The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yoabu akaambiwa, Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea.
2Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.
3Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedheha wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani.
4Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu![#2 Sam 15:30; 1 Sam 4:12; 2 Sam 18:33]
5Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wake zako, na roho za masuria wako;
6kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angalikuwa hai, na sisi sote tungalikuwa wafu leo, ingekuwa vyema machoni pako.
7Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa BWANA, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hadi sasa.[#Mit 14:28]
8Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme.[#Rut 4:1; 2 Sam 18:4,24; 2 Fal 14:12; 1 Fal 12:16]
Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake.
9Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii kwa sababu ya Absalomu.[#2 Sam 5:18; 1 Sam 17:1; 18:1; 2 Sam 15:14]
10Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lolote juu ya kumrudisha tena mfalme?
11Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake.
12Ninyi ni ndugu zangu, ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu; mbona basi ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme?[#Mwa 2:23; Amu 9:2; 2 Sam 5:1]
13Kisha mkamwambie Amasa, Je! Si wewe uliye mfupa wangu, na nyama yangu? Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, usipokuwa wewe jemadari wa jeshi mbele yangu daima mahali pa Yoabu.[#2 Sam 17:25; 1 Nya 2:16,17; 12:18; Rut 1:17; 1 Fal 19:2; 2 Sam 3:29,30; 8:16; 18:14]
14Akawainamisha mioyo watu wote wa Yuda, kama mtu mmoja; basi wakatuma kwa mfalme, Rudi wewe na watumishi wako wote.[#Amu 20:1; Zab 110:2,3; Mdo 4:32]
15Hivyo mfalme akarudi, akafika Yordani. Kisha watu wa Yuda wakaja Gilgali kumlaki mfalme, na kumvusha mfalme Yordani.[#Yos 5:9; 1 Sam 11:14,15]
16Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.[#2 Sam 16:5-13; 1 Fal 2:8,36,46]
17Na Watu elfu moja wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumishi wa nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumishi wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme.[#2 Sam 9:2,10; 16:1,2]
18Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema.
Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani.
19Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumishi wako kwa upotovu siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake.[#1 Sam 22:15; Zab 32:2; Rum 4:6,8; 2 Kor 5:19; 2 Sam 16:5,6; Mit 28:13; Mt 5:25; 2 Sam 13:33]
20Kwa kuwa mimi mtumishi wako ninajua ya kwamba nimekosa; kwa hiyo, tazama, nimekuja leo, wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu, kushuka ili nimlaki bwana wangu mfalme.[#2 Sam 16:5]
21Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA?[#Kut 22:28; 1 Sam 24:6; 26:9; 2 Sam 16:5,7,13; Mhu 10:20; Mdo 23:5; 2 Pet 2:10,11; Yud 1:8; #19:21 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]
22Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu yeyote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli?[#1 Sam 26:8; 2 Sam 16:10; Mt 8:29; 1 Sam 11:13]
23Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia.[#1 Fal 2:8,9,37,46]
24Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hadi siku hiyo aliporudi kwake kwa amani.[#2 Sam 9:1-13; 16:1-4]
25Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?[#2 Sam 16:17]
26Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumishi wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumishi wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumishi wako ni kiwete.
27Naye amenisingizia mimi mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako.[#2 Sam 16:3; Zab 15:3; 63:11; Mit 21:6; 26:28; Yer 9:4,5; 1 Sam 29:9; 2 Sam 14:17,20]
28Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumishi wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi?[#2 Sam 9:7-13]
29Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi.[#Kum 19:16-21; Zab 82:2; 101:1-8; Mit 29:4]
30Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake.
31Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani.[#2 Sam 17:27-29; 1 Fal 2:7; Ezr 2:61; Neh 7:63]
32Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, alikuwa na umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa.[#2 Sam 17:27]
33Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu.
34Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Nina miaka mingapi ya kuishi, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu?[#Mwa 47:9; Zab 39:4,5; Yak 4:14]
35Sasa nina miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumishi wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji wa kiume na wa kike? Kwa nini basi mtumishi wako azidi kumlemea bwana wangu mfalme?[#Zab 90:10; Mhu 12:3-6]
36Mtumishi wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii?
37Niache nirudi basi, mimi mtumishi wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumishi wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako.[#1 Fal 2:7; Yer 41:7]
38Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako.
39Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarudi nyumbani kwake.[#Mwa 31:55; 14:19; Kut 39:43; Yos 22:6; 1 Sam 2:20]
40Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli.
41Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye?[#2 Sam 19:15]
42Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ni wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yoyote?[#2 Sam 19:12; Rut 4:12,18-22; 1 Nya 2:3-15; Zab 78:68,70; Mt 1:1-6]
43Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, msitake ushauri wetu kwanza katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.[#1 Fal 11:30,31; Amu 8:1; 12:1]