote kunako watu ili kuutangaza uweza wa Mungu!
18Lakini maumivu yake hayakupungua, kwa kuwa hukumu ya Mungu imempata kwa haki. Akakata tamaa, akaandika barua kwa Wayahudi kuwaomba hivi:
19Kwa Wayahudi washarifu, raia zake: Antioko, mfalme na jemadari mkuu, anawatakia furaha na afya na hali njema.
20Kama ninyi na watoto wenu hamjambo, na mambo yenu yanakwenda vizuri, namshukuru Mungu.
21Kwa kuwa tumaini langu limewekwa mbinguni, nakumbuka kwa mapenzi heshima yenu na nia yenu njema. Nilipokuwa nikirudi toka nchi ya Shamu nilishikwa na ugonjwa mkubwa, basi naona sina budi kuuangalia usalama wa raia zangu.
22Si kama nimekata tamaa juu ya hali yangu, la! Natumaini sana kupona katika ugonjwa wangu.
23Ila nakumbuka ya kuwa baba yangu alipopeleka jeshi lake katika nchi za juu alimtaja mrithi wake,
24ili, kama mambo yakitokea yasivyotazamiwa, au habari mbaya zikipatikana, watu wa nchi wajue ni nani aliyeusiwa ufalme, na kwa hiyo wasione wasiwasi.
25Zaidi ya hayo, najua ya kuwa wakuu wa nchi za jirani zinazopakana na ufalme wangu wanangoja nafasi yao na kuvizia yatakayotokea. Kwa hiyo nimemweka mwanangu Antioko awe mfalme. Mara nyingi, nilipokuwa nikienda wilaya za juu kwa haraka, nilimkabidhi kwenu na kumtakia urafiki wenu; nami nimemwandikia yaliyoandikwa hapa.
26Nawaonya, basi na kuwaomba, mzikumbuke fadhili mlizotendewa, katika nchi yenu na katika jamaa zenu, na kudumu wote katika nia yenu njema kwangu mimi na kwa mwanangu.
27Naamini ya kuwa yeye, kwa upole na kwa wema, atafuata shauri langu la kuwatendea kwa huruma.
28Hivyo yule mwuaji mkufuru, akipatwa na maumivu makali sana, kwa alivyowapatia watu wengine, alikufa milimani katika nchi ya kigeni kwa mauti ya kutisha mno.
29Filipo, mtu mkuu katika jumba la mfalme, alipeleka maiti nyumbani, kisha, kwa hofu ya mwana wa Antioko, alimwendea Tolemayo Filometo huko Misri.