2 Timotheo 1

2 Timotheo 1

Salamu

1Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu;

2kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.[#Mdo 16:1]

Shukrani na mahimizo

3Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana.[#Mdo 23:1; 24:16; Flp 3:5]

4Nikiyakumbuka machozi yako, natamani sana kukuona, ili nijawe na furaha;

5nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika nyanya yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.[#Mdo 16:1]

6Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.[#1 The 5:19; 1 Tim 4:14]

7Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.[#Rum 8:15]

8Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa uweza wa Mungu;[#Rum 1:16]

9ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake mwenyewe na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu kabla ya wakati kuanza,[#Tit 3:5]

10na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutoharibika, kwa ile Injili;[#Rum 16:26; Ebr 2:14; 1 Kor 15:55,57]

11kwa ajili ya Injili hiyo niliwekwa niwe mhubiri, mtume na mwalimu.[#1 Tim 2:7]

12Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, lakini sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.

13Shika mfano wa mafundisho ya kweli uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.[#1 Tim 6:3; Tit 2:1]

14Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.[#1 Tim 6:20]

15Waijua habari hii, ya kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene.[#2 Tim 4:16]

16Bwana awape rehema wale walio wa jamaa wa Onesiforo; maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu;

17bali, alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii na kunipata.

18Bwana na amjalie ili kwamba apate rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana.[#Yud 1:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya